Waziri wa Nchi - Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji Mhe.Angellah Kairuki amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania Sarah Cooke machi 13, 2019 katika Ofisi zake Jijini Dodoma.

Lengo la mazungumzo hayo ilikuwa kujadili masuala mbalimbali ikiwemo namna ambavyo Serikali ya Uingereza inaweza kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kusaidia kutekeleza vipaumbele vya kuboresha uwekezaji na mazingira ya biashara Nchini, ikiwa ni kuunga mkono kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa hafla ya kuukaribisha mwaka mpya wa 2019 aliyowaandalia Mabalozi na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa nchini (Sherry party) iliyofanyika Ikulu tarehe 08 Machi, 2019

“Tumekutana wakati sahihi kwa kuzingatia kauli ya Mheshimiwa Rais aliyotoa katika hafla ya kukaribisha mwaka, kwamba mwaka 2019 ni Mwaka wa Uwekezaji kwa Tanzania hivyo Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa Nchini watumie fursa hiyo kukaribisha wawekezaji kutoka nchi zao na kuwekeza Nchini,”alisema Kairuki

Katika kuelezea vipaumbele vya kuboresha uwekezaji na mazingira yake nchini, Waziri Kairuki aliishukuru Serikali ya Uingereza kwa misaada mbalimbali ya maendeleo inayoitoa katika sekta mbalimbali kwa Serikali ya Tanzania.

“Serikali ya Tanzania inajivunia kuwa na mdau wa maendeleo kama Uingereza ambaye uhusiano wake na Tanzania umeendelea kuimarika na kushuhudia Uingereza kuwa moja ya nchi zenye uwekezaji mkubwa nchini Tanzania,”alisistiza Kairuki

Aidha, Waziri alimuomba Balozi Cooke kuisadia Tanzania katika gharama za utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mifumo ya Udhibiti wa Biashara Nchini kwa kutoa fedha na utaalam unaotokana na uzoefu kutoka nchi zilizofanikiwa katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji na ambazo zinafanya vizuri katika wepesi wa kufanya biashara.

Waziri Kairuki alibainisha miongoni mwa jitihada za Serikali katika kutatua changamoto zinazowakabili wawekezaji wa Uingereza nchini ni pamoja na kuandaa kikao cha kusikiliza na kutatua changamoto za wawekezaji hao kitakachohusisha Wizara na Taasisi zote zinazohusika na masuala ya uwekezaji na biashara na kukubaliana kifanyike mapema iwezekanavyo.

Aidha, aliishukuru Serikali ya Uingereza kwa kuendelea kuiunga mkono Tanzania na kuwataka kuendeleza urafiki huo na ushirikiano kwa kuwekeza zaidi katika maeneo ya vipaumbele alivyobainisha awali.

Kwa upande wake Balozi wa Uingereza Nchini Tanzania, Sarah Cooke alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) kwa kuongeza nguvu ya ufuatiliaji na utatuzi wa changamoto zinazokabili uwekezaji nchini ili kuleta mabadiliko.

“Nampongeza Mhe.Rais kwa kuboresha mazingira ya biashara na Uwekezaji na jitihada zake zimesaidia kurudisha imani ya wawekezaji waliopo na wenye nia ya kuwekeza Tanzania,”alisisitiza Cooke.

Aliongeza kuwa, Serikali ya Uingereza imepokea maombi ya Mhe. Kairuki ya kusaidia kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara nchini na kuyafanyia kazi ikiwa ni pamoja na kuendelea kutoa misaada ya maendeleo na kuimarisha mahusiano yaliyopo baina ya ya nchi hizo mbili.

=MWISHO=