MHAGAMA: TUMIENI NGUVUKATIKA KUWALAZIMISHA WANANCHI KULIMA KUKABILIANA NA NJAA

WAZIRI wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge Vijana Ajira Kazi na Watu Uenye Ulemavu Jenista Mhagama, amemwagiza mkuu wa wilaya ya Mpwapwa kuhakikisha anatumia nguvu katika kuwalazimisha wananchi kulima ili kukabiliana na tatizo la njaa ambalo limekuwa likiukabili mkoa wa Dodoma.

Mhagama aliyasema hayo Tarehe 18 Juni, 2016, wakati alipofanya ziara ya kuwatembelea wakulima wa zao la mhogo ambao walihamasishwa kulima zao hilo linalostahimili ukame ili kukabiliana na njaa.

Alisema kuwa katika kuhakikisha tatizo la njaa linakwisha mkuu wa wilaya huyo anatakiwa kuweka mikakati mipya ambayo itakuwa na tija katika kuhakisha njaa inakwisha wilayani hapo.

Aidha alisema kuwa uongozi wa wilaya hiyo unatakiwa kubuni mikakati mipya tofauti na ile ya zamani ili kutumia nguvu kazi iliyopo katika kushiriki kilimo na kusaidia kuondokana na tatizo la njaa.

“Kama mtaendelea na mikakati yenu ya kila siku tatizo la njaa halitakwisha mnatakiwa hivi sasa kutumia nguvu lazimisheni wananchi walime mazao yanayostahimilimi ukame kama mihogo na mtama”alisema Mhagama.

Alisema kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia kitengo cha maafa ilitoa sh. Milioni 35 kwajili ya kununua mbegu za mihogo na mtama kwa ajili ya wananchi ya wilaya hiyo waliokuwa wanakabiliwa na baa la njaa.

Aliongeza kuwa kwa namna alivyo jionea maendeleo ya baadhi ya wakulima waliolima mihogo wameweza kujikwamua kiuchumi na kuondokana na baa la njaa kwa kipindi kirefu.

“Kwa hali hii basi sisi kama Ofisi ya Waziri Mkuu hatuna haja ya kuendelea kuleta chakula cha msaada tena huku kwakuwa zao la mihogo ambalo sisi tulileta mbegu imeweza kuwasaidia wakulima kuondokana na njaa lakini pia wengine wamejenga nyumba na kuezeka kwa bati”alisema Mhagama.

Aidha Mhagama alisema kuwa kutokana na wakulima hao kuonyesha mafanikio uongozi wa wilaya hiyo uongeze bidii katika kuhamasisha kilimo cha zao hilo.

“Inabidi muwe na hata sheria ambazo zitawalazimisha wananchi kila mmoja wao kulima heka mbili za muhogo na mbili zingine za mtama na katika hili msimbembeleze mtu tumieni nguvu ili kuweza kuondokana na na tatizo la njaa mkoani hapa”alisema.

Hatahivyo alimwagiza ofisa kilimo wa wilaya Yustina Munishi , kuhakisha idadi ya wakulima inaongezeka tofauti na iliyopo hivi sasa.

“Hadi mwakani tarehe kama ya leo nataka kuja kukaguma mashamba zaidi ya 300 na kama sitayakuta kwa idadi hiyo utakuwa huna kazi afisa kilimo”alisema.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Mpwapwa Mohamed Utaly alisema kuwa watakipanga kuhamasisha kilimo cha zao hilo la muhogo ambalo limeonekana kuwa mkombozi wa njaa.

“Katika kipindi kijacho cha kilimo kupitia mikakati yetu tutahakikisha kila kaya inalima heka mbili za mhogo na heka mbili za mtama ili kuondokana na baa la njaa ambalo limekuwa likiikabili wilaya hiyo kila mwaka”alisema Utaly.

Naye mmoja wakulima hao Bahati Mtonyi,alisema kuwa kupitia zao hilo la muhogo ameweza kujenga nyumba na kujilipia ada kila mwaka kiasi cha sh. 600.000.

Mwisho.