WAZIRI MKUU AWAOMBA WANANCHI WAWE WATULIVU

*Awashukuru kwa kusaidia zoezi la uokoaji tangu mwanzo

WAKATI zoezi la uopoaji miili ya watu waliopoteza maisha kwenye ajali ya MV Nyerere likiendelea, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaomba Watanzania waendelee kuwa watulivu.

Waziri Mkuu ambaye aliwasili Mwanza jana jioni (Ijumaa, Septemba 21, 2018) alikwenda moja kwa moja kwenye kisiwa cha Ukara kuwapa pole wafiwa na kuangalia kazi ya uokoaji inavyoendelea. MV Nyerere ilipinduka juzi mchana wakati ikitoka bandari ndogo ya Bugolora, kisiwani Ukerewe kurejea kisiwa kidogo cha Ukara.

Waziri Mkuu ambaye yuko hapa Mwanza akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli alisema: “Mheshimiwa Rais amepokea tukio hili kwa mshtuko mkubwa na anawapa pole sana.”

“Tunaungana nanyi kwa huzuni hii kubwa ya kupoteza ndugu zetu. Tunawaomba wananchi muendelee kuwa watulivu na Serikali itatoa taarifa mwishoni mwa zoezi hili,” alisema.

Alisema Serikali imeshaunda kamati ya uchunguzi ambayo itafanya uchunguzi wa kina juu ya tukio hilo. “Imeshaelezwa kuwa meli hii ilikuwa na uwezo wa kubeba tani 25 za mizigo na abiria 100, lakini kwa idadi ya waliopoteza maisha ni dhahiri kuwa watu walizidi. Serikali haiwezi kufumbia macho jambo hili na tumeunda kamati iweze kufanya uchunguzi wa kina tatizo hasa lilikuwa ni nini,” alisisitiza.

Alisema Serikali ilishanunua injini mbili na kuifanyia ukarabati meli hiyo kwa hilo ilikuwa na uwezo wa kufanya kazi.

Alitumia fursa hiyo kuwashukuru wananchi wote waliojitokeza kusaidia kazi ya uokoaji tangu ajali hiyo ilipotokea. Pia aliwashukuru watumishi wa kituo cha afya na timu nzima inayofanya kazi ya uokoaji na uopoaji wa miili kwa kazi kubwa waliyoifanya.

-ends-