SERIKALI KUACHANA NA UAGIZAJI MAFUTA YA KULA - WAZIRI MKUU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imedhamiria kuimarisha kilimo cha mbegu za mafuta ili Tanzania iachane na uagizaji wa mafuta ya kula kutoka nje.

Amesema malengo ya kampeni hiyo ni kuhakikisha kuwa mkoa wa Kigoma na maeneo mengine yenye fursa ya kulima zao la chikichi yanaimarisha kilimo hicho. “Hivi sasa, nchi yetu inatumia takribani Dola za Marekani milioni 294 kila mwaka kwa ajili ya kuagiza mafuta hayo.”

Ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Septemba 14, 2018) katika hotuba yake aliyoitoa wakati wa kuahirisha Mkutano wa 12 wa Bunge jijini Dodoma. Bunge limeahirishwa hadi Novemba 6, mwaka huu.

Amesema sambamba na azma ya Serikali ya kuweka mkazo katika kusimamia uzalishaji na masoko ya mazao makuu matano ya biashara ambayo ni pamba, kahawa, korosho, chai na tumbaku, Serikali imedhamiria pia kupanua wigo kwenye mazao mengine muhimu ikiwemo chikichi, alizeti na ufuta ili kukidhi uzalishaji wa mbegu za mafuta nchini.

“Katika kutekeleza azma ya Serikali, kuhusu kuongeza uzalishaji wa mafuta ya kula nchini, tarehe 28 Agosti, 2018 nikiwa mkoani Kigoma nilizindua kampeni maalumu ya kuendeleza zao la chikichi ambalo kwa sasa linatambulika kama zao kuu la sita la kipaumbele,” amesema.

Amesema ili kuhakikisha nchi inajitosheleza kwa mahitaji ya mafuta ya kula, Serikali imeweka mikakati ya kuendeleza zao la chikichi kwa kuanzisha kituo cha utafiti wa zao la chikichi katika eneo la Kihinga, mkoani Kigoma.

“Serikali imeandaa mpango mkakati wa uzalishaji wa miche bora ya chikichi milioni 20 ifikapo mwaka 2021. Kwa kuanzia, mwaka 2018/2019, Serikali inakusudia kuzalisha miche bora ya chikichi milioni 10 ambayo itasambazwa kwa wakulima,” amesema.

Aidha, Waziri Mkuu amesema Serikali pia imeandaa mpango mkakati wa miaka mitano wa utafiti wa mbegu bora ili kuongeza tija kutoka tani 1.6 hadi kufikia tani 4.0 za matunda ya chikichi kwa hekta kwa mwaka.

Amesema Serikali imeweka mazingira mazuri ya kuvutia uwekezaji na matumizi ya teknolojia ya kisasa kwa ajili ya uchakataji zao la chikichi na imepanga kusimamia vituo vikuu vya uzalishaji vya gereza la Kwitanga, Ilagala na JKT Bulombora.

Amewataka Watanzania wachangamkie fursa ya kilimo cha zao la chikichi ili nchi iweze kujitosheleza kwa mafuta ya kula na ziada kuuza nje. “Nitoe rai pia kwa wawekezaji, waje kuanzisha viwanda vya kuchakata chikichi na mazao yake,” amesisitiza.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali kwa upande wake, inaimarisha taratibu za uingizaji wa sukari na mafuta ya kula kwa kuweka madaraja na usimamizi makini.

Ameitaka Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo wakamilisha jukumu hilo kwa wakati.

“Pia, naagiza vyombo vya dola viongeze ushirikiano na mamlaka husika ambazo ni TRA, TFDA, Bodi ya Sukari na TBS ili kudhibiti uingizaji holela wa sukari na mafuta ya kula ikiwa ni pamoja na kuziba mianya ya magendo,” amesema.

-ends-