IDADI YA WANAWAKE WALIOFARIKI AJALI YA MV NYERERE NI KUBWA KULIKO WANAUME

*Wanawake ni 126, wanaume 71, watoto wa kike 17 na wa kiume ni 10

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe amesema hadi mazishi ya kitaifa yanafanyika, jumla ya watu 224 walikuwa wamepoteza maisha kutokana na ajali ya MV Nyerere iliyotokea Septemba 20, mwaka huu.

Akitoa taarifa ya tukio zima mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye ameongoza mazishi hayo leo (Jumapili, Septemba 23, 2018), Waziri Kamwelwe amesema wanawake waliopoteza maisha jumla yao ni 126, wanaume 71, watoto wa kike ni 17 na wa kiume ni 10.

Awali, kabla ya ibada kuanza, idadi ya waliopoteza maisha ilikuwa 223 lakini mwili mmoja wa mwanamke ulipatikana mchana huu na kufanya idadi yao kufikia 224.

Amesema mipango ya Serikali ya muda mrefu ni kujenga kivuko kikubwa ambacho kitakuwa kikifanya safari zake kati ya bandari ndogo ya Bugolora iliyopo kisiwa cha Ukerewe na kisiwa kidogo cha Ukara.

“Tumefanya utafiti kwenye visiwa vidogo vyote na kubaini kuna mialo zaidi ya 140. Hii itaimarishwa ili iweze kufikika na vyombo vya usafiri ambavyo ni imara,” amesema.

Akitoa taarifa kuhusu tukio zima, Waziri Kamwelwe amesema ajali hiyo ilitokea Septemba 20, saa 7:48 mchana na taarifa zilifikishwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza saa 8:10 mchana ambapo yeye na Kamati ya Ulinzi ya Usalama ya Mkoa walikimbia kuwahi eneo la tukio na kukuta watu watu 40 wameshaokolewa na wakazi wa kisiwa cha Ukara.

Amesema meli ya MV Nyerere ilijengwa mwaka 2004 na kufanyiwa ukarabati mkubwa mwaka 2013. “Julai mwaka huu, tulinunua injini mbili mpya na gear box zake,” amesema.

Mapema, akizungumza kwenye ibada hiyo ya mazishi, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, Bw. George Nyamaha aliiomba Mamlaka ya Usafirishaji Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) iongeze watumishi kwenye visiwa hivyo ili waweze kudhibiti matukio ya ujazaji abiria kwenye vyombo vya usafiri majini.

“Tunashukuru hapa Ukerewe tumeletewa mtendaji mmoja, lakini hawezi kufanya chochote kwa sababu hana hata chombo cha usafiri. Tuna visiwa 38 kwenye wilaya hii na kati ya hivyo, visiwa 34 kuna watu wanaishi ambao wanalazimika kusafiri ili kujipatia mahitaji yao. Sasa huyu mtendaji mmoja atafikaje kote huko?” alihoji.

Akifafanua adha ya usafiri kwenye visiwa hivyo alisema: “Ilugwa kuna watu zaidi ya 10,000 na huwa inachukua saa nne kutoka huko hadi kufika Nansio (makao maku ya wilaya ya Ukerewe). Watu wanatumia boti tu na ajali ni nyingi sana. Pia tunahitaji usafiri wa uhakika kutoka Kitale hadi Kweru ambako kuna wakazi zaidi ya 20,000” alisema.

Wakati huohuo, Mbunge wa Ukerewe, Bw. Joseph Mkundi ambaye ni mzaliwa wa kisiwa cha Ukara, amesema wilaya ya Ukerewe inahitaji kupatiwa usafiri wa uhakika baina yake na visiwa jirani ili kuepuka maafa kama hayo yasitokee.

“Ukerewe tunahitaji chombo kizuri cha uhakika kinachoweza kustahimili maafa kama haya yasitokee. Ni kipindi kigumu kwetu wana Ukara, niombe tushikamane,” alisema.

-ends-