OCD KYERWA ATUHUMIWA KUSINDIKIZA KAHAWA YA MAGENDO

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi awafuatilie kwa karibu Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Kyerwa, Justin Joseph pamoja na askari wake wanaodaiwa kusindikiza kahawa za magendo.

Ametoa agizo hilo leo (Jumapili, Oktoba 7, 2018) baada ya kukagua kiwanda cha kukoboa kahawa cha Nkwenda wilaya Kyerwa katika siku ya pili ya ziara yake ya kikazi mkoani Kagera. Katika ziara hiyo Waziri Mkuu ameambatana na mkewe Mama Mary Majaliwa.

“Askari polisi wa wilaya ya Kyerwa pamoja na OCD wao wanatuhumiwa kusindikiza kahawa inayosafirishwa kwa njia ya magendo kwenda nchi ya jirani kupitia njia mbalimbali zisizo rasmi zikiwemo za Kumisongo, Kashaijo na Omukatoma.”

Waziri Mkuu amesema ni jambo la hatari kama askari polisi wanasindikiza kahawa inayouzwa kwa magendo, hivyo ameagiza jambo hilo lidhibitiwe haraka. “Ni marufuku kupeleka kahawa nje ya nchi kwa njia ya magendo na polisi msishiriki katika biashara ya butura,’” ameonya.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema kuanzia msimu ujao wa kahawa, minada yote ya kahawa inayozalishwa mkoani Kagera itafanyika ndani ya mkoa huo badala ya kufanyika Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Waziri Mkuu amesema minada hiyo ikifanyika mkoani humo itawawezesha wakulima kulipwa fedha zao ndani ya muda mfupi na pia itapunguza makato yasiyokuwa ya lazima ambayo yamekuwa kero kwa wakulima.

“Wanunuzi watafuata kahawa ilipo, utaratibu huu utawawezesha wakulima kulipwa fedha zao kwa wakati. Mnada ukifanyika katika maeneo ya uzalishaji utamuwezesha mkulima kujua bei, tofauti na unavyofanyika Moshi kwani ni rahisi mkulima kuibiwa.”

Waziri Mkuu amewataka wananchi waendelee kuiamini Serikali kwani imedhamiria kuwaletea maendeleo na kuhakikisha wakulima wanasaidiwa kutafutiwa masoko ya mazao yao.

-ends-