RAIS MAGUFULI ATAKA WIZARA YA KILIMO IJITATHMINI

*Majaliwa aagiza Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho arudishwe wizarani

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ameitaka Wizara ya Kilimo ijitathmini kutokana na jinsi suala la mauzo ya zao la korosho linavyoendelea pamoja na utendaji wa Bodi ya Korosho Tanzania.

Agizo la Rais Magufuli limetolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika kikao chake na wakuu wa mkoa inayolima korosho kilichofanyika leo (Ijumaa, Oktoba 26, 2018) kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi.

Pia Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Kilimo imrudishe wizarani Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Prof. Wakuru Magigi kwa vile Serikali hairidhishwi na utendaji wake.

“Haturidhishwi na utendaji wa Bodi, umekiuka maelekezo ya msingi ya Serikali katika kusimamia mfumo mzima wa zao la korosho na kusababisha kuvurugika kwa minada.”

Kutokana na hali hiyo, Waziri Mkuu amesema kuanzia leo, Serikali imesitisha minada yote ya korosho nchini na kuwataka wakulima wawe watulivu wakati suala hilo likishughulikiwa.

Kaimu Mkurugenzi huyo wa Bodi ya Korosho analalamikiwa kwa kufanya kazi bila ya kushirikisha ushirika wa zao hilo na kutotambua mamlaka zilizowekwa kisheria kama vile Mkuu wa Mkoa.

Mbali na malalamiko hayo, pia anadaiwa kuendesha operesheni kwa kutumia silaha na askari dhidi ya viongozi wa ushirika kinyume cha taratibu za nchi.

Hivyo, Waziri Mkuu amewaagiza Makamanda wa Polisi wa mikoa ya Lindi na Mtwara wahakikishe gari lenye namba T 814 DDM pamoja na dereva wake linatafutwa popote.

Waziri Mkuu amesema gari hilo ndilo linalodaiwa kutumika katika kuwakamata viongozi wa ushirika waliokuwa wanawasimamia wananchi waliokataa kuuza korosho kwa bei ndogo.

Amesema baada ya dereva wa gari hilo kukamatwa, ahojiwe na aeleze askari hao alikuwa anawatoa wapi na ni nani aliyemtuma. Ameagiza askari wote waliohusika watafutwe.

“Bodi imekuwa ikiwatisha na kuwalazimisha wakulima na viongozi wa ushirika wakubali kuuza korosho kwa bei ya chini jambo ambalo Serikali haiwezi kulikubali.”

Waziri Mkuu amesema Serikali haiwezi kulifumbia macho suala hilo kwa sababu limekuwa likiipaka matope kwani Mkurugenzi huyo alikuwa anaingiza askari katika mikoa hiyo bila ya mamlaka kuwa na taarifa.

Kadhalika, Waziri Mkuu ameitaka Wizara ya Kilimo isikae kimya pindi zinapotokea changamoto kama hizo na badala yake watoe taarifa mapema. “Mambo kama haya yanatokea halafu wizara mmekaa kimya tu.”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Rais Dkt. Magufuli anawapongeza wakulima wa korosho kwa uamuzi wao wa kukataa kuuza zao hilo kwa bei ndogo na kwamba yuko pamoja nao.

“Rais Dkt. Magufuli ameitaka Wizara ya Kilimo ijitathmini katika suala la mauzo ya zao la korosho linavyoendelea,” amesema Waziri Mkuu.

Pia Waziri Mkuu amesema Rais Dkt. Magufuli ana taarifa kwamba kuna baadhi ya watendaji Serikalini wanatumia vibaya jina lake na kuahidi kwamba wahusika wote lazima watachukuliwa hatua.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Bw. Gelasius Byakanwa na Mkuu wa mkoa wa Lindi, Bw. Godfrey Zambi walilalamikia kitendo cha Prof. Magigi kuvuruga mfumo wa uuzaji wa korosho.

Pia walisema licha ya kumshauri kiongozi huyo juu ya namna bora ya kuendesha minada ya uuzaji wa korosho, hakuwasikiliza na kwamba hakuwa tayari kushirikiana nao na pia alikuwa akidharau mamlaka zao.

Pia alikuwa akiingiza askari na kuwatisha na kukamata viongozi wa ushirika bila ya wao kujua jambo ambalo walisema limezua taharuki kwa watendaji wa ushirika.

-ends-