SERIKALI YATOA SIKU NNE KWA WANUNUZI WA KOROSHO

*Yawataka waandike barua wakionesha tani wanazohitaji na lini watazichukua

*Yasema zaidi ya hapo haitoruhusu kampuni yoyote kununua korosho tena

SERIKALI imetoa siku nne kwa wanunuzi wote 35 waliojiandikisha kununua korosho wawe wamepeleka barua katika Ofisi ya Waziri Mkuu wakionesha kiasi cha tani wanazohitaji na lini watazichukua.

“Wanunuzi waliojiandikisha wakiwemo na wale wote ambao wamekuwa wananunua kwenye minada lakini kwa kiasi kidogo, wahakikishe ndani ya siku hizo nne kuanzia leo, Ijumaa hadi Jumatatu saa 10 alasiri, wawe wameleta barua na ofisi yangu ipo wazi saa 24.”

Hayo yamesemwa leo (Ijumaa, Novemba 9, 2018) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akitoa tamko la Serikali kuhusu ununuzi wa zao la korosho, ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma.

Amesema baada ya siku hizo kwisha, Serikali italazimika kufuta usajili kwa wote waliojisajili kununua zao hilo kwa sababu walikubaliana kwenda kununua lakini hali inayoonekana sasa ni kama kumkomoa mkulima kitu ambacho imesema haikubaliani nacho.

“Mwenye nia ahakikishe katika siku hizo nne iwe ndio mwisho wa kununua korosho na waandike barua kwani ofisi yangu ipo wazi saa 24, wana nafasi ya kuleta barua wakati wowote wakionesha nia yao na kiwango wanachokihitaji ili tuweze kuratibu. Zaidi ya hapo Serikali haitoruhusu kampuni yoyote kununua korosho tena,” amesisitiza.

Hatua hiyo imekuja baada ya zao la korosho kuendelea kununuliwa kwa bei ya chini na idadi ya wanunuzi kuwa ndogo huku tani zinazonunuliwa nazo pia zikiwa ni kidogo.

Waziri Mkuu amesema kwenye msimu wa ununuzi wa korosho wa mwaka huu, walishuhudia kusuasua kwa minada, ambapo Serikali ilikutana na wanunuzi wa korosho katika kikao kilichoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli ambapo walikubali kununua kwa bei inayoanzia sh. 3,000 na kuendelea.

“Mjadala ulikuwa wa wazi na wafanyabiashara wenyewe walipendekeza bei ambayo ilikuwa inaanzia sh. 3,000, hata hivyo baada ya kikao hicho ununuzi katika minada umeendelea kusuasua na hata tani zilizokuwa zikinunuliwa zilikuwa kidogo sana. Sisi tunaiona hali hii kama mgomo baridi ambao si sawa sawa sana kwani malengo yetu sisi na sekta binafsi ni kumfanya mkulima apate bei nzuri.”

“Hali hii haifurahishi kwa sababu Serikali imedhamiria kuboresha mazao yanayolimwa na wakulima kwa kuwasaidia kuanzia katika hatua za utayarishaji wa mashamba, upatikanaji wa pembejeo na masoko ili waweze kunufaika na kilimo na kupata tija kutokana mazao yao,” amesema.

Waziri Mkuu amesema baada ya kugundua bei imekuwa tatizo, Serikali ilifanya jitihada za kupeleka wataalamu wake katika masoko makuu duniani na kupata bei halisi ambayo bado inatosha kumlipa mkulima sh. 3,000.

Amesema uzalishaji wa mwaka huu ni mdogo ukilinganisha na msimu wa mwaka jana. “Msimu wa mwaka jana, uzalishaji ulikuwa zaidi ya tani 370,000 na mwaka huu zinatarajiwa kuvunwa tani zaidi ya 200,000, hivyo wafanyabiashara wanao uwezo kununua korosho zilizopo,” amesema.

Hata hivyo, Serikali imewataka wananchi hususani wakulima wa korosho nchini waendelee kuwa wavumilivu na watulivu wakati ikiendelea kushughulikia suala hilo.

-ends-