WAZIRI MKUU ASIKITISHWA NA WIZI KWENYE MRADI WA NYUMBA WA NSSF DEGE

*Aagiza wakurugenzi wakuu wa NSSF, AZIMIO, Kamishna TRA wakutane

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametembelea mradi wa nyumba unaojengwa kwa ubia kati Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na kampuni ya Azimio Housing Estate Limited katika eneo la Dege Beach Kigamboni na kusema kuwa amesikitishwa na uharibifu wa mali na wizi unaendelea kwenye eneo hilo.

Amewaagiza Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. William Erio na Mkurugenzi wa Mkuu kampuni ya Azimio Housing Estate Limited, Bw. Mohammed Iqbal wakutane na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Charles Kichere ili wajadiliane namna ya kudhibiti wizi na kuimarisha ulinzi.

Waziri Mkuu alitembelea eneo la mradi huo jana jioni (Jumatatu, Novemba 12, 2018) ambapo baada ya kufika katika eneo ambalo linajengwa nyumba zaidi ya 7,000 alionesha kusikitishwa na uharibifu wa mali na wizi unaoendelea na kutoa maagizo kwa wahusika.

“Kuna mpango gani wa ulinzi hapa? Mali zinaendelea kuibiwa, tutakuja kuanza ujenzi hapa na kukuta hakuna mali hata moja. Ulinzi lazima uimarishwe pande zote mbili za mradi huu, eneo la ujenzi na eneo la kuhifadhia vifaa vya ujenzi,” alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Erio alimuahidi Waziri Mkuu kwamba atahakikisha wanakutana na Kamishna wa TRA na Mkurugenzi Mkuu wa Azimio ili wajadili namna ya kuimarisha ulinzi na kutatua changamoto ya wizi unaoendelea katika eneo hilo.

Mkataba kati ya NSSF na Azimio Housing Estate Limited (AHEL) ulisainiwa mwaka 2012 na kuanzisha kampuni ya hodhi ya “Hifadhi Builders” ambapo AHEL ilikuwa na asilimia 55 na NSSF asilimia 45. Katika asilimia 55 za AHEL, asilimia 20 ni ardhi iliyotoa kwenye mradi huo na asilimia 35 ilipaswa iwe ni fedha taslimu.

Mradi huo ulihusisha ujenzi wa nyumba 7,460 ambapo jumla ya gharama za mradi zilikadiriwa kuwa dola za Marekani 653,436,675 ambazo kati yake ujenzi ungegharimu dola 544,530,562 wakati gharama za ardhi zingekuwa dola 108,906,113. Kwa fedha za Tanzania, mradi pamoja na ardhi ungegharimu sh. trilioni 1.5.

Hadi kufikia Juni 2018, NSSF walishailipa kampuni ya Hifadhi Builders dola za Marekani 133,838,662.2 kama mchango wake kwenye ujenzi wa mradi huo ambazo ni sawa na sh. bilioni 305.8 wakati kampuni ya Azimio ikitoa dola za Marekani 5,500,000 sawa na sh. bilioni 12.6 tu.

-ends-