MAJALIWA: NIMERIDHISHWA NA HATUA ZA AWALI ZA UWEKEZAJI MKINGA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametembelea eneo la mradi wa ujenzi wa viwanda 11 katika kijiji cha Mtimbwani wilayani Mkinga, ambapo amesema ameridhishwa na hatua za awali za uwekezaji huo.

Katika eneo hilo vinatarajiwa kujengwa viwanda mbalimbali kikiwemo cha saruji cha Hengya, kiwanda cha vioo, kiwanda cha vifaa vya kisasa vya ujenzi na uzalishaji wa umeme kwa kutumia makaa ya mawe.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumanne, Oktoba 30, 2018) wakati akizungumza na wananchi katika kijiji cha Mtimbwani wilayani Mkinga akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani Tanga.

Amesema uwekezaji huo unatarajiwa kulinufaisha Taifa na wananchi wakazi wa wilaya ya Mkinga kwa kuwa kinatarajiwa kuajiri zaidi ya watu 8,000, hivyo amewaomba wananchi hao waendelea kutoa ushirikiano kwa wawekezaji hao.

Kuhusu wananchi ambao eneo lao limechukuliwa na wawekezaji na bado hawajalipwa fidia, Waziri Mkuu amewataka wawe na subira kwa kuwa wote watalipwa. “Mwekezaji amenihakikishia kwamba atawalipa wananchi wote wanaodai fidia.”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka watumishi wa umma watenge siku tatu kila wiki na wawafuate wananchi waishio vijijini ili kusikiliza kero zao na kuzipatia ufumbuzi.

Amesema Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imedhamiria kuwatumikia wananchi bila ya ubaguzi wa kidini, kisiasa, rangi na kimapato, hivyo amewataka watumishi hao wafanye kazi kwa bidii.

Awali, Mbunge wa jimbo la Mkinga, Bw. Dunstan Kitandula ameishukuru Serikali kwa niaba ya wananchi wa Mkinga baada ya Serikali kufuta hati ya shamba la moa na kuirudisha ardhi hiyo kwa wananchi, pia ameomba ifute hati za mashamba mengine yaliyotelekezwa katika tarafa ya Maramba.

-ends-