WAZIRI MKUU AAGIZA KUKAMILISHWA KWA KANUNI ZA MASOKO YA MADINI

*Ataka maagizo ya Rais kuhusu masoko ya madini yatekelezwe haraka

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi wa Wizara ya Madini uhakikishe kanuni za uendeshaji wa masoko ya madini katika mikoa yote nchini zinakamilika na kuanza kutumika kwa wakati huku lengo likiwa ni kuongeza tija kwenye sekta hiyo.

Katika kukabiliana na changamoto ya utoroshwaji wa madini nchini, Rais Dkt. John Magufuli aliagiza kuanzishwa kwa masoko ya madini kwenye mikoa yote, hivyo Waziri Mkuu ameitaka Wizara ya Madini na wakuu wote wa mikoa watekeleze maagizo  hayo haraka.

Ameyasema hayo leo (Jumamosi, Januari 26, 2019) wakati akifungua mkutano kuhusu uanzishwaji wa masoko ya madini katika mikoa yote nchini. Mkutano huo umefanyika kwenye ukumbi wa Kambarage, Wizara ya Fedha na Mipango jijini Dodoma.

Mkutano huo wa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa umehudhuriwa na Mawaziri, Manaibu Waziri, Makatibu Wakuu na Manaibu Makatibu Wakuu pamoja na watendaji wa Wizara ya Madini pamoja na watendaji wa Tume ya Madini.

Waziri Mkuu amesema katika kuanzishwa kwa masoko hayo, rasimu ya kanuni imeandaliwa na hivyo ni vema wakazielewa vizuri kwa sababu wao ndiyo watakaozitekeleza kwenye maeneo yao ili Serikali iweze kufikia lengo ililojiwekea katika kuimarisha sekta ya madini.

”Kutokana na umuhimu wa masoko hayo naagiza kanuni hizo zikamilishwe haraka iwezekanavyo ili kuwasaidia watu wetu kupata masoko ya uhakika ya madini na Serikali itanufaika na mrabaha na tozo mbalimbali zitakazokuwa zikitozwa kwa mujibu wa sheria.”

Kadhalika, Waziri Mkuu ameagiza pindi kanuni hizo zitakapokamilika, Wizara ya Madini ihakikishe zinafikishwa kwa Wakurugenzi wa Majiji, Manispaa na Halmashauri za wilaya, maeneo ya machimbo, wachimbaji na wafanyabiashara wa madini ili kuondoa migogoro.

Hata hivyo, Waziri Mkuu ameongeza kuwa OR-TAMISEMI kupitia wakuu wa Mikoa na Maafisa Tawala wa Mikoa wakishirikiana na Wizara na Tume ya Madini waandae taratibu zitakazowezesha Wakurugenzi wa halmashauri kutoa maoni katika kuanzisha masoko.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka wakuu wa mikoa wakasimamie kikamilifu masuala ya ulinzi na usalama kwenye masoko hayo ili kuwahakikishia wafanyabiashara, wachimbaji na wananchi usalama wa kutosha wakati wa kuuza madini hayo.

Amesema kwa muda mrefu Rais Dkt. Magufuli amekuwa akisisitiza kuhusu sekta ya madini kuchangia ipasavyo katika pato la Taifa na hivyo kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijami kwa wananchi, lakini sekta hiyo imekuwa na matatizo ikiwemo utoroshwaji wa madini na migogoro kwa wachimbaji hususani wachimbaji wadogo.

”Jitihada mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa kuhakikisha changamoto hizo zinaondolewa kwa lengo la kuongeza tija kwenye sekta ya madini. Napenda mfahamu kuwa mna nafasi muhimu katika kuifanya sekta hii iweze kuleta manufaa yanayotarajiwa kwa Taifa.”

Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Doto Biteko amesema mkutano muhimu kwa sababu linalenga kumaliza changamoto ya masoko ya madini nchini, hivyo amewataka wakuu wa mikoa wahakikisha walipa kipaumbele jambo hilo kwa kuwa linamanufaa kwa Taifa.

Amesema kwa sasa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini hawana maeneo maalum wanayoweza kufanyia biashara ya madini  hali ambayo inachangia kuwepo kwa utoroshwaji wa madini, jambo ambalo linasababisha Serikali kukosa mapato.

Waziri Biteko ameongeza kuwa ili kukabiliana na changamoto ya masoko ya madini, Wizara iliunda kamati iliyojumuisha wajumbe kutoka katika taasisi mbalimbali za Serikali zikiwemo Ofisi ya Rais Ikulu, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wizara ya Madini, Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Viwanda na Biashara, Benki  Kuu na Tume ya Madini. 

Amesema kamati hiyo iliundwa ili kuandaa rasimu ya Kanuni za kuanzisha na kusimamia Masoko ya Madini Nchini. “Katika kuandaa kanuni hizo, jina la kanuni linapendekezwa liwe The Mining (Mineral and Gem House) Regulations, 2019," amesema Waziri Biteko.

-ends-