SERIKALI YATOA MWEZI KWA WIZARA, BODI YA MAZAO MCHANGANYIKO

*Februari 15 wawe wamekamilisha uhakiki na malipo kwa wakulima wa korosho

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Kilimo pamoja na Bodi ya Mazao Mchanganyiko wahakikishe hadi Februari 15 mwaka huu wawe wamekamilisha uhakiki na kuwalipa wakulima wote wa zao la korosho.

Pia amesema Serikali inaendelea kufuatilia mwenendo wa mazao makuu ya biashara kuanzia hatua ya uzalishaji hadi masoko yake likiwemo zao la korosho kwa lengo la kuwapatia tija wakulima.

Amesema zao la korosho ambalo awali soko lake halikwenda vizuri kutokana na utaratibu uliokuwa ukitumiwa na wafanyabiashara kwa kutenda bei ndogo na wakulima wenyewe kugomea bei hiyo.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumapili, Januari 27, 2019) wakati akizungumza na wadau wa zao la korosho mkoani Mtwara, lengo likiwa ni kupata taarifa juu ya mwenendo mzima wa bidhaa hiyo kwa msimu wa mwaka 2018/2019.

Amesema Serikali ilitoa nafasi kwa wafanyabishara kufanya    marekebisho ili waweze kununua bidhaa hiyo kwa bei nzuri bila mafanikia hali iliyopelekea Serikali kuamua kununua korosho zote ili wakulima wapate tija.

Naibu Waziri wa Kilimo Omary Mgumba amesema kuwa, taarifa iliyotolewa na timu ya uhakiki ilisema msimu wa 2018/2019 matarajia yalikuwa ni kuvuna tani 150,000 kutokana na kushuka kwa uzalishali.

“Lakini kwa kazi nzuri iliyofanywa na timu nzima ya Wizara, wilaya na mkoa na timu ya uhakiki hadi sasa korosho tulizozipokea ambazo ziko katika maghala ni zaidi ya tani laki mbili.”

Amesema zoezi hilo limewapa tija kubwa katika zao hilo tofauti na taarifa zilizowafikia hapo awali, ambapo wanatarajia baada ya zoezi hilo kumalizika watafikisha zaidi ya tani 200,000 ikiwa ni nyongeza zaidi ya tani 100,000.

Amesema, Wilaya inayoongoza kwa uzalishaji mkubwa hapa nchini ni Tandahimba amabpo wamefikia asilimia 96 ya uhakiki hadi kufikia jana huku zoezi la malipo kwa korosho zote zilizohakikiwa kwa mkoa wa Mtwara yamefikia asilimia 83.

Hata hivyo, Waziri huyo amesema kuwa fedha za kununulia korosho hizo zipo kwa kuwa Serikali imejipanga vizuri. Jumla ya sh bilioni 700 zimetengwa kwa ajili ya zoezi hilo ambapo hadi sasa zaidi ya sh. bilioni 400 zimeshalipwa wakulima waliohakikiwa hadi juzi.

-ends-