WAZIRI MKUU AFUNGA SOKO LA NDUTA WILAYANI KIBONDO

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amelifunga soko la pamoja baina ya wakimbizi na wananchi lililoanzishwa nje ya kambi ya Nduta iliyopo wilayani Kibondo mkoani Kigoma.

Amechukua hatua hiyo baada ya kubaini kuwa soko hilo limegeuka kuwa chanzo cha wakimbizi kutoka nje ya kambi kiholela na kushiriki matukio ya uhalifu.

Waziri Mkuu ametangaza uamuzi huo leo (Jumanne, Februari 19, 2019) wakati akizungumza na watumishi wa umma katika ya Halmashauri ya Kibondo. ”Vitendo vya uhalifu wilayani Kibondo vikiwemo vya utekaji wa watoto vimeongezeka na kusababisha hofu na taharuki miongoni mwa wananchi.”

Waziri Mkuu amesema ni vema halmashauri hiyo ikaandaa utaratibu wa kujenga soko ndani ya kambi na kutoa vibali vitakavyowaruhusu Watanzania wapeleke bidhaa ndani ya kambi hiyo.

Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka wananchi waliopewa dhamana ya kufanya kazi kwenye kambi za wakimbizi wawe waadilifu na wasimamie sheria. “Nafahamu tunao watendaji wetu ambao wapo kambini kusimamia shughuli mbalimbali za wakimbizi, tekelezeni wajibu wenu ipasavyo na si vinginevyo.”

Baada ya kuzungumza na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Kibondo, Waziri Mkuu alikwenda wilayani Kakonko na kukagua mradi wa maji Muhange.

Pia Waziri Mkuu ameweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa makao makuu ya Halmashauri ya wilaya ya Kakonko unaotarajiwa kugharimu sh. bilioni 4.5.

-ends-