WAZIRI MKUU AFUNGUA MICHUANO YA AFCON U-17

*Asema kuanzia kesho hakuna kiingilio kwa Watanzania

*Tanzania yaanza vibaya, yapigwa 5-4

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amefungua michuano ya fainali za mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 (AFCON U-17) na kutangaza kuwa kuanzia kesho Watanzania wataingia bure uwanjani kuangalia mashindano hayo.

Ametoa kauli hiyo leo jioni (Jumapili, Aprili 14, 2019) kwenye ufunguzi wa michuano hiyo iliyoanza leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. 

Waziri Mkuu ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa michuano hiyo, aliambatana na Rais wa Shirikisho la Soka na barani Afrika (CAF), Ahmad Ahmad kukagua timu zilizofungua dimba na kisha akatangaza uamuzi huo wa Serikali. 

“Ngugu wanamichezo niko mbele yenu kutangaza kuwa mashindano ya AFCON chini ya umri wa miaka 17 mwaka 2019 yanayochezwa hapa Tanzania yamefunguliwa rasmi. Kwa Watanzania, wapenda michezo, Serikali inatangaza kuwa kuanzia kesho, Watanzania wote wataingia uwanjani kuangalia michezo hii bure,” amesema na kuamsha shangwe kwa mashabiki.

Timu zilizofungua dimba leo ni Serengeti Boys ya Tanzania na Nigeria. Katika mchezo wa leo Nigeria imeibuka kidedea baada ya kuifunga Tanzania mabao 5-4. Hadi mapumziko timu ya Nigeria ilikuwa ikiongoza kwa mabao 3-1.

Mabao ya Nigeria yalipatikana dakika ya 20, 29, 36, 71 na 78 wakati mabao ya Tanzania yalipatikana dakika ya 21, 51, 56 na 60 ambapo magoli mawili kati ya hayo, yalipatikana kwa njia ya penati.

Bao la kwanza la Nigeria lilifungwa dakika ya 20 na Olatomi Olaniyan na dakika moja baadaye, Tanzania ilisawazisha kupitia kwa mchezaji wake Alphonce Msanga. Bao la pili kwa Nigeria lilifungwa dakika ya 29 na Idom Onyedikachi Ubani na la tatu lilifungwa na Akinkunmi Amoo katika dakika ya 36.

Tanzania ilianza kipindi cha pili kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la pili kwenye dakika ya 51 lililofungwa na Kelvin John.

Dakika tano baadaye, Morice Abraham aliipatia Tanzania bao la tatu lililofungwa kwa njia ya penati. Kabla vijana wa Nigeria hawajakaa sawa, dakika ya 60, Edmund John alitinga kimiani bao la nne, ambalo pia lililifungwa kwa penati.

Hata hivyo, vijana wa Nigeria walisawazisha bao la nne katika dakika ya 71 kwa mchomo uliopigwa na Wisdom Onyendikachi Ubani huku bao la tano likitinga wavuni katika dakika ya 78 kwa shuti ya mpira wa adhabu uliopigwa na Ibraheem Jabaar.

Timu ya Tanzania iko kundi A na imepangwa na Nigeria, Uganda na Angola. Michuano hii inatarajiwa kumalizika Aprili 28. Endapo timu hiyo ya Taifa ya vijana ya Serengeti Boys itaibuka na ushindi katika michezo yake miwili, itakuwa imekata tiketi ya kushiriki mashindano ya dunia kwa vijana wa umri wa miaka 17 yatakayofanyika mwakani huko Brazil.

Kikosi cha Tanzania kilikuwa na Mwinyi Yahya, Arafat Swakali, Mustafa Nankuku, Alphonce Msanga, Misungwi Chananja/Edson Mshirakandi (dk.34), Edmund John, Kelvin John, Pascal Msindo, Dominic William, Ally Rutibinga na Morice Abraham/Ladaki Chasambi (dk.71).

Nigeria iliwakilishwa na Suleman Shaibu, Shedrack Tanko, Ogaga David Oguko, Samson Tijani, Clement Ferdinand Ikenna, David Ishaya, Olakunle Olusegun, Mayowa Abayomi/Fawaz Abdullahi (dk.80), Wisdom Onyedikachi Ubani, Akinkunmi Amoo na Olatomi Olaniyan/ Ibraheem Jabaar (dk.71).

-ends-