TIMU ZA BUNGE, WAWAKILISHI ZATOKA SARE 2-2

TIMU ya Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoka sare kwa kufungana mabao 2-2 na timu ya Wajumbe wa Baraza Wawakilishi katika mchezo wa kirafiki uliofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.

Mtanange huo umechezwa leo (Ijumaa, Aprili 26, 2019) ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 55 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Hadi mapumziko timu hizo zilikuwa suluhu.

Timu ya Wabunge ndiyo ilikuwa ya kwanza kupata goli kwenye dakika ya pili ya kipindi cha pili   lililofungwa na Venance Mwamoto.

Iliwachukua dakika mbili tu, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kusawazisha bao hilo lililofungwa na Juma Ally baada ya kupiga shuti kali la umbali wa mita 20.

Hata hivyo, goli hilo lilizua utata na kusababisha mpira huo kusimamia kwa dakika tano ili wavu wa goli urekebishwe kwa sababu mpira ulipita kwenye wavu ambao umechanika, upande wa kushoto juu ya goli.

Ilimlazimu mwamuzi Byrceson Msuya wa Dodoma awasiliane na mshika kibendera wake na hatimaye wakaridhia kuwa hilo lilikuwa ni goli.

Mara baada ya mpira kuanza, kapteni wa timu ya Baraza la Wawakilishi, Hamza Hassan aliipatia timu yake bao la pili kwenye dakika ya nane baada ya kupiga kichwa kupitia mpira wa krosi uliopigwa na Masoud Abraham.

Mpira uliendelea kwa kasi huku kila timu ikijaribu kutafuta goli ambapo kwa upande wa Baraza la Wawakilishi, wachezaji Mohammed Mgaza na Juma Ali walikuwa mwiba kwa ngome ya Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha, kwa upande wa Jamhuri ya Muungano washambuliaji Venance Mwamoto na Yona Kirumbi ambaye aliingia kipindi cha pili, walikuwa mwiba kwa ngome ya Baraza la Wawakilishi lakini ustadi wa golikipa wa Baraza la Wawakilishi, Fakhi Suleiman ulikuwa kikwazo kikubwa kwao kwani aliokoa michomo mingi ya washambualiaji wa timu ya Bunge.

Ikiwa imebakia dakika moja mchezo huo kumalizika, mchezaji wa timu ya Bunge, Yona Kirumbi aliisawazishia timu yake bao la pili baada ya kupikea pasi ndefu kutoka kwa Onesmo Raurau.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mchezo huo kumalizika, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye alichezesha mechi hiyo kwa dakika tano, alisema mechi ilikuwa nzuri na imetumika kudumisha Muungano wa Tanzania Bara na Zanzibar.

Pia aliahidi kwamba, kwenye maadhimisho ya miaka 56 ya Muungano, timu ya Bunge itakwenda kucheza uwanja wa Aaman, Zanzibar pamoja na timu ya Baraza la Wawakilishi.

Naye Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema timu ya Bunge imecheza vizuri sana na ameshuhudia timu ya Baraza la Wawakilishi ikiwa imezidiwa, na kama wangeongeza dakika tano, ni lazima timu yake ingetoka na ushindi.

Kwa upande wake, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zuberi Ali Maulid aliwapongeza wachezaji wa timu zote mbili kwa umahiri waliounyesha na kuongeza kwamba watawasubiria mwakani timu ya Bunge Sports Club katika mtanange utakaofanyika huko Zanzibar.

Timu ya Bunge iliwakilishwa na Ally Salum, Abdallah Haji, Salum Rehani/ Pascal Haonga, Ally King/Chiza Amani, Yusuf Kaiza, Venance Mwamoto, William Ngeleja/Yona Kirumbi, Cosato Chumi, Sixtus Mapunda/Onesmo Raurau, Godfrey Mgimwa/Peter Msigwa na Alex Gashaza/Rajab Kipilo.

Timu ya Wawakilishi ilikuwa na Fakhi Suleima, Ali Salum, Ramadhani Hamisi, Amour Mohammed, Juma Ali, Miraji Khamis, Mohammed Mgaza, Masoud Abrahman, Rashid Ali Juma/Dau Maulid, Hamza Hassan na Suleiman Sarahan.

 

-ends-