WAZIRI MKUU AONGOZA MAZISHI YA ASKOFU MMOLE

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Watanzania wote wamuenzi marehemu Askofu Mstaafu Gabriel Mmole (80) wa Jimbo Katoliki Mtwara kwa wema, upole na utumishi mwema aliouonesha wakati wote wa maisha yake.

Ametoa wito huo leo (Jumanne, Mei 21, 2019) wakati wa mazishi ya Askofu Mmole yaliyofanyika katika Kanisa Katoliki Mtwara na kuhudhuriwa na viongozi, waumini wa Kanisa Katoliki pamoja na wakazi wa mkoa wa Mtwara

Askofu Mmole alizaliwa Januari Mosi, 1939 katika Parokia ya Nangoo, ambapo alibatizwa na kupata kipaimara Oktoba 5, 1952. Mwaka 1971 alipata daraja ya upadre na kuwa Askofu kuanzia mwaka 1988, alifariki Mei 15, 2019 Mkoani Mtwara baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Maeneo aliyoyatumikia tangu apate daraja la padri ni Paroko msaidizi wa Mnero (1972), Pastoral Institute GABA - Uganda (1973), Gombera wa Seminari ya Namupa (1974 hadi Mei 1988), alitangazwa kuwa Askofu wa Jimbo la Mtwara Machi 12, 1988 na alisimikwa kuwa Askofu wa Jimbo hilo, Mei 25, 1988.

Mwaka 1951 hadi 1954 alipata elimu katika shule ya msingi Ndanda; 1955 alisoma Nyangao Middle School, 1956 akahamia Lukuledi ambako alihitimu 1958. Alienda Chuo cha Ualimu Peramiho 1959 hadi 1960, ambapo 1962 alijiunga na seminari ndogo ya Namupa na alihitimu 1964.

Mwaka 1965 hadi 1966 alichukua masomo ya falsafa kwenye Seminari Kuu ya Peramiho na mwaka 1967 hadi 1971 alichukua masomo ya theolojia katika seminari hiyo hiyo ya Peramiho. Mwaka 1971 alifanya mitihani ya Baccalaureate inayotoka Chuo Kikuu cha Kipapa Urbaniana Roma na kupata shahada ya theolojia.

Ibada ya mazishi iliongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo la Songea, Mhashamu Askofu Damian Dallu ambaye alitumia fursa hiyo kuwaasa Watanzania waishi kwa kuheshimiana na wawe na maadili mema.

Waziri Mkuu amesema enzi za uhai wake, Askofu Mmole alitoa kipaumbele katika masuala muhimu ya maendeleo ya jamii ikiwemo elimu ambapo alisaidia sana watawa waliomaliza darasa la saba na kuwasaidia wajiunge na shule za sekondari.

“Hata uanzishwaji wa Chuo Kikuu cha STEMMUCO ambacho ni tawi la SAUT hapa Mtwara ni moja ya jitihada zake alizozifanya katika kuhakikisha anawapa elimu bora vijana na jamii. Kifo chake ni pigo kubwa kwa Taifa kwa sababu tumepoteza kiongozi wa kiroho aliyesimamia kwa uadilifu ustawi wa jamii ya Kitanzania.”

Kwa upande wake, Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania, Mhashamu Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga wa Jimbo Kuu la Mbeya amesema wamepata simanzi kubwa kufuatia kifo cha Askofu Mmole kwani walitegemea hekima zake katika Baraza la Maaskofu.

“Askofu Mmole alikuwa kielelezo cha dhamira njema na alilitumikia kanisa katika hali yoyote, hivyo yatupasa kumuombea apumzike kwa amani,” aliongeza.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Bw. Gelasius Byakanwa aliwashukuru viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini mkoani Mtwara kutokana kwa ushirikiano mzuri anaopata unaomwezesha kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Mazishi hayo yamehudhuriwa na maelfu ya wananchi, maaskofu wa majimbo mbalimbali nchini, Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Mheshimiwa Benjamin Mkapa na mkewe Mama Anna Mkapa, Waziri wa Nchi (OR-Utumishi na Utawala Bora), Mhe. Huruma George Mkuchika.

-ends-