TUSIKWEPE JUKUMU LA KUWATUNZA WAZEE-MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka vijana na jamii kwa ujumla wasikwepe jukumu la kuwatunza wazee kwa sababu nguvu zao za uzalishaji mali zimepungua kutokana na kazi waliyoifanya wakiwa vijana kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa familia zao na Taifa kwa ujumla.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kutekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Kutokomeza Mauaji ya Wazee uliozinduliwa Januari, 2019 ili kwa kutokomeza ukatili kwa wazee ifikapo 2023 na kuhakikisha wazee na watu wenye ulemavu wanatambuliwa na kulindwa dhidi ya ubaguzi, uonevu, ukatili na mila potofu.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumapili, Septemba 29, 2019) wakati akizindua kambi ya utoaji wa huduma za afya kwa wazee na watu wenye ulemavu katika viwanja vya Kichangani mjini Iringa akiwa katika siku ya sita na ya mwisho ya ziara yake ya kikazi mkoani Iringa.

Amesema wajibu wa kuwahudumia au kuwasaidia wazee na watu wenye ulemavu ni wa kila mmoja na wanapaswa watambue kwamba wazee hao wamelitumikia Taifa kwa muda mrefu tena kwa namna mbalimbali ikiwemo kuwaletea na kuhakikisha wanapata mafanikio hayo ambayo wanajivunia sasa.

“Kwa msingi huo, tunao wajibu wa kuwajali wazee wetu kwa hali na mali ikiwa ni sehemu ya matunda ya uwajibikaji wao kwetu na kwa Taifa kwa ujumla. Hivyo basi, tutumie vema Kambi hii kuwasaidia wazee wetu na watu wenye ulemavu kwa kutambua afya zao na kuwapatia matibabu ya kiafaya ili waendelee kuwa salama na wenye furaha nasi tuvune busara zao.”

Kutokana na umuhimu wa kuwatunza wazee na kuwasaidia watu wenye ulemavu, Waziri Mkuu ametoa rai kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa, wananchi na wadau mbalimbali kuendelea kuimarisha upatikanaji wa fursa, haki na ustawi wa wazee ikiwemo kuondokana kabisa na vitendo vya ukatili dhidi yao.

“Vituo vyote vya kutoa huduma za afya vya umma kutoa huduma bora na za haraka kwa wazee wetu wenye vitambulisho. Tengeni dirisha maalumu kwa ajili ya kuwahudumia ili wasikae kwenye foleni muda mrefu. Serikali itaendelea kuweka miundombinu na mazingira rafiki ili kuwawezesha kupata mahitaji yao.”

Amesema Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kuimarisha ustawi na maendeleo ya wazee, hatua hizo ni pamoja na kuanzishwa kwa mpango wa TASAF wa kunusuru kaya masikini. Mpango huo umelenga kuyasaidia makundi mbalimbali ya jamii yanayoishi katika umasikini uliokithiri ikiwemo kundi la wazee.

Amesema hadi kufikia Septemba 2019, jumla ya wazee 680,056 kutoka kaya 1,118,747 wananufaika na Mpango wa TASAF kwa Tanzania Bara na Zanzibar. Mpango huu, umesaidia wazee kujikimu kimaisha na kumudu majukumu ya kulea wajukuu ambao wazazi wao wamepoteza maisha kwa sababu mbalimbali ikiwemo ugonjwa wa UKIMWI.

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kusimamia maelekezo yake kwa Halmashauri zote nchini kuwatambua wazee wasiojiweza na kuwapatia vitambulisho vya matibabu bila malipo. “Namshukuru Mbunge wa Viti Maalum, Ritha Kabati amebainisha mafanikio yanayoendelea kupatikana kutokana na utekelezaji wa agizo hilo.

“Haidhuru nasi tukiiga mfano wa Mheshimiwa Ritha Kabati, Mbunge wa Viti Maalumu na kaka yangu Mheshimiwa Pinda, Waziri Mkuu Mstaafu kwa moyo wao wa kizalendo kabisa kuona kuna haja ya kusaidia na kuunga mkono juhudi za Rais wetu mpendwa Dkt. John Magufuli za kuwahudumia wanyonge.”

Hata hivyo, Waziri Mkuu ameendelea kuziagiza Halmashauri zote nchini kuhakikisha zoezi hilo linakuwa endelevu kwa kuwatambua na kuwapatia vitambulisho wazee wote nchini wasio na uwezo ili waweze kunufaika na huduma ya matibabu bila malipo pamoja na huduma zingine za kijamii.

Vilevile, Waziri Mkuu amesema kwa kuwa Novemba 2019 nchi inatarajia kufanya uchaguzi wa Serikali za Mitaa, wazee kama sehemu ya jamii wana haki ya kushiriki katika uchaguzi huo kwa kuchagua viongozi wanaoona watafaa kuwaongoza na wao kuchaguliwa kuongoza katika nafasi mbalimbali. Hivyo wasaidiwe kushiriki zoezi hilo.

-ends-