IMARISHENI HALI YA USALAMA, MAJALIWA AAGIZA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi wa mkoa wa Mjini Magharibi kuhakikisha hali ya usalama inaimarishwa ili kuboresha shughuli za utalii na kulinda usalama wa raia na mali zao.

Pia, Waziri Mkuu amemwagiza Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ahakikishe Jeshi la Polisi linadhibiti mianya yote ya uingizwaji, usafirishwaji, uzalishaji na utumiaji wa dawa za kulevya pamoja na vitendo vya ukatili wa jinsia dhidi ya wanawake na watoto.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumamosi, Januari 18, 2020) wakati akizungumza na viongozi na watumishi wa Mkoa wa Mjini Magharibi kwenye ukumbi wa mikutano wa hotel Verde. Amewasisitiza watumishi kutimiza majukumu yao ipasavyo.

“Huu ni mji wa kitalii, hivyo ni lazima polisi wakaimarisha hali ya usalama, vitendo vya wizi na uporaji lazima vidhibitiwe. Pia halmashauri ya Jiji nayo ihakikishe hali ya usafi inaimarishwa hususani katika barabara. Mji huu lazima uvutie.”

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema hali ya ufaulu kwa upande wa elimu ya msingi si nzuri. Hivyo, ameuagiza uongozi wa wizara ya elimu uhakikishe unafanya mabadiliko katika kuisimamia sekta hiyo. “Maafisa elimu waache kukaa maofisini waende mashuleni kusimamia ufundishaji.”

Amesema Serikali inataka kuona watoto wakifanya vizuri kuanzia ngazi ya elimu ya msingi hadi elimu ya juu. “Ili malengo hayo yatimie ni lazima watendaji katika sekta ya elimu wakabadilika na kusimamia vizuri ufundishwaji. “Tunataka watoto wanapoanza masomo yao ya msingi wafike hadi ngazi ya chuo kikuu ili tuwe na wataalamu wengi.”

Akizungumzia kuhusu sekta ya afya, Waziri Mkuu amewataka watumishi waimarishe utoaji wa huduma hizo kwa wananchi kwa sababu Serikali imefanya mabadiliko kwenye sekta hiyo ikiwa ni pamoja na kuongeza bajeti ya dawa.

Pia, Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa mkoa wa Mjini Magharibi ufanye tathmini ya utendaji wake na kubaini mafanikio yanayopatikana katika ukusanyaji wa mapato pamoja na changamoto zitakazojitokeza ili waweze kupatia ufumbuzi kwa wakati.

Amesema ni vema wakasimamia makadirio ya ukusanyaji wa mapato na wahakikishe wanabaini vyanzo vyote na wafuatilie iwapo makadirio hayo ni sahihi na fedha zote zinazokusanywa kama zinaingia katika mfuko mkuu wa Serikali. Makusanyo yafanyike kielektroniki.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Bw. Hassan Khatibu amemuhakikishia Waziri Mkuu kwamba maelekezo yote aliyotoa kwao ameyapokea na kwamba watayafanyia kazi ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuimarisha ukusanyaji wa mapato.

 -ends-