WAZIRI MKUU AONGOZA HARAMBEE YA PAPO KWA PAPO

*Achangisha mifuko 2,000 ya saruji ujenzi wa uzio wa sekondari

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amechangisha mifuko 2,000 ya saruji na sh. milioni 50 kwenye harambee ya papo kwa papo kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa sekondari ya Mwendakulima wilayani Kahama.

Waziri Mkuu ameendesha zoezi hilo leo (Jumapili, Julai 15, 2018) wakati akizungumza na walimu na wanafunzi wa sekondari ya Mwendakulima, wilayani Kahama mkoani Shinyanga ambako alienda kupokea mabweni mawili ya wasichana.

Ujenzi wa mabweni hayo yenye uwezo wa kulaza wanafunzi 126, umegharimu sh. milioni 560 na umefadhiliwa na kampuni kuchimba madini ya ACACIA kupitia fedha za Corporate Social Responsibility. Mabweni ya awali yaliteketea kwa moto.

Waziri Mkuu ameendesha harambee hiyo baada ya kuombwa na Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mwendakulima, Bi. Neema Mfunya. Kwa wastani, mfuko mmoja wa saruji unagharimu sh. 16,500.

Katika harambee hiyo, Waziri Mkuu alichangaia mifuko 500 ya saruji, huku kampuni ya ACACIA ikichangia mifuko 400 kutoka kwa watumishi wake. MNEC wa Simiyu, Bw. Emmanuel Nsangali aliahidi kuchangia mifuko 200.

Ahadi nyingine zilizotolewa na Naibu Mawaziri, wabunge, na wakuu wa taasisi waliombatana na Waziri Mkuu kwenye ziara yake zilikuwa ni za mifuko 50 hadi 100.

Shule ya sekondari ya Mwendakulima ina wanafunzi 336 wa kidato cha tano na cha sita. Lakini kwenye kidato cha kwanza hadi cha nne, shule hiyo ina wanafunzi 771 ambao kati yao, wavulana ni 423 na wasichana ni 348.

-ends-