CAF YARIDHISHWA NA MAANDILIZI YA AFCON

RAIS wa Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF), Bw. Ahmad Ahmad amesema ameridhishwa na maandalizi ya michuano ya Afrika ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (AFCON).

Mashindano ya mpira wa miguu kwa Vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 AFCON yanayotarajiwa kufanyika mwaka 2019 nchini Tanzania.

Ameyasema hayo leo (Jumatatu, Agosti 27, 2018) wakati akizungumza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika makazi ya Waziri Mkuu, Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Pia ameihakikishia Serikali kwamba hakuna mabadiliyo yoyote ya ratiba yatakayofanyika kuhusu wenyeji wa mashindano na kwamba CAF itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kufanikisha michuano hiyo.

Rais wa CAF yupo nchini kwa ajili ya kuongoza mkutano maalum wa mabadiliko ya katiba ya Baraza la Vyama vya Soka katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA). Mkutano huo unaofanyika jijini Dar es Salaam, umehudhuriwa na viongozi wa juu wa nchi wanachama wote 12 wa CECAFA wakiwemo marais.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu amesema mechi zote za michuano ya Afrika ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (AFCON) zitafanyika jijini Dar es Salaam.

“Tupo kwenye hatua za mwisho za maandalijzi ya michuano hiyo itakayofanyika jijini Dar es Salaam katika viwanja vya Taifa, Uhuru, Chamanzi na JK Park utatumika kwa mazoezi.”

Waziri Mkuu amesema ni muhimu kwa Tanzania kushiriki katika mashindano makubwa kama hayo kwa kuwa yanasaidia ukuzaji wa vipaji kwa vijana ambao wengi wao ni wanafunzi.

-ends-