Logo
JENISTA MHAGAMA: AWATAKA WATANZANIA KUJENGA TABIA YA KUPIMA AFYA
Thursday, 01 December 2016 09:18    PDF 

Waziri wa Nchi Ofisi ya waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Watu Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (Mb) amewataka watanzania kujenga tabia ya kupima afya zao na pale wanapogundulika kuwa na maambukizo ya VVU wawe tayari kuanza dawa mara moja.

Amesema hayo wakati akizungumza na vyombo vya habari katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani tarehe 1 Desemba, 2016 Jijini Dar es Salaam.

“Siku ya UKIMWI duniani ni muhimu sana kwani nchi zote duniani zinawakumbuka wahanga wa janga hili na pia kufanya tafakuri ya kina ya namna bora ya kuongeza kasi katika kupambana na UKIMWI ikizingatia kauli mbiu ya mwaka huu inasema “Hands Up for HIV Prevention “– Tuungane Wote kuzuia Maambukizi Mapya ya VVU.

Tafiti za viashiria vya UKIMWI(VVU)/UKIMWI na Malaria (THMIS, 2011/12) inaonesha kuwa maambukizo ya VVU kwa upande wa Tanzania bara ni 5.3%, ambapo wanawake waathirika zaidi na janga hili ni 6.2% kulinganisha na wanaume ambao ni 3.8%, alisema Mhagama.

“Kutokana na changamoto na maambukizo hayo, inakadiriwa kuwa kuna watu 1,538,382 wanaoishi na VVU Tanzania, ambapo vijana wenye umri kati ya miaka 15 – 24 ni 10.6% na watoto walio chini ya miaka 15 ni 11.8% ya watu wanaoishi na VVU nchini. Kati ya idadi hiyo asilimia 50 ndio wanaopata dawa za kupunguza makali ya VVU, hivyo Takwimu za mwaka 2015 zinaonesha kuwa maambukizo mapya yana kadiriwa kufikia watu 48,000 kwa mwaka”, alisisitiza Mhagama.

“UKIMWI ukiwa bado ni janga kubwa Duniani na nchini Tanzania, dunia imejiwekea malengo ya kutokomeza UKIMWI kama janga ifikapo mwaka 2030. Hivyo Ili kufikia malengo hayo, Shirika la Umoja wa Mataifa linaloratibu mapambano dhidi ya UKIMWI (UNAIDS), limeweka malengo ya muda wa kati ya (90-90-90), na sisi Tanzania tunaenda sambamba na malengo hayo”, alisema.

“Asilimia tisini ya kwanza ya watu wote wanaokisiwa kuwa na VVU kujua hali zao. 90 ya pili ikimaanishwa kuwa asilimia tisini ya waliobainika kuwa na VVU kuanza kutumia dawa mara moja. Na 90 ya tatu ikimaanisha kuwa asilimia tisini ya walioanza dawa waweze kuwa na ufubazo endelevu wa virusi vya UKIMWI mwilini mwao”.

“Natoa rai kwa wananchi kuendelea kujitokeza kupima afya zao ili wajitambue na kujua namna ya kujiandaa, Serikali inatambua na kusisitiza kwa wale ambao watakutwa na maambukizo ya VVU, waanzishiwe huduma ya dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI mara moja ili waweze kuishi maisha marefu ya yaliyo na afya bora”, amesititiza Mhagama.

Ikiwa ni sehemu ya kupambana na Maambukizo ya VVU, Shirika la Afya Dunia inazitaka nchi zote kuwaanzishia dawa mara moja watu wote watakaopima na kugunduliwa wana VVU, yaani “test and Treat”. Katika kutekeleza agizo hili Wizara ya afya imeshatoa waraka wa kuanza mpango huu tangu Oktoba 2016 ambapo mpango huu unatarajiwa kuongeza sana mahitaji ya huduma za matibabu na dawa.

“Serikali itahakikisha kwamba watu wote watakaojitokeza kupata huduma za tiba wanapata dawa na huduma nyingine zinazoambatana na tiba kwa kutumia rasilimali za ndani”, alisema. “

Pamoja na maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani, tunazindua Mfumo wa Udhamini wa UKIMWI pamoja na Bodi yake ambayo malengo yake makuu ni kuhakikisha uwepo wa rasilimali za kutosha na za uhakika katika kupambana na UKIMWI, zinazotokana na mapato ya ndani na kupunguza utegemezi kwa wafadhili. Serikali tayari imetenga Bilioni 1 kwa ajli ya mfumo huo ambao ulishapitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungan1 wa Tanzania kupitia Sheria Na. 6 ya mwaka 2015 alisema.

“Mfumo huu utasaidia katika kukusanya fedha za kuratibu shughuli za UKIMWI nchini ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa dawa za ARV, HIV test kit pamoja na vifaa vya Maabara. Hii ni fursa ya kipekee kwa wadau tofauti, Mashirika, sekta binafsi na wafanyabiashara kuchangia katika mfuko huo ikiwa ni mwanzo wa kukusanya fedha kwa matumizi ya mwitiko wa UKIMWI kwa vyanzo vya mapato ya ndani ya nchini”, alisisitiza Mhagama.

Mapema: Mwenyekiti Mtendaji wa Tume ya UKIMWI Dr. Leonard L. Maboko alieleza kwamba maambukizo mapya ni milioni 2.1 duniani kwa mwaka 2015, kwa nchi za Kusini Jangwa la Saraha na Afrika Mashariki maambukizo ni 960,000 ambayo ni sawa na asilimia 46% ya maambukizo mapya na Tanzania ikiwa miongoni mwa makadirio hayo. “Kwa mantiki hiyo tatizo sio kubwa sana lakini hatutakiwi kukaa kimya hatunabudi kupamba na kuongeza kasi ili tuweze kuondoa kabisa maambukizo mapya” alisema Dr. Maboko.

-mwisho-

 

 
Our website is...
 
mod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_counter
mod_vvisit_counterToday70
mod_vvisit_counterYesterday121
mod_vvisit_counterThis week70
mod_vvisit_counterLast week867
mod_vvisit_counterThis month2188
mod_vvisit_counterLast month3157
mod_vvisit_counterAll days516980
Copyrights ©2013, The United Republic of Tanzania, Prime Minister's office All Rights Reserved