Logo
Mavunde: Awataka Vijana kuwa Wabunifu
Wednesday, 14 December 2016 00:00    PDF 


Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira), Anthony Mavunde amesema Serikali itaendelea kuwatunza, kuwatangaza na kuwaendeleza vijana wabunifu nchini ili kuwahamasisha kufanya shughuli za ubunifu nchini.

Aliyasema hayo tarehe 14 Desemba, 2016 akiwa Ofisi ya Waziri Mkuu Jijini Dar es Salaam wakati akipokea tuzo ya Mkurugenzi wa kampuni ya Malkia Investment Ltd, Bi. Jennifer Shigole aliyoshinda katika tuzo za African Entrepreneurship Awards nchini Morocco. Katika shindano hilo, Jennifer aliiibuka mshindi wa kwanza katika kipengele cha masuala ya elimu na mazingira na kujishinda mtaji wa dola laki moja na nusu.

“Mtakumbuka Mhe. Rais katika hotuba yake ya ufunguzi wa Bunge alituagiza kuwatambua vijana wabunifu na tayari tumewatambua na kuwaendeleza na natoa rai kwa vijana kujitokeza ili waweze kushirikiana na Serikali” Alisema Mavunde.

Aidha alisema Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo  ya Vijana wataikopesha kampuni ya Jenifa ya Malkia Investment Ltd kiasi cha Tsh Milioni 30 ili zisaidie kupanua mradi wake kwa lengo la kuongeza uzalishaji ili bidhaa zake ziwafikie vijana wengi zaidi waishio vijijini.

Mavunde alisema kuwa Serikali imeipatia kampuni hiyo ekari moja ya kiwanja kilichopo Wilayani Kibaha Mkoani Pwani ili kujenga kiwanda cha kutengeneza pedi za kike ambazo ni mkombozi kwa vijana wa kike hasa walio mashuleni.

Anaongeza kuwa Serikali pia itamtambulisha kwa vijana waelimishaji wa kitaifa wa stadi za maisha walioandaliwa na Serikali  kwa ajili ya kufundisha stadi za maisha katika mikoa ya Kagera,Mwanza, Geita, Simiyu, Dar es salaam, Pwani, Lindi, Mtwara, Morogoro, Dodoma, Singida, Tabora na  Manyara.

Wakati huo huo, Mavunde alisema kwa hatua hii Shigole ameleta ukombozi kwa watoto wa kike ambao wakati mwingine walikuwa wanashindwa kuhudhuria masomo kwa wakati, hivyo kwa kupata namna bora ya kutumia bidhaa yake aina ya Elea Reusable Sanitary Pads zitawasaidia vijana wa kike kutunza afya zao.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Jeniffer Shigole aliishukuru Serikali kwa kutambua mchango wake na vijana wenzake kwa kuona mchango wao katika jamii na kutoa wito kwa vijana wengi kuwa wabunifu wa miradi mbalimbali.

“Masuala ya hedhi yamekuwa changamoto kubwa sana kwa vijana wa kike hususani wale wa vijijini kuna wakati mwingine wanashindwa hata kuhudhuria masomo kwa wakati, hivyo kwa kupitia Elea Reusable Sanitary Pads watakuwa huru na salama mwaka mzima”alisisitiza Shigole.

Alisema kiwanda kitachotarajiwa kuanzishwa na kampuni hiyo kitaisaidia kutengeneza ajira na kupunguza uharibifu wa mazingira kwani pedi wanazotengeneza zimetengenezwa kwa pamba tofauti na zingine ambazo zimetengenezwa kwa plastic.

Aidha Shigole ametoa wito kwa vijana wengi zaidi kushiriki kupitia fursa za African Entrepreneurship Awards kuondoa woga na kuandaa maandiko yenye manufaa na uhalisia na mazingira tunayoishi ili waweze kujikwamua kiuchumi kwa kubuni miradi ambayo itawasaidia kimaendeleo na kujiajiri.

-Mwisho-

 
Our website is...
 
mod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_counter
mod_vvisit_counterToday104
mod_vvisit_counterYesterday117
mod_vvisit_counterThis week283
mod_vvisit_counterLast week825
mod_vvisit_counterThis month2168
mod_vvisit_counterLast month3455
mod_vvisit_counterAll days513803
Copyrights ©2013, The United Republic of Tanzania, Prime Minister's office All Rights Reserved