Logo
TIMU YA KUCHUNGUZA CHANZO CHA MOTO SOKO KUU LA KAYANGA YAUNDWA
Saturday, 07 January 2017 11:09    PDF 


Kufuatia kuungua kwa mara ya pili kwa soko kuu la kayanga katika Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe, Ofisi ya Mkuu wa mkoa Kagera imeiagiza Halmashauri hiyo kuunda timu mara moja na kuanza uchunguzi wa chanzo cha moto huo katika soko hilo, ambalo kwa mara ya kwanza liliungua tarehe 11 Machi, 2016.

Sehemu ya soko kuu la Kayanga imeungua usiku wa kuamkia tarehe 7 Januari, 2016, saa 9:00 usiku, ambapo vibanda 52 vilivyojengwa kwa mbao na meza 24 za wafanyabashara wadogowadogo wa nafaka, matunda na mbogamboga vimeteketea kwa moto pamoja na mali za wamachinga waliokuwa wanapanga chini wapatao 33 nao mali zao zimeteketea kwa moto.

Akiongea mara baada  ya kukagua athari za janga la moto katika soko hilo Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Kamishna Diwani Athumani, leo tarehe 7 Januari, 2017, amebainisha kuwa tayari Halmashauri ya wilaya hiyo imeshatekeleza maelekezo yao ya kuunda timu ya uchunguzi ambayo inaanza kutekeleza majukumu yake kesho, tarehe 8 Januari, kwa muda wa siku nne.

“Tumeunda timu tujue kwa nini hili soko linakuwa na majanga ya moto ya mara kwa mara, nawaomba wananchi wote wa Kayanga toweni ushirikiano wa kutosha kwa timu hii na yeyote mwenye taarifa ya chanzo cha moto  awasilishe taarifa zake kwenye kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hii”  Alisisitiza Athumani.

Aidha, Athumani alifafanua kuwa yeyeyote atakaye bainika kuwa ndo chanzo cha kusababisha majanga ya moto kutokea mara kwa mara katika soko  hilo hatua stahiki zitachukuliwa kwa kuwa  kuungua kwa soko hilo kumesababisha hasara kubwa kwa wafanyabiashara wa soko hilo.

Akiongea wakati wa ziara hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Adeodata  Agustine, amefafanua kuwa thamani ya awali ya mali iliyoteketea inakisiwa kuwa Tsh, 80,000,000/= (mazao ya nafaka, mbogamboga , matunda pamoja na nguo na bidhaa za dukani), na thamani ya vibanda ni Tsh, 52,000,000/= na meza ni 9,600, 000/=.

“Chanzo cha moto hadi sasa hakijajulikana na kikosi cha zimamoto kwa kushirikiana na Polisi na TANESCO wanaendelea na uchunguzi, taarifa hii ni ya awali tutapata taarifa kamili ya thamani ya mali na chanzo cha  janga la moto baada ya timu kukamilisha kazi kwa muda uliopangwa” alisema Adeodata.

Naye mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Soko kuu la Kayanga, Wilton William, aliishukuru halmashauri hiyo kwa juhudi walizo zifanya za kuzima moto huo pamoja na hatua walizozichukua za kuchunguza chanzo cha moto huo ambao umeunguza soko hilo kwa mara ya pili mfululizo.

Soko la Kayanga lina jumla ya vibanda 257, ambapo vibanda 122 vimejengwa kwa matofali, na vibanda 135 vimejengwa kwa mbao.  Katika tukio la janga la moto la mwaka jana vibanda 117 ikiwa ni vibanda 83 vya mbao na 34 vya tofali viliteketea kwa moto.

Mwisho.

 
Our website is...
 
mod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_counter
mod_vvisit_counterToday70
mod_vvisit_counterYesterday121
mod_vvisit_counterThis week70
mod_vvisit_counterLast week867
mod_vvisit_counterThis month2188
mod_vvisit_counterLast month3157
mod_vvisit_counterAll days516980
Copyrights ©2013, The United Republic of Tanzania, Prime Minister's office All Rights Reserved