Logo
Waziri Mhagama Ashauri MAKAMU SACCOS Ofisi ya Waziri Mkuu kuwa Wabunifu
Thursday, 19 January 2017 00:00    PDF 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama ameshauri uongozi wa Chama cha Akiba na Mikopo cha Ofisi ya Waziri Mkuu (Makamu Saccos) kuwa na ubunifu katika utendaji ili kuleta manufaa zaidi kwa wanachama wake.

Mhe. Mhagama ameyasema hayo wakati wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Wanachama wa Chama hicho uliofanyika Januari 19, 2017 katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Dodoma.

Katika Mkutano huo Mhe. Waziri alisisitiza kuwepo na mikakati madhubuti ya kubuni miradi itakayowezesha chama kuwa na vyanzo vyake vya mapato na kuwa na mikakati ya kuongeza wanachama wapya kwa kuzingatia umuhimu wa chama hicho.

“Ni muhimu kuwa na mikakati madhubuti ya kubuni miradi, kuongeza wanachama pamoja na kuwa na vitu vya kiupekee na vya kiufanisi vitakavyokisaidia chama kuwa imara katika utendaji wake”, alisema Waziri Mhagama.

Aliongeza kuwa chama hicho kimekuwa msaada mkubwa kwa wanachama wake amabapo wengi wao wamekuwa na maendeleo mbalimbali kutokana na uwepo wa fursa za mikopo isiyokuwa na masharti magumu.

“Chama kimekuwa mkombozi mkubwa kwa wanachama wake kwani wamekuwa wakikopa na kusaidia katika shughuli za kimaendele, ikumbukwe kuwa asilimia kubwa ya wafanyakazi wana maendeleo kwakuwa wanachukua mikopo mbalimbali inayowasaidia kuwepo na maendeleo ya kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja”, alisisitiza Mhe.Mhagama.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama hicho Bw. Joseph Muhamba aliahidi kuyachukua mapendekezo yote yaliyotolewa na Mhe.Waziri na kuyaweka katika vitendo ili kuhakikisha chama kinaongeza mbinu za ubunifu ikiwemo eneo la kuongeza wanachama wapya na kuweka mazingira mazuri zaidi kwa wanachama waliopo.

Mhe. Mhagama aliahidi kutoa ushirikiano wake kwa Chama hicho na kueleza kuwa chama kiitumie fursa ya Serikali kuhamia Dodoma kama chachu ya kuongeza wanachama wapya.

“Ninawaahidi kuwapa ushirikiano wa hali na mali na kuamini kuwa chama hiki ni msaada mkubwa kwa wafanyakazi wa Ofisi ya Waziri Mkuu kwani kipo kisheria kabisa na zipo kanuni zinazoelekeza juu ya uwepo wa chama na kwa kuonesha mfano mimi na Naibu Waziri Mhe. Dkt. Possi tunajiunga rasmi hii leo ili kuwa mstari wa mbele kukisaidia chama hiki”. Alisema Mhe. Mhagama.

-Mwisho-

 
Our website is...
 
mod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_counter
mod_vvisit_counterToday104
mod_vvisit_counterYesterday117
mod_vvisit_counterThis week283
mod_vvisit_counterLast week825
mod_vvisit_counterThis month2168
mod_vvisit_counterLast month3455
mod_vvisit_counterAll days513803
Copyrights ©2013, The United Republic of Tanzania, Prime Minister's office All Rights Reserved