Logo
Tuesday, 21 February 2017 23:12    PDF 

Waziri Mkuu: Wakurugenzi simamieni vizuri matumizi ya fedha za umma

*Afagilia ujenzi wa madarasa ya shule msingi Mogitu ya Katesh

*Kamati ya shule yatumia sh. 183m kujenga madarasa 8 na vyoo 14

*Ataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini waige mfano huo

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini wasimamie vizuri matumizi ya fedha za umma hasa kwenye majengo.

Ametoa agizo hilo leo jioni (Jumanne, Februari 21, 2017) wakati akizungumza na wazazi na baadhi ya watendaji wa wilaya ya Hanang baada ya kuzindua madarasa mapya manane na matundu ya vyoo 14 kwenye shule ya msingi Mogitu iliyopo Katesh wilayani humo, mkoani Manyara.

Waziri Mkuu alipangiwa kuzindua mradi wa ujenzi wa vyumba vinane vya madarasa, ukarabati wa vyumba vitatu na ofisi moja na ujenzi wa vyoo vya wanafunzi matundu 14 lakini hakuamini hadhi ya madarasa aliyoikuta kwenye shule hiyo kutokana na ubora wake.

“Nilipoingia hapa shuleni nilijua ni shule ya sekondari, kumbe ya msingi. Nimeambiwa ujenzi wa madarasa haya mapya, ukarabati wa madarasa matatu, ofisi moja na ujenzi wa vyoo matundu 14, vimegharimu sh. milioni 183 lakini ingekuwa kwa tenda za kawaida, hii fedha ingetosha kujenga madarasa matatu tu na ikaisha.”

“Mkurugenzi na timu yako ya Halmashauri, ukweli kwamba kiasi hiki cha fedha kimeweza kujenga madarasa nane, na vyoo vyote hivyo pamoja na kukarabati madarasa mengine matatu, ni lazima Hanang iwe mfano kwa Halmashauri nyingine nchi nzima,” amesisitiza.

Amempongeza Mhandisi wa wilaya hiyo, Eng. Steven Luwagwa kwa kusimamia kazi hiyo akisaidiana na Mwenyekti wa kamati ya shule, Mzee Giloya Memoya Semhonda usiku na mchana hadi mradi ukakamilika.

“Mhandisi Steven ni mfano wa kuigwa. Wako watumishi wengine kazi yao ni kugawana asilimia 10 ya fedha za Halmashauri wakishirikiana na Diwani na Mwenyekiti. Lakini hapa nimekuta kitu cha tofauti na nimevutiwa sana na kazi iliyofanyika. Hongera sana,” alisema.

Mapema, akisoma taarifa ya ujenzi wa shule hiyo, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Bi. Ruth Shuma alimweleza Waziri Mkuu kwamba walipokea sh. milioni 185.4 Septemba 2016 kutoka Serikali kuu na kazi ya ujenzi ilianza Novemba, mwaka jana na kukamilika Februari, mwaka huu.

“Fedha hizo zilitolewa chini ya Mpango wa Lipa Kulingana na Matokeo (Performance for Results –P4R) na Halmashauri ya Wilaya iliamua kutumia njia ya manunuzi ya ‘Force Account’ badala ya kutumia wakandarasi ili kupunguza gharama na kutaka kukamilisha mradi ndani ya muda mfupi,” alisema.

Mwalimu Shuma alisema faida ya kufanya manunuzi kwa kutumia ‘Force Account’ ni kuwezesha mradi huo kukamilika ndani ya muda mfupi na kuokoa fedha ambazo wamezitumia kukarabati madarasa mawili zaidi na ofisi moja ya walimu.

“Hadi mradi kukamilika, tumetumia sh. 183,441,532.00 na tutatoa kiasi cha sh. 1,958,468.00 ili kutengeneza madawati 35 ambayo yataondoa upungufu wa madawati 29 tulionao hapa shuleni,” alisema mwalimu Mkuu huyo.

Alisema shule hiyo ambayo ilianzishwa mwaka 1977, sasa hivi ina madarasa 17 na jumla ya wanafunzi 963 wakiwemo wavulana 459 na wasichana 504.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu alimkabidhi Mwenyekti wa kamati ya shule hiyo, Mzee Giloya Memoya Semhonda sh. 500,000 na cheti cha kuthamini kazi ya usimamizi wa fedha za umma na uadilifu katika kazi hiyo.

Fedha taslimu na cheti hicho vilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dk. Joel Bendera kwa niaba ya uongozi wa mkoa kutokana na kazi ambayo mzee huyo mwenye miaka 53 aliifanya ili kuhakikisha ujenzi wa shule hiyo unakamilika.

Mzee Semhonda ambaye ana elimu ya darasa la saba, amesema yeye ni mkulima na mkazi wa kijiji cha Mogitu. Hajawahi kuajiriwa mahali popote.

Waziri Mkuu kesho atamalizia ziara yake mjini Babati kwa kuzindua daraja la Bonga, atafanya mkutano wa hadhara na kufanya majumuisho ya ziara yake mkoani humo.

-ends-

 

 
Our website is...
 
mod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_counter
mod_vvisit_counterToday81
mod_vvisit_counterYesterday106
mod_vvisit_counterThis week290
mod_vvisit_counterLast week798
mod_vvisit_counterThis month2447
mod_vvisit_counterLast month3555
mod_vvisit_counterAll days524632
Copyrights ©2013, The United Republic of Tanzania, Prime Minister's office All Rights Reserved