Logo
Tuesday, 21 February 2017 23:24    PDF 

Waziri Mkuu ataka Madiwani wasimamie makusanyo

*Ataka Wakurugenzi na Wakuu wa idara watoe taarifa kila mara

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema madiwani wanao wajibu wa kusimamia makusanyo ya fedha kwenye halmashauri zao na ametaka wakuu wa idara wawape taarifa kila inapobidi.

Alitoa kauli hiyo jana (Jumatatu, Februari 20, 2017) wakati akizungumza na madiwani na watumishi wa umma wa wilaya ya Mbulu kwenye kikao kilichofanyika katika hospitali ya Haydom wilayani Mbulu, mkoani Manyara.

Waziri Mkuu ambaye amejiwekea utaratibu wa kukutana na watumishi wa umma katika kila halmashauri, kila anapofanya ziara za mikoa, amesema anafanya hivyo ili kuwakumbusha watumishi wajibu walionao wa kuwatumikia wananchi ambao wameichagua na kuiweka Serikali madarakani.

“Serikali inatambua mchango mkubwa unaofanywa na watumishi wa chini na ndiyo maana katika ziara zangu nimeweka ratiba ya kukutana na watumishi wa umma ili kuwapa msimamo wa Serikali ya awamu ya tano katika kuwahudumia Watanzania,” alisema.

“Nimekuja kuwasisitiza watu wafanye kazi na Mheshimiwa Rais Magufuli anataka watumishi wafanye kazi ya kuwahudumia Watanzania bila ubaguzi. Msiwabague watu kwa uwezo wao wa kifedha, itikadi za siasa au kwa rangi zao,” alisisitiza.

“Tunataka muwahudumie wananchi kwa umahiri kila mmoja katika sekta yake. Hatutaki kusikia kauli za ‘njoo kesho’, ‘njoo kesho’ kwa sababu inajenga nafasi ya rushwa. Tunapambana na walarushwa kwa sababu wametupotezea fedha nyingi ambazo zingetumika kuwahudumia wananchi kwenye miradi ya maji au miradi mingine ya maendeleo,” alisema.

Alisema jambo kubwa ambalo anawasisitizia watumishi hao ni uadilifu na uaminifu kwani Serikali hivi imeamua kuleta fedha nyingi kwenye miradi ya maendeleo na inataraji fedha hizo zitatumika kule zilikopangiwa.

“Fedha za maendeleo ziende kutumika kwenye miradi iliyopangwa. Fedha hizi msiziguse kwa sababu zina moto. Mtumishi yoyote ukizichezea zitakuunguza. Kuweni makini na hizi fedha,” alisisitiza.

Alisema wakurugenzi wa halmashauri na wakuu wa idara washirikiane na madiwani na wawajulishe kila mara wanapopokea fedha kutoka Serikali kuu. “Ni lazima muwajulishe kuwa mmepokea fedha kiasi gani na zimekuja kwa ajili ya kazi gani mahsusi. Wao kwa mujibu wa madaraka yao, ni wasimamizi wa hizi fedha.”

“Hakikisha wanapata taarifa na ili kurahisisha mawasilano, wakuu wa idara mkipata fedha hizi ni lazima muwajulishe wasaidizi wenu ili wajue nini kinaendelea. Ushirikikishwaji ni kitu cha muhimu kwenye halmashauri zetu. Mkipata mafanikio wajulisheni pia madiwani wenu ili wakawasemee kwa wananchi,” alisisitiza.

Akitoa mfano kuhusu mtiririko wa fedha kwenye halmashauri, Waziri Mkuu alisema Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu iliomba sh. milioni 203.6 kwa ajili ya kununulia dawa na mpaka sasa Serikali imekwishatuma sh. milioni 175. “Halmashauri ya Mji wa Mbulu wameshapokea sh. milioni 88 kati ya sh. milioni 102 walizoomba kwa ajili ya dawa. Lakini pia wamepokea sh. milioni 117 kati ya sh. 137 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya zahanati na vituo vya afya,” aliongeza.

Akifafanua kuhusu maslahi ya watumishi wa umma, Waziri Mkuu alisema Serikali inajali maslahi ya watumishi na kwamba imeanza kulipa madeni ya nyuma ambapo walimu zaidi ya 63,000 wamelipwa sh. bilioni 29 na watumishi wa kada nyingine wamelipwa kiasi cha sh. bilioni 21.

Alisema Serikali pia imedhibiti malimbikizo ya watumishi yaliyotokana na likizo, kupanda madaraja, kupitia mfumo wa kielektroniki wa malipo ya mishahara kwa watumishi wa umma ambao umewezesha kuondoa tatizo la madai ya malimbikizo ya stahili zao. Mfumo huo unajulikana kama LAWSON.

Alisema mfumo huo ambao unatumika kwenye ajira za watumishi wote nchini, wa Serikali Kuu na wale wa Serikali za Mitaa umesaidia kutunza, kutuma na kuhuisha taarifa za watumishi kwa wakati na kwa ufanisi tangu mtu anapoajiriwa hadi inapofikia wakati wa kupandishwa madaraja na hata anapostaafu.

Waziri Mkuu leo anaendelea na ziara yake ya kikazi ya siku sita mkoani Manyara kwa kutembelea wilaya ya Hanang ambako atapokea taarifa ya wilaya hiyo atazungumza na watumishi wa umma, na kuzungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara.

-ends-

 

 
Our website is...
 
mod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_counter
mod_vvisit_counterToday81
mod_vvisit_counterYesterday106
mod_vvisit_counterThis week290
mod_vvisit_counterLast week798
mod_vvisit_counterThis month2447
mod_vvisit_counterLast month3555
mod_vvisit_counterAll days524632
Copyrights ©2013, The United Republic of Tanzania, Prime Minister's office All Rights Reserved