Logo
Tuesday, 28 February 2017 00:00    PDF 

Waziri Mkuu ataka mashirika ya umma yaishauri Serikali

 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameyataka mashirika na taasisi za umma yaangalie utendaji wa Serikali ya awamu ya tano katika kipindi cha mwaka mmoja na yatoe ushauri wa namna bora ya kuboresha maendeleo nchini.

Ametoa kauli hiyo leo asubuhi (Jumanne, Februari 28, 2017) wakati akifungua Mkutano wa kujadili Nafasi ya Mashirika ya Umma katika Utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano Ikulu jijini Dar es Salaam.

Akifungua mkutano huo wa siku moja kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, Waziri Mkuu amesema ana imani kuwa washiriki wa mkutano huo wataangalia uzoefu ambao Serikali imeupata katika mwaka mmoja tangu iingie madarakani na kushauri namna bora ya kukabiliana ba vikwazo ambavyo vimejitokeza.

“Ninaamini mtaangalia uzoefu tulioupata kwa mwaka mmoja uliopita ambao Serikali hii imekuwa madarakani, mtaangalia ni mpango upi tuliopanga na upi umefanikiwa ama upi umekwama na nini kilisababisha vikwazo hivyo vitokee,” amesema.

Alisema matarajio ya Serikali kutokana na mkutano huo ni kwamba washiriki wa wataainisha namna mashirika ya umma yatakavyoweza kuchangia katika utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo hususan katika kujenga uchumi wa viwanda.

“Ninaamini mtaweka wazi hatua za haraka za kisheria na za kimuundo zinazotakiwa kuchukuliwa na Serikali ili ushiriki wa mashirika yetu usikumbane na mikingamo ya kisheria na vikwazo vya mazoea ya watumishi na watendaji,” amesema.

Amesema anatarajia kuwa washiriki wa mkutano huo watapendekeza namna mashirika yanavyoweza kuunganisha nguvu katika kutekeleza aina fulani ya mradi na ushirika huo ukawa na tija.

“Kutokana na majadiliano yenu, naamini mtaainisha vihatarishi (risks) vilivyopo kwa mashirika ya Serikali kushiriki moja kwa moja kwenye utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo na kupendekeza mbinu za kukabiliana na vihatarishi hivyo; na pia mtashauri namna bora ya kutekeleza mapendekezo yenu bila kuathiri majukumu mahsusi ya uanzishwaji wa mashirika,” amesema.

Amesema yaya binafsi anasubiri kwa shauku kubwa, muhtasari wa mkutano huo ambao anataraji utakuwa na mapendekezo yanayotekelezeka ya namna gani mashirika yaliyopo nchini kwa umoja wake au moja moja yanavyoweza kushiriki kikamilifu kwenye ajenda hiyo ya maendeleo.

-ends-

 

 
Our website is...
 
mod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_counter
mod_vvisit_counterToday81
mod_vvisit_counterYesterday106
mod_vvisit_counterThis week290
mod_vvisit_counterLast week798
mod_vvisit_counterThis month2447
mod_vvisit_counterLast month3555
mod_vvisit_counterAll days524632
Copyrights ©2013, The United Republic of Tanzania, Prime Minister's office All Rights Reserved