Logo
Tuesday, 28 February 2017 00:00    PDF 

Ujenzi wa kiwanda cha saruji Tanga ni faraja - Waziri Mkuu

 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema uamuzi wa kampuni ya Kichina kujenga kiwanda kikubwa cha saruji mkoani Tanga ni wa faraja kutokana na mahitaji makubwa yaliyopo nchini.

Ametoa kauli hiyo jioni hii (Jumanne, Februari 28, 2017) wakati akizungumza na ujumbe wa kampuni ya Sinoma na kampuni ya Hengya Cement (T) Ltd ambao ulimtembelea ili kumpa taarifa ya uamuzi wao huo. Ujumbe huo ulifuatana na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Bw. Martin Shigella na viongozi kutoka TIC na Wizara ya Viwanda na Biashara.

Waziri Mkuu amesema ujenzi wa kiwanda hicho ni fursa kubwa kwa sababu utaenda sambamba na ujenzi wa bomba la mafuta la Hoima - Tanga na kwamba saruji ambayo itatengenezwa itapata soko la uhakika.

Amesema licha kuwa mkoa huo una viwanda vingine vya saruji bado mahitaji ya saruji nchini ni makubwa na kwamba ongezeko la viwanda litapaswa lisaidie kushusha bei ya saruji. “Tunahitaji kuwa na viwanda vingi zaidi ili bei ya mfuko wa saruji ishuke na wananchi waweze kumudu bei,” amesema.

Amesema kuendelea kuwepo kwa viwanda vingi katika mkoa huo, ni tija kwa nchi kwani mkoa huo ulikuwa na viwanda vingi kama ilivyo kwa Dar es Salaam na Morogoro lakini vikafa kutokana na mabadiliko ya teknolojia na kwa vile wenye viwanda hawakuwa tayari kuendana na kasi hiyo ya mabadiliko.

“Wawekezaji wa sasa wako tayari kwenda na teknolojia ya kisasa kwa hiyo Watanzania wawe tayari kuwapokea wawekezaji ili tushirikiane nao kukuza uchumi wetu na Tanzania itoke hapa ilipo na kwenda kwenye uchumi wa kati,” amesema.

Mapema, akielezea hatua ambazo wameshafikia, Rais wa kampuni ya Sinoma, Bw. Peng Jianxin alisema uwekezaji wao utafanyika kwa awamu mbili na kwamba katika awamu ya kwanza wameshatenga mtaji wa dola za Marekani bilioni moja (trilioni 2.2).

Alisema pindi uzalishaji utakapoanza, wanataraji kutoa asilimia 70 na kuiuza nje ya nchi ilhali asimilia 30 itakayobakia ndiyo italengwa kwa ajili ya matumizi ya ndani.

“Tukianza uzalishaji tunataraji kutumia bahari ya Hindi kusafirisha saruji yetu kwenda Somalia, Kenya na Msumbiji, lakini pia ziko nchi za Sudan, DRC na Uganda ambao wako tayari kuchukua saruji tutakayozalisha.”

Alisema wakati ujenzi wa kiwanda ukitarajiwa kuanza Mei mwaka huu, wanataka pia waanze ujenzi wa gati yao (wharf) katika kipindi hichohicho ili iwe rahisi kusafirisha mzigo moja kwa moja kutoka kiwandani.

Pia alisema ili kuepuka kutumia malori kusomba mizigo, watajenga pia njia maalum ya juu (conveyor belt) ya kutolea malighafi kutoka mgodini hadi machimboni.

-ends-

 

 
Our website is...
 
mod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_counter
mod_vvisit_counterToday81
mod_vvisit_counterYesterday106
mod_vvisit_counterThis week290
mod_vvisit_counterLast week798
mod_vvisit_counterThis month2447
mod_vvisit_counterLast month3555
mod_vvisit_counterAll days524632
Copyrights ©2013, The United Republic of Tanzania, Prime Minister's office All Rights Reserved