Logo
Wednesday, 01 March 2017 00:00    PDF 

Waziri Mkuu akaribisha wawekezaji kutoka Italia

 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewakaribisha wawekezaji kutoka Italia ili waje kuwekeza kwenye viwanda na usindikaji bidhaa za mifugo na uvuvi kwa sababu ni eneo wanalolimudu vizuri.

“Tumedhamiria kujenga Tanzania ya viwanda, tunawakaribisha wawekezaji kutoa Italia ili waje kuwekeza kwenye viwanda vya usindikaji mazao ya mifugo pamoja na uvuvi kwa sababu tunatambua kuwa ninyi mmebobea katika eneo hilo,” alisema.

Ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumanne, Februari 28, 2017) alipokutana na Balozi wa Italia nchini Tanzania, Bw. Roberto Mengoni kwenye makazi yake Oysterbay jijini Dar es Salaam.

“Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kujenga uchumi wa viwanda ili kuongeza ajira na kuondoa umaskini miongoni mwa wananchi wake. Tunahitaji uwekezaji mkubwa kwenye maeneo mbalimbali,” alisema Waziri Mkuu.

Kwa upande wake, Balozi Mengoni alimweleza Waziri Mkuu kwamba katika muda wa miezi nane ambayo ameishi hapa nchini, amebaini kuwa Tanzania ni nchi yenye fursa nyingi za kiuchumi. “Ni soko kubwa ambalo halijaguswa (untapped market) hasa kwenye masuala ya viwanda na uwekezaji.

Hata hivyo, Balozi huyo alikiri kwamba bado wananchi wengi wa Italia wanahitaji kupatiwa elimu zaidi juu ya fursa zilizopo hapa nchini. “Hadi leo kuna Waitaliano ambao hawajui kuwa Mlima Kilimanjaro uko Tanzania. Wengi wanajua uko Kenya, kwa hiyo elimu zaidi inahitajika katika suala zima la kutangaza utalii wa Tanzania,” alisema.

Alisema tangu afike nchini, wawekezaji kutoka Italia wameonesha nia ya kuwekeza kwenye nishati jadidifu, kiwanda cha kutengeneza nguo za michezo (sports wear) na kwamba wafanyabiashara wengine zaidi wanatarajia kuja hapa nchini.

Ili kutoa uelewa mpana kwa wafanyabiashara na raia wa Italia, ubalozi kwa kushirikiana na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) tumeandaa mkutano mkubwa kuhusu biashara na uwekezaji utakaotoa maelezo kuhusu fursa zilizopo Tanzania katika nyanja mbalimbali.

“Mkutano huu utakaofanyika Mei 6, mwaka huu, utawalenga zaidi wafanyabiashara na utajikita kwenye maeneo makuu sita ambayo ni viwanda vya usindikaji, viwanda vya nguo (textiles), ngozi na mazao yake, miundombinu, nishati na utalii,” alisema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amekutana na Balozi wa Japan hapa nchini, Bw. Masaharu Yoshida ambapo katika mazungumzo yao wamejadiliana mambo mbalimbali yakiweo ya miundombinu, elimu na nishati.

-ends-

 

 
Our website is...
 
mod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_counter
mod_vvisit_counterToday81
mod_vvisit_counterYesterday106
mod_vvisit_counterThis week290
mod_vvisit_counterLast week798
mod_vvisit_counterThis month2447
mod_vvisit_counterLast month3555
mod_vvisit_counterAll days524632
Copyrights ©2013, The United Republic of Tanzania, Prime Minister's office All Rights Reserved