Logo
Friday, 24 March 2017 00:00    PDF 

Majaliwa: Tuna utashi wa dhati kuboresha uwekezaji

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli ina utashi wa dhati wa kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara nchini.

Amesema Tanzania imefanya mageuzi makubwa ya kiuchumi kwa kubadili mifumo yake ya kisheria, kitaasisi na kifedha ili kuhakikisha wawekezaji wanahudumiwa ipasavyo na kupewa umuhimu wanaostahili kwani ni wadau muhimu kwa maendeleo ya Taifa.

“Serikali imefanya jitihada za kuondoa rushwa na urasimu katika sekta ya umma, hivyo tuwakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara wa Mauritius kuja kuwekeza nchini.”

Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana (Alhamisi, Machi 23,2017) wakati akifungua Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Mauritius lililofanyika kwenye hoteli ya Labourdonnaise mjini  Port Louis nchini Mauritius. Kongamano hilo  liliandaliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).

Alisema Tanzania ina uchumi imara unaofuata misingi ya soko huria, ambapo mwekezaji ana uhuru wa kufanya biashara bila ya kuingiliwa na Serikali; hivyo sekta binafsi imepewa kipaumbele katika shughuli za kiuchumi na kibiashara nchini.

“Kwa niaba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Magufuli nawakaribisha  kwa mikono miwili mje kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali zikiwemo za viwanda na utalii, mje mtembelee vivutio vya utalii na kupata burudani ya aina yake. Kwa wafanyabiashara mliopo hapa,  Tanzania ni mahali pazuri kwa kuwekeza,” alisema.

Alisema TIC na Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar kwa pamoja vimeweka taratibu ambazo zinamwezesha mwekezaji kupata mahitaji yake muhimu ya kuwekeza katika kituo kimoja (One Stop Centre).

Alibainisha baadhi ya mahitaji hayo kuwa ni huduma za kusajili kampuni, kulipia kodi, masuala ya uhamiaji, ardhi, leseni za biashara na masuala mengine yanayohusu uwekezaji; hali ambayo alisema inachangia Tanzania kupata wawekezaji wengi kutoka ndani na nje.

Waziri Mkuu alisema wawekezaji wanaokuja kuwekeza Tanzania wanatoka katika nchi mbalimbali kama Marekani, Canada, Afrika Kusini, Kenya, Australia, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na hivi karibuni inatarajia wawekezaji kutoka Mauritius.

“Ujio wa wawekezaji hawa haukuwa wa bahati bali ni kutokana na mazingira mazuri yaliyowekwa na Serikali pamoja na  suala zima la soko kubwa la bidhaa zao na huduma. Soko hili linalozidi watu milioni 300 katika nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika, linatoa uhakika wa soko kubwa kwa mwekezaji yeyote anayekuja Tanzania.”

“Kuwekeza nchini Tanzania kunampa fursa mwekezaji kupata fursa maalumu kupitia Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) na ile ya Kusini mwa Afrika (SADC) pamoja na soko la nchi ambazo hazipakani na bahari. Nchi ambazo Tanzania ina mahusiano nazo mazuri ya kibiashara ni Rwanda, Burundi, Uganda, Malawi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Zambia.

Waziri Mkuu aliongeza kuwa katika kuheshimu wawekezaji, Tanzania  imesaini mikataba mbalimbali inayolenga kuwalinda popote walipo kama Multilateral Investment Guarantee Agency (MIGA) na Africa Trade Insurance Agency.

Alisema Tanzania mbali ya hali ya amani na utulivu wa kisiasa, pia imebarikiwa kuwa na utajiri mkubwa wa rasilimali asilia ambazo zinatoa fursa nzuri kwa mwekezaji. “Hii ni pamoja na ardhi yenye rutuba nzuri kwa kilimo, madini ya kila aina kuanzia dhahabu, almasi, makaa ya mawe, tanzanite, chuma na gesi asilia.”

Kongamano hilo lilihudhuriwa na Waziri Mkuu wa Mauritius, Mheshimiwa Pravind Kumar Jugnauth; Waziri wa Mambo ya Nje wa Mauritius, Bw. Seetanah Lutchmeenaraidoo; Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Khalid Salum Mohammed na  Balozi wa heshima wa Tanzania nchini Mauritius, Bw. Merday Venkatasamy.

Wengine ni Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Bw. Cliford Tandari; Mwenyekiti wa ‪Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Bw. Godfrey Simbeye pamoja na Maofisa wa Serikali ya Tanzania na Mauritus.

-ends-

 
Our website is...
 
mod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_counter
mod_vvisit_counterToday16
mod_vvisit_counterYesterday120
mod_vvisit_counterThis week496
mod_vvisit_counterLast week810
mod_vvisit_counterThis month2993
mod_vvisit_counterLast month3838
mod_vvisit_counterAll days521623
Copyrights ©2013, The United Republic of Tanzania, Prime Minister's office All Rights Reserved