Logo
Tuesday, 06 June 2017 00:00    PDF 

HOTUBA YA MHESHIMIWA KASSIM M. MAJALIWA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KATIKA HAFLA YA UZINDUZI WA USAMBAZAJI WA VIFAA VYA MAABARA KWA SHULE ZA SEKONDARI TANZANIA BARA, ULIOFANYIKA LUGALO DAR ES SALAAM, TAREHE 06 JUNI 2017


Mheshimiwa Joyce Lazaro Ndalichako (Mb.), Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia;

Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi (Mb.), Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa;

Mheshimiwa Paul Makonda Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;

Mheshimiwa Ali Salum Hapi, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni;

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Mama Maimuna Tarishi;

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo;

Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais –TAMISEMI, Bw. Tixon Nzunda;

Mnadhimu Mkuu wa Jeshi, Luteni Jenerali James Mwakibolwa;

Wakurugenzi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia;

Afisaelimu wa Mkoa wa Dar es Salaam;

Washirika wa Maendeleo mliopo hapa;

Viongozi wa Elimu na Viongozi wa Dini mliopo;

Walimu Wakuu, Walimu na Wanafunzi;

Wanahabari, Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana.

Habari za asubuhi.

UTANGULIZI

Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana siku ya leo kwa ajili ya shughuli hii muhimu.

Nitumie fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Prof. Joyce Ndalichako (Mb) na Kamati ya Maandalizi, kwa kunialika kushiriki kwenye tukio hili muhimu kwa ustawi wa nchi yetu na mustakbali wa elimu ya sayansi nchini. Ninawashukuru sana.

Nakupongeza sana Mheshimiwa Waziri na timu yako kwa kutoa kipaumbele na msukumo mkubwa katika elimu ya sayansi na kufuatilia kwa karibu maslahi ya watoto wenye mahitaji maalum. Nawasihi muendelee hivyo kwa sababu bado tunalo jukumu la kuhakikisha vifaa zaidi vinapatikana.

Ninakushukuru pia Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi (Mb.), Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, kwa kutunza vifaa hivi na kukubali kuvisambaza kwenye shule zetu zilizoko kwenye maeneo mbalimbali nchini kote. Mwaka 2015 mliifanya vizuri kazi kama hiyo katika usambazaji wa vitabu nchini kote.

Nitumie fursa hii pia kumpongeza Mheshimiwa, George Simbachawene (Mb.) Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kuratibu zoezi hili kwa kushirikiana na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Kipekee kabisa, ninaishukuru Benki ya Dunia, Serikali ya Uingereza, Serikali ya Sweden pamoja na Shirika la Global Partnership for Education (GPE) walioshirikiana na Serikali kusaidia upatikanaji wa vifaa hivi. Kwa kushirikiana nasi kwenye sekta ya elimu, mnakuwa mmetufundisha namna ya kuvua samaki, badala ya kutupatia samaki. Excellencies, on behalf of the Government and the peoples of Tanzania, I thank you very much for your generosity. Kwa niaba ya Serikali ninawaahidi kwamba vifaa hivi vitatumika kama ilivyokusudiwa na vitatunzwa vizuri ili vinufaishe watoto wengi zaidi.

UMUHIMU WA HAFLA HII

Ndugu Wananchi;

Siku ya leo ni siku muhimu sana kwa sekta ya elimu nchini. Hii ni kutokana na umuhimu wa masomo ya sayansi nchini. Usambazaji wa vifaa vya Maabara kwa shule 1,696 za Sekondari nchini ni mwendelezo wa utekelezaji wa Ilani ya CCM inayosisitiza elimu ya kisasa na yenye mwelekeo wa Sayansi na Teknolojia kwa lengo la kujenga uchumi wa kisasa wa Taifa linalojitegemea.

Wakati nazindua Bunge la Bajeti linaloendela, nilieleza umuhimu wa watoto wetu kutoa kipaumbele kwenye masomo ya sayansi. Nilisema, endapo watoto wetu hawatasoma masomo ya sayansi, watabaki kuwa watazamaji tu kwenye uchumi wa viwanda. Tutumie elimu hii ili itusaidie kuendesha viwanda vyetu.

Hivyo, tukio hili ni kudhihirisha utayari wa Serikali kuweka mazingira wezeshi kwa watoto wetu watakaojiunga kwenye masomo ya sayansi. Hivyo, tunayo kila sababu ya kujivunia hatua hii, na hivyo, nitumie fursa hii kuwasihi wazazi kote nchini, waendelee kuwahamasisha watoto wao wachangamkie masomo ya sayansi.


SHULE ZA SEKONDARI ZITAKAZONUFAIKA NA MGAO WA VIFAA VYA MAABARA


Ndugu Wananchi,

Kama alivyobainisha Mheshimiwa Waziri, vifaa vya Maabara vitatolewa katika shule za Tanzania Bara zilizokamilisha majengo na miundombinu muhimu ya maabara. Hivyo, ni vizuri sasa Halmashauri zote ambazo shule zake hazijakamilisha ujenzi wa maabara ziongeze bidii ili ziweze kunufaika na utaratibu huu. Mheshimiwa Waziri wa Nchi TAMISEMI (simamia suala hili)!


Tumeanza na waliokamilisha ujenzi wa maabara, lakini kutakuwa na utoaji vifaa kwa awamu ya pili na ya tatu kadri wanavyokamilisha ujenzi. Nia yetu ni kuhakikisha kuwa shule zetu zote 4,587 zinapata vifaa hivi. Tunapoimarisha elimu nchini ni vizuri jitihada hizi zikahusisha pande zote mbili za Muungano. Hivyo, wekeni utaratibu wa kubadilishana uzoefu na wenzetu wa Zanzibar, ili jitihada hizi zinufaishe pande zote mbili za Muungano.


Ndugu walimu na Wanafunzi,

Kiasi kikubwa cha fedha kimetumika kununua vifaa hivi, huu ni uwekezaji mkubwa ambao kila mmoja wetu ana wajibu wa kuulinda, ili uweze kunufaisha wanafunzi wengi zaidi. Jiwekeeni utaratibu wa namna ya kuvitunza, na kwa yeyote atakayeviharibu kwa maksudi au kwa uzembe, alipie gharama halisi ya kifaa alichokiharibu. Ni matarajio yangu kwamba mtavitunza vifaa hivi na kuvitumia ipasavyo ili kusaidia kuinua ubora wa elimu ya sayansi na kupata wahitimu wenye ujuzi stahiki kwa maendeleo ya nchi yetu.


DHAMIRA YA KUENDELEA KUBORESHA ELIMU NCHINI NA UMUHIMU WA KUDUMISHA NIDHAMU SHULENI


Ndugu Wananchi,

Serikali itaendelea kuchukua hatua madhubuti zinazolenga kuboresha Elimu nchini ili kuwa na kizazi kilicho bora. Tutaendelea kutoa elimu bila malipo, kuboresha maslahi ya walimu na kufanya mapitio ya mara kwa mara kwenye mitaala yetu. Vilevile tunaziwezesha shule zetu ziwe na Maabara za kisasa ili watoto wapate elimu bora.

Hata hivyo, juhudi zetu hizo hazitakuwa na maana endapo nidhamu ya wanafunzi itakuwa mbaya. Hivyo, natoa wito kwa wazazi, walimu na jamii kwa ujumla kusimamia nidhamu ya watoto wetu, ili tujenge Taifa la wasomi wenye nidhamu na uzalendo kwa nchi yao. Mwanafunzi asiye na nidhamu asivumiliwe hata kidogo.

Vilevile, tuendelee kuwafuatilia watoto wetu na kuwalinda dhidi ya mimba za utotoni na kujiingiza kwenye matumizi ya pombe na dawa za kulevya. Hatuwezi kufanya uwekezaji mkubwa kama huu, kisha watu wachache wasio na maadili wanawakatisha masomo watoto wetu kwa kuwarubuni na kuwapa ujauzito, au kuwaingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya. Ni lazima hatua zichukuliwe dhidi ya watu hawa wanaohujumu jitihada za Serikali za kuwawezesha watoto wetu kupata elimu.

HITIMISHO

Baada ya maelezo hayo, napenda sasa kutamka kuwa zoezi la usambazaji wa vifaa vya maabara limezinduliwa rasmi.

Asanteni sana kwa kunisikiliza

 

 
Our website is...
 
mod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_counter
mod_vvisit_counterToday82
mod_vvisit_counterYesterday106
mod_vvisit_counterThis week291
mod_vvisit_counterLast week798
mod_vvisit_counterThis month2448
mod_vvisit_counterLast month3555
mod_vvisit_counterAll days524633
Copyrights ©2013, The United Republic of Tanzania, Prime Minister's office All Rights Reserved