Logo
VISION FUND YAUNGANISHA WAKULIMA 9000 KUPITIA UWEZESHAJI WA MIVARF
Wednesday, 17 May 2017 00:00    PDF 

Programu ya Miundo Mbinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini (MIVARF) imeijengea uwezo Benki ya Vision Fund na kuiunganisha na wakulima 9000 Nchini.

Akizungumza wakati wa mahojiano na waandishi wa habari Mei 17, 2017, Kaimu Mkurugenzi wa Benki ya Vision Fund Bibi Joyce Temu alisema, uwezeshaji kutoka programu ya MIVARF umeisaidia benki kuongeza huduma ambapo sasa kuna matawi 54 nchini na kuweza kuongeza idadi ya wakulima kufikia 9000 na kutoa mikopo ya shilingi milioni 232.

“MIVARF imeweza kutusaidia kujenga uwezo wa wafanyakazi wetu kwa kuwafundisha jinsi ya kutoa mikopo, kutoa elimu kwa wakulima juu ya kilimo bora, uhifadhi wa mazao bora, utunzaji wa vitabu ambapo kwa sasa wakulima wanaweza kulima kilimo cha kisasa na chenye tija,” amesema Bibi. Temu.

Aidha, MIVARF imeiwezesha Vision Fund kuboresha huduma zake za kibenki kutokana na kuboresha mifumo ya benki hiyo, awali huduma za kibenki zilikuwa zinaendeshwa kwa kutumia mifumo ya zamani baada ya uwezeshaji wa MIVARF benki hiyo imeweza kuboresha mifumo ya kibenki kwa kutumia mifumo ya Tehama, pia kutumia huduma za kibenki kwa njia ya simu ambayo imesaidia kuwafikia wateja wengi wa vijijini ambao ni wakulima.

“Uwezeshaji huu wa MIVARF umeiwezesha Vision Fund kuwaunganisha wakulima wa masoko kama vile (GAFCo, World Vision) na wadau wengine ili kuweza kuwawezesha wakulima kupata wigo mpana wa masoko yao na hata kuanzisha huduma za Bima kwenye masuala ya Kilimo”, alisema Bibi Temu.

Alifafanua kuwa kabla ya kujiunga na MIVARF, Benki ya Vision Fund haikuwa na uelewa wa kufanya kazi na watoa huduma (Service Providers) wakiwemo SEIDA na watoa huduma wengine ila kupitia MIVARF wameweza kufanya kazi na watoa huduma hao ambao wameweza kuwahamasisha wakulima na kuwaweka katika vikundi na imekuwa rahisi kuwahudumia wakulima wengi zaidi katika mikopo pamoja na kutoa huduma kwa urahisi.

“MIVARF imetuwezesha pia kufanya kazi na kujenga mahusiano mazuri na Serikali na kuweza kuendesha shughuli zetu za kila siku, Vision Fund imekuwa Benki ya kipekee kutokana na ufadhili wa MIVARF”, alisisitiza Bibi Temu.

Benki ya Vision Fund imeweza kuongeza wigo mpana na kufika katika Mikoa ya Simiyu Shinyanga, Mwanza na Geita, hii ni kutokana na uwezeshaji uliofanywa na MIVARF na kusaidia kuwafikia wakulima wa mikoa hiyo alieleza.

Pamoja na hayo, MIVARF imeweza kubadilisha hasa maisha ya wakulima kwani, idadi kubwa ya wakulima wameweza kupata mikopo kupitia Benki ya Vision Fund na wameweza kuboresha kilimo chao na kupata mazao bora yenye thamani.

“Upatikanaji wa masoko ya kuuzia mazao yao umewawezesha wakulima kuongeza vipato vyao na kuboresha maisha yao kwa ujumla wakulima wameweza kupeleka watoto shule, kupata makazi bora, pamoja na lishe hii imeenda sambamba na lengo kuu la Programu ya MIVARF la kuwahudumia wananchi wa kipato cha chini na kuwakwamua kiuchumi”, alisema.

Aidha, Matarajio yetu Vision Fund ni kuendelea kuwahudumia wakulima na kuongeza wigo zaidi kwani asilimia 80 ya idadi ya Watanzania ni wakulima, ambao bado wanahitaji kupata huduma zetu za kibenki kwa kuwapa elimu ya kilimo, kuwatafutia masoko, kuwapa elimu ya kuweka na kukopa hivyo kutokana na ufadhili wa MIVARF bado tuna nafasi kubwa ya kuweza kuwafikia kama benki na kuleta maendeleo katika nchi yetu, alisisitiza, Bibi Temu.

Programu ya Miundombinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini (MIVARF) inagharamiwa na Serikali ya Tanzania ikishirikiana na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB) chini ya uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu. Lengo likiwa ni kuongeza kipato kwa wakulima na kuchangia katika kuboresha uhakika wa chakula kwa Kaya zenye kipato cha chini hasa maeneo ya vijijini.

-Mwisho-

 

 
Our website is...
 
mod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_counter
mod_vvisit_counterToday104
mod_vvisit_counterYesterday117
mod_vvisit_counterThis week283
mod_vvisit_counterLast week825
mod_vvisit_counterThis month2168
mod_vvisit_counterLast month3455
mod_vvisit_counterAll days513803
Copyrights ©2013, The United Republic of Tanzania, Prime Minister's office All Rights Reserved