Logo
Monday, 31 July 2017 18:42    PDF 

Waziri Mkuu aagiza TAKUKURU iwachunguze vigogo 12

*Ni baada ya kulisababishia Jiji la Mbeya hasara ya sh. bilioni 63

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Mbeya, Bw. Emmanuel Kiabo amkamate na kumhoji aliyekuwa Meya wa Jiji la Mbeya, Bw. Athanas Kapunga na wenzake 11 kwa tuhuma za kuisababishia Serikali hasara ya sh. bilioni 63.448.

Waziri Mkuu amesema watumishi hao wanatakiwa kuchukuliwa hatua stahiki za kisheria kwa kuwa wameisababishia Serikali hasara kubwa katika mradi wa ujenzi wa soko la Mwanjelwa, lililoko Jijini Mbeya ambalo hadi sasa halijaonyesha tija.

“Serikali hii haiwezi ikawaachia watu hawa ambao wameisababishia hasara kubwa kiasi hiki tena kwa halmashauri moja. Kama wako humu ndani, naagiza wakamatwe na waanze kuhojiwa na wale ambao wamestaafu au kuhamishwa kituo cha kazi wasakwe popote walipo ili nao waje kujibu hoja.”

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Julai 31, 2017) wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri za wilaya ya Mbeya na Halmashauri ya Jiji la Mbeya katika mkutano uliofanyika ukumbi wa Benjamin Mkapa.

Wengine ni waliowahi kuwa Wakurugenzi wa Jiji hilo ambao ni Bw. Mussa Zungiza, Bi. Elizabeth Munuo, Bw. Juma Idd na Dkt. Samwel Lazaro aliyekuwa akikaimu nafasi ya Ukurugenzi.

Pia wamo aliyekuwa Mweka Hazina wa Jiji, Bw. James Jorojik pamoja na waliokuwa wajumbe wa Bodi ya Zabuni ambao ni Bw. Mussa Mapunda, Bw. Samweli Bubengwa, Bw. Davis Mbembela, Bi. Lydia Herbert na Bw. Bernard Nsolo ambao walipitisha nyongeza ya mradi huo bila ya kuzingatia maslahi ya Jiji pamoja Emily Maganga ambaye hakuishauri vizuri bodi hiyo.

Amesema mradi huo wa soko la Mwanjelwa uligubikwa na changamoto nyingi kuanzia hatua za awali ambapo hata uchukuaji wa mkopo haukuwa umezingatia mpango mkakati wa biashara, hivyo kusababisha Halmashauri ya Jiji ichukue mkopo zaidi ya kiasi kilichokusudiwa.

Waziri Mkuu amesema mbali na kuzidisha kiasi cha mkopo, hata baada ya kukamilika kwa ujenzi, watuhumiwa hao waligushi mikataba ya upangaji, jambo ambalo ni kinyume na matakwa ya Sheria ya Manunuzi ya Umma. Pia waligawa vizimba kwa wafanyabiashara bila kupitia mchakato wa manunuzi.

“Hata wahanga ambao walikuwepo awali kabla ya kuungua kwa soko hawakupewa kipaumbele katika mchakato wa upangishaji wa soko jipya, ambapo kwa hali ya kawaida ilitarajiwa wangekuwa wa kwanza kufikiriwa kutokana na hasara waliyoipata baada ya kuunguliwa mali zao,” amesema.

Pia Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Bw. Amos Makalla akutane na Madiwani wa Halmashauri ya Jiji na kuweka mikakati na namna ambavyo watapanga bei ya vizimba katika soko hilo ili wafanyabiashara wapange na wao waweze kuanza kupata fedha za kupunguza deni la benki.

-ends-

 

 
Our website is...
 
mod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_counter
mod_vvisit_counterToday70
mod_vvisit_counterYesterday121
mod_vvisit_counterThis week70
mod_vvisit_counterLast week867
mod_vvisit_counterThis month2188
mod_vvisit_counterLast month3157
mod_vvisit_counterAll days516980
Copyrights ©2013, The United Republic of Tanzania, Prime Minister's office All Rights Reserved