Logo
Friday, 28 July 2017 00:00    PDF 

Rais Magufuli aagiza Naibu Kamishna wa Uhamiaji asimamishwe kazi

*Ni baada ya kutoa vibali vya uraia kwa Wasomali 50

MHESHIMIWA RAIS Dkt. John Pombe Magufuli ameagiza Naibu Kamishna wa Uhamiaji, Bi. Grace Hokororo asimamishwe kazi kwa tuhuma za kuingiza nchini raia 50 wa Somalia na kuwapa vibali vya kuishi kinyume cha taratibu.

Kauli hiyo imetolewa leo (Ijumaa, Julai 28, 2017) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa mara baada ya kumaliza kikao chake na Makamishna wa Uhamiaji. Kikao hicho kilifanyika Makao Makuu ya Uhamiaji, Kurasini, jijini Dar es Salaam.

Pia Waziri Mkuu amemuagiza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Bw. Mwigulu Nchemba aunde tume ya uchunguzi kuhusu utoaji wa vibali vya uraia nchini.

Amesema haiwezekani raia wa kigeni wawe wanaingizwa nchini na kupewa vibali vya kuishi bila ya kufanyiwa uchunguzi wa kina. “Idara ya Uhamiaji tunaitegemea kusimamia mipaka yetu na kuziba mianya ya watu kuingia bila ya kufuata taratibu lakini kwa mapenzi yake, ofisa huyu ameruhusu Wasomali waingie nchini bila kufuata utaratibu.”

Waziri Mkuu amesema ni lazima uchunguzi ufanyike ili kubaini kwa nini alifanya hivyo, “Tutafute ni kitu gani kilimsukuma atoe vibali kwa Wasomali hao ambao hawakuwepo nchini; ni ajabu kwamba wameingia nchini na kupewa vibali moja kwa moja kwa mapenzi yake tu. Sasa hii ni dosari, hatuwezi  kuivumilia,” alisisitiza.

Amesema Serikali inaitegemea Idara ya Uhamiaji isimamie na kuzuia mianya ya uingiaji raia mbalimbali kutoka nje ya nchi bila ya kufuata taratibu, hivyo Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli ameagiza ofisa huyo asimamishwe kazi na uchunguzi ufanyike ili kubaini malengo yake.

"Hawa Wasomali aliowapa vibali vya kuishi wala hawakuwa wanaishi nchini, wameingia tu na kupewa vibali, hivyo Mheshimiwa Rais, Dkt. John Magufuli ameagiza ofisa huyo akae pembeni na achunguzwe kujua ni kitu gani kilimsukuma atoe vibali kwa raia hao."

Pia Waziri Mkuu ameiagiza Idara ya Uhamiaji iongeze udhibiti kwenye kitengo cha utoaji hati za kusafiria za kibalozi na kwa wanaomaliza muda wao wasipewe tena. "Lazima hati hizo zikaguliwe kwenye mipaka yote na maeneo yote ya usafiri ili kujua kama huyo anayeitumia bado anastahili hadhi hiyo na msiporidhika ichukueni kwani kuna watu wanazitumia vibaya,” aliongeza.

Hata hivyo, Waziri Mkuu ameagiza uchungzi wa kina ufanyike kwa watu wote walioomba hati za kusafiria pamoja na vibali vya makazi kama wanakidhi matakwa ya kisheria kabla ya kuwakabidhi.

-ends-

 

 
Our website is...
 
mod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_counter
mod_vvisit_counterToday69
mod_vvisit_counterYesterday121
mod_vvisit_counterThis week69
mod_vvisit_counterLast week867
mod_vvisit_counterThis month2187
mod_vvisit_counterLast month3157
mod_vvisit_counterAll days516979
Copyrights ©2013, The United Republic of Tanzania, Prime Minister's office All Rights Reserved