Logo
Saturday, 29 July 2017 00:00    PDF 

Majaliwa azindua meli mbili zilizoundwa na Mtanzania

*Aonya zisitumike kuvushia wahamiaji haramu na dawa za kulevya

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezindua meli mbili za mizigo za MV Njombe na MV Ruvuma zitakazotumika kusafirishia mizigo kwenye Ziwa Nyasa na akaonya zisitumike kuvushia wahamiaji haramu na dawa za kulevya.

Waziri Mkuu amezindua meli hizo zilizojengwa na kampuni ya Kitanzania ya M/S Songoro Marine Transport leo (Jumamosi, Julai 29, 2017) katika bandari ya Kiwira, wilayani Kyela akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Mbeya.

Amesema kukamilika kwa ujenzi wa meli hizo zilizogharimu sh. bilioni 11.253, ni utekelezaji wa ahadi ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Magufuli alizozitoa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 kwa lengo la kutatua changamoto ya usafiri wa abiria na mizigo kwenye Ziwa Nyasa.

Amesema ni jambo la faraja na la kujivunia kwa Serikali na wananchi kwa pamoja kushuhudia meli zilizotengenezwa na Mtanzania, zikiwa zimekamilika tayari kuanza kazi ya kuwahudumia wananchi, ambapo awali suala hilo lilikuwa likifanywa na raia wa kigeni.

Amesisitiza kwamba meli hizo zitumike kukuza uchumi wa wananchi kwa kusafirisha mizigo na biashara halali kati ya nchi za Tanzania na Malawi na zisitumike kama eneo la kuingiza wahamiaji haramu pamoja na dawa za kulevya nchini.

Waziri Mkuu amewataka wananchi wa maeneo hayo kuwa walinzi na kuhakikisha meli hizo zifanya shughuli halali za kiuchumi ambazo zitawaletea tija wao na Taifa kwa ujumla na kamwe wasikubali zikatumika kama kichaka cha uhalifu.

“Changamoto ya usafiri wa mizigo katika Ziwa Nyasa itakuwa historia kwani meli hizi zitarahisisha usafiri na kupanua wigo wa biashara kati ya Tanzania na nchi za Malawi na Msumbiji, hivyo tunamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli kwa kutoa ahadi hii ambayo leo utekelezaji wake umekamilika.”

Awali, Naibu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) anayeshughulikia miundombinu, Mhandisi Karim Mataka alisema meli hizo ambazo ujenzi wake ulianza Juni 2015, zina uwezo wa kubeba tani 1,000 za mizigo kila moja.

Mhandisi huyo alisema mbali ya kukamilika kwa mradi huo, TPA pia imeingia mkataba na kampuni ya M/S Songoro Marine Transport Ltd kwa ajili ya ujenzi wa meli ndogo ya abiria yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na tani 300 za mizigo.

Mradi huo ambao upo katika hatua za mwisho kamilika, utagharimu sh. bilioni 9.12.

-ends-

 

 
Our website is...
 
mod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_counter
mod_vvisit_counterToday70
mod_vvisit_counterYesterday121
mod_vvisit_counterThis week70
mod_vvisit_counterLast week867
mod_vvisit_counterThis month2188
mod_vvisit_counterLast month3157
mod_vvisit_counterAll days516980
Copyrights ©2013, The United Republic of Tanzania, Prime Minister's office All Rights Reserved