Logo
Saturday, 29 July 2017 00:00    PDF 

Waziri Mkuu awapa siku mbili madiwani Kyela wamalize tofauti zao

*Asema wakiendelea, Serikali italivunja Baraza

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewapa siku mbili Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya wamalize tofauti zao zinazokwamisha utendaji wa Halmashauri hiyo na waendelee kufanya kazi walizotumwa na wananchi.

Tofauti hizo ambazo zimedumu kwa takriban mwaka mmoja, zimesababisha madiwani hao washindwe kufanya vikao, jambo linalokwamisha shughuli za maendeleo ya wananchi katika Halmashauri hiyo.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumamosi, Julai 29, 2017) wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Mbeya.

Amesema ikifika Jumatatu (Julai, 31, 2017) Madiwani hao wawe wamemaliza tofauti zao na wawaite wakuu wa Idara na kuwapa taarifa hiyo ili shughuli za maendeleo ziendelee kutekelezwa ndani ya Halmashauri hiyo.

"Baraza la Madiwani limegawanyika, mna mgogoro. Tunataka uishe na mshirikiane na mshikamane katika kufanya shughuli za maendeleo ili wananchi waweze kupata manufaa. Mkiendeleza migongano hatutawavumilia! Serikali ina uwezo wa kulivunja Baraza," ameonya.

Amesema baadhi ya Madiwani hao wanawatetea watumishi waliosimamishwa kazi kwa tuhuma za kuiibia Serikali mabilioni ya fedha, jambo ambalo amesema halikubaliki na halivumiliki. “Naombeni mmalize tofauti zenu mara moja, kabla sijaondoka.”

Hata hivyo, Waziri Mkuu ameiagiza Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Mbeya ihakikishe watumishi wote waliohusika kula fedha za umma wanachukuliwa hatua kama alivyopendekeza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

-ends-

 

 
Our website is...
 
mod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_counter
mod_vvisit_counterToday70
mod_vvisit_counterYesterday121
mod_vvisit_counterThis week70
mod_vvisit_counterLast week867
mod_vvisit_counterThis month2188
mod_vvisit_counterLast month3157
mod_vvisit_counterAll days516980
Copyrights ©2013, The United Republic of Tanzania, Prime Minister's office All Rights Reserved