Logo
Tuesday, 01 August 2017 00:00    PDF 

Waziri Mkuu atembelea mtambo wa kusafisha dhahabu Chunya

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametembelea na kujionea mtambo wa kisasa wa kusafisha dhahabu kwa asilimia  99 unaomilikiwa na kampuni ya Sunshine Group uliopo katika kata ya Matundasi, wilayani Chunya, mkoani Mbeya.

Ametembelea mtambo huo leo (Jumanne, Agosti 1, 2017) akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Mbeya na kusema kuwa mtambo huo ni wa kwanza kuweza kusafisha dhahabu kwa kiwango hicho hapa nchini.

Amesema kwa sasa hapa nchini, kampuni ya Sunshine Group ndiyo yenye mtambo wenye uwezo wa kusafisha dhahabu na kufikia asilimia 99 ukilinganisha na makampuni mengine yanayomiliki migodi.

Pia Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kufanya mazungumzo na makampuni mbalimbali yenye nia ya kuwekeza katika mradi wa ujenzi wa mtambo wa kuchenjulia makinikia ili kuweza kusafirisha dhahabu halisi.

Naye, Ofisa Madini Mkoa wa Mbeya, Mhadisi Said Makwama amesema dhahabu inayosafishwa katika mtambo huo ikipelekwa nje ya nchi inaingizwa sokoni moja kwa moja tofauti na migodi mingine.

Mhandisi huyo alisema sheria mpya ya madini imesaidia Serikali kupata kodi ya juu itokanayo na mrabaha wa asilimia sita na ‘clearance and inspection fee’ ya asilimia moja ya thamani ya madini  yanayosafirishwa ukilinganisha na mrabaha wa awali wa asilimia nne.

“Kutokana na uzalishaji uliofanyika mwezi Julai tu, Serikali imepata mrabaha wa sh. milioni 333 ukilinganisha na sheria ya zamani ambapo Serikali ingepata shilingi milioni 191. Sheria mpya imewezesha Serikali kupata mapato zaidi ya sh. milioni 142. Awali ilikuwa inapata  sh. milioni 191 kwa gramu 52. 518 kwa mgodi mmoja wa Sunshine,” amesema.

Kwa upande wake, mbunge wa Chunya, Mheshimiwa Victor Mwambalaswa ameiomba Serikali ikubali maombi ya Kampuni ya Sunshine ya kujenga mtambo wa kuchenjulia mabaki ya mchanga wa dhahabu wilayani Chunya ili iweze kuongeza fursa za ajira, ambapo Waziri Mkuu amesema suala hilo linashughulikiwa.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Sunshine Group, Bw. Leo Le alisema kampuni ya Sunshine Group ni miongoni mwa makampuni makubwa kutoka nchini China yaliyowekeza Tanzania, ambapo thamani ya uwekezaji wao ni zaidi ya Dola za Marekani milioni 100.

-ends-

 

 
Our website is...
 
mod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_counter
mod_vvisit_counterToday70
mod_vvisit_counterYesterday121
mod_vvisit_counterThis week70
mod_vvisit_counterLast week867
mod_vvisit_counterThis month2188
mod_vvisit_counterLast month3157
mod_vvisit_counterAll days516980
Copyrights ©2013, The United Republic of Tanzania, Prime Minister's office All Rights Reserved