Logo
Monday, 21 August 2017 00:00    PDF 

Waziri Mkuu: Watanzania imarisheni uzalendo

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Watanzania wote wahakikishe wanaboresha mshikamano wao pamoja na kuimarisha uzalendo kwa Taifa lao.

Ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumapili, Agosti 20, 2017) wakati akizungumza na wanafunzi wa Kitanzania wanaosomea udaktari nchini Cuba.

Waziri Mkuu ambaye yuko Cuba kwa ziara ya kikazi yenye lengo la kudumisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, alisema uzalendo kwa Taifa ni jambo muhimu.

“Uzalendo ni muhimu sana kwa sababu tumekosa fursa nyingi za kimaendeleo kutokana na baadhi ya wananchi kutokuwa wazalendo kwa Taifa lao. Kutokana na hali hiyo Serikali inawasisitiza wananchi wawe wazalendo na washirikiane kuhakikisha fursa za kimaendeleo zilizoko nchini zinaendelezwa,” alisema.

Alisema wakati Serikali inatekeleza miradi mingi kwa lengo la kukuza uchumi kutoka wa chini kwenda wa kati, ni vema wananchi wakashirikiana nayo ili kufanikisha azma hiyo.

Pia Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwasihi wanafunzi hao wazingatie sheria za nchi hiyo na wakumbuke kurudi nyumbani mara wamalizapo masomo yao.

Alisema Serikali inatambua uwepo wao wa kimasomo nchini Cuba na kwamba inatarajia kupata mchango mkubwa kutoka kwao punde wamalizapo masomo yao.

“Nawaomba msome kwa bidii na mfaulu mitihani yenu. Elimu yenu iwasaidie katika ajira na muweze kurejesha mikopo mliyopewa na Serikali ili iwanufaishe wengine,” alisisitiza.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwataka mabalozi wote wanaoiwakilisha Tanzania katika mataifa mbalimbali wahakikishe wanatangaza vivutio vya utalii.

Alisema Tanzania imejaliwa kuwa na vivutio vingi vya utalii, hivyo ni vema mabalozi wakavitangaza jambo ambalo litasaidia kuongeza idadi ya watalii wanaofika nchini.

Miongoni mwa vivutio vya utalii vilivyoko nchini ni pamoja na Mlima Kilimanjaro, visiwa vya Zanzibar, mbuga mbalimbali zenye wanyama wa aina tofauti tofauti.

Awali, Mwenyekiti wa wanafunzi hao, Bw. Goodchance Tarimo alimhakikishia Waziri Mkuu kwamba watarejea nyumbani mara baada ya kumaliza masomo yao nchini humo.

Alisema wao wana imani kubwa na Serikali na wanaunga mkono jitihada zinazofanywa na viongozi wa Taifa kwa lengo la kuboresha maendeleo pamoja na kukuza uchumi.

“Tunapongeza jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano katika kujenga uchumi wa viwanda, mapambano dhidi ya rushwa, ufisadi na ujenzi wa miundombinu ya kisasa.”

-ends-

 

 
Our website is...
 
mod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_counter
mod_vvisit_counterToday105
mod_vvisit_counterYesterday117
mod_vvisit_counterThis week284
mod_vvisit_counterLast week825
mod_vvisit_counterThis month2169
mod_vvisit_counterLast month3455
mod_vvisit_counterAll days513804
Copyrights ©2013, The United Republic of Tanzania, Prime Minister's office All Rights Reserved