Logo
Thursday, 24 August 2017 00:00    PDF 

Waziri Mkuu aitaka Wizara iongeze mbinu za kuvutia watalii

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii itafute mbinu bora za kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini ili kukuza sekta hiyo.

Amesema licha ya Tanzania kuwa na vivutio vingi vya utalii, idadi ya watalii wanaoingia nchini kwa mwaka ni ndogo, hivyo kuna haja ya kuboresha matangazo.

Waziri Mkuu aliyasema hayo jana (Jumatano, Agosti 23, 2017) wakati alipofanya ziara katika mji wa kitalii wa Varadero ulioko kwenye mkoa wa Matanzas nchini Cuba.

Alisema mji wa Varadero tu unaingiza watalii zaidi ya milioni moja kwa mwaka na unategemea kivutio kikubwa kimoja tu cha fukwe ambayo ina urefu wa kilomita 22.

Alisema idadi hiyo ni tofauti na Tanzania ambayo imejaliiwa kuwa na vivutio vingi vya utalii huku watalii wanaovitembelea ni wachache. “Tunatakiwa kujitangaza zaidi.”

Waziri Mkuu alitaja baadhi ya vivutio vya utalii ambavyo ni Mlima Kilimanjaro, mbuga za wanyama, miji ya kihistoria ya Kilwa, Bagamoyo, Stone Town pamoja na Mikindani.  “Vivutio vingine ni eneo la Olduvai George ambako binadamu wa kwanza aliwahi kuishi, hifadhi ya Gombe ambako kuna sokwe ambao wanaishi kama binadamu.”

Alisema Serikali itahakikisha jitihada zinafanyika katika kukuza sekta ya utalii ikiwa ni pamoja na kutangaza vivutio vilivyoko nchini ili kuweza kuongeza idadi ya watalii.

Kwa upande wake, Kiongozi wa Sekta ya Utalii katika mkoa wa Matanzas, Bw.  Luis Martinez de Armas alisema mji wa Varadero ni kivutio kikubwa cha utalii nchini Cuba.

Alisema kivutio kingine cha utalii ni hoteli zilizojengwa ndani ya bahari, maeneo ya kihistoria na migahawa inayouza vyakula vya asili vya nchi hiyo.

Bw. Luis alisema mwaka 1990 ndipo walianza kuendeleza sekta ya utalii katika mkoa wao na ulikuwa na hoteli 4,436 ambazo kwa sasa zimeongezeka na kufikia hoteli 20,696.

Hata hivyo, Bw. Luis alisema Tanzania ina vivutio vingi vya utalii na kwamba anavutiwa na Mlima Kilimanjaro pamoja na wanyama na viumbe vingine vilivyoko katika mbuga mbalimbali. Alisema wako tayari kushirikiana na Serikali kukuza sekta ya utalii.

-ends-

 

 
Our website is...
 
mod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_counter
mod_vvisit_counterToday105
mod_vvisit_counterYesterday117
mod_vvisit_counterThis week284
mod_vvisit_counterLast week825
mod_vvisit_counterThis month2169
mod_vvisit_counterLast month3455
mod_vvisit_counterAll days513804
Copyrights ©2013, The United Republic of Tanzania, Prime Minister's office All Rights Reserved