Logo
Sunday, 27 August 2017 00:00    PDF 

Waziri Mkuu akutana na Makamu wa Rais wa Cuba

*Asisitiza nia ya kufungua ubalozi nchini humo

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekutana na Makamu wa Rais wa Cuba, Bi. Gladys Bejarano na amemhakikishia nia ya Serikali kufungua ofisi za ubalozi wa Tanzania nchini humo.

Amesema Tanzania inayatambua na kuyathamini mahusiano mazuri ya kidiplomasia, kisiasa, kiuchumi, kielimu, kiafya na kiutamaduni kati yake na Cuba, hivyo inatarajia kufungua ubalozi nchini humo ili kurahisisha utendaji wa kazi za kibalozi.

Waziri Mkuu alikutana na Bi. Bejarano jana jioni (Jumamosi, Agosti 26, 2017) wakati alipokuwa akihitimisha ziara yake ya kikazi nchini Cuba. Malengo ya ziara yalikuwa ni kuimarisha na kudumisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.

“Tunatambua mahusiano mazuri yaliyopo kati Tanzania na Cuba, ambayo yalikuwepo kuanzia Serikali ya Awamu ya kwanza chini ya uongozi wa Baba wa Taifa, Hayati Mwl. Julius Nyerere, hivyo lazima tufungue ofisi za ubalozi na tutamleta balozi wetu hapa.”

Pia Waziri Mkuu ameishukuru Serikali ya Cuba kwa ujenzi wa kiwanda cha dawa za kuulia vijidudu vya malaria pamoja na ufadhili wa masomo ya udaktari inaoutoa kwa wanafunzi wa Kitanzania ambao wanasoma katika vyuo mbalimbali nchini humo.

Hata hivyo, aliiomba Serikali hiyo iendelee kutoa ufadhili wa masomo kwa madaktari hao hadi ngazi ya shahada ya uzamili kwa sababu Serikali ya Tanzania inawahitaji madaktari bingwa wengi kwa vile walioko nchini ni wachache.

Kwa upande wake, Makamu huyo wa Rais alimshukuru Waziri Mkuu kwa kufanya ziara nchini Cuba na alimhakikishia kwamba uhusiano wa Serikali yake na Serikali ya Tanzania utaendelea kuimarishwa kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.

Alisema Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. John Magufuli inafanya jitihada kubwa za kuhakikisha uchumi wake unakua kwa kasi jambo ambalo ni tofauti na mataifa mengine. “Nawapongeza kwa hatua za kimaendeleo mnazozifanya,” alisema.

Makamu huyo wa Rais alisema Serikali ya Cuba itaendelea kushirikiana na Tanzania kuboresha sekta za afya, utamaduni, kilimo, uchumi na elimu. Kuhusu ombi la kuongeza ufadhili wa shahada ya uzamili kwa madaktari, alisema amelipokea na atalifanyia kazi.

Awali, Balozi wa Tanzania nchini Canada, ambaye anasimamia nchi ya Cuba, Balozi Jack Zoka alisema Serikali ya Cuba ni miongoni mwa nchi zinazoshirikiana kwa karibu na Tanzania katika uboreshaji wa shughuli za maendeleo, hivyo uwepo wa ofisi za ubalozi nchini humo utazidi kuimarisha mahusiano hayo

-ends-

 

 
Our website is...
 
mod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_counter
mod_vvisit_counterToday47
mod_vvisit_counterYesterday124
mod_vvisit_counterThis week517
mod_vvisit_counterLast week867
mod_vvisit_counterThis month2635
mod_vvisit_counterLast month3157
mod_vvisit_counterAll days517427
Copyrights ©2013, The United Republic of Tanzania, Prime Minister's office All Rights Reserved