Logo
Thursday, 07 September 2017 00:00    PDF 

Serikali yatenga sh. bilioni 11 kukabili utapiamlo

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imetenga sh. bilioni 11 ili kukabiliana na utapiamlo na amemtaka kila mdau wa lishe aonyeshe bayana mchango wake katika kukabiliana na utapiamlo nchini.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana jioni (Jumatano, Septemba 6, 2017) wakati akifungua mkutano wa nne wa mwaka wa wadau wa lishe wa kutathmini afua za lishe nchini kwenye ukumbi wa Hazina mjini Dodoma. Pia alizindua Mpango Mkakati Jumuishi wa Kitaifa wa Lishe wa mwaka 2016/2017 hadi 2020/2021 (Joint Multisectoral Nutrition Review).

“Viongozi wa Serikali katika ngazi mbalimbali wabaini kiwango cha utapiamlo katika maeneo yao, waonyeshe mbinu za kukabiliana na hali hiyo, wafanye tathmini ya ufanisi na watoe taarifa za ufanisi,” amesema.

Amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote, wahakikishe shilingi 1,000 ambazo Halmashauri zilielekezwa kutenga kwenye bajeti kutoka kwenye vyanzo vyao vya mapato kwa ajili ya kuboresha lishe kwa kila mtoto mwenye umri chini ya miaka mitano, zinatolewa na kutumika kama ilivyopangwa.

“Tulikubaliana kila Halmashauri lazima ikusanye makusanyo ya ndani kwa asilimia zaidi ya 80. Nilisema kiwango cha chini kisipungue asilimia 80. Na kupitia makusanyo hayo, ndipo tunapata fedha za kutenga kwa masula kama haya,” alisisitiza.

“Napenda kusisitiza kwamba ni lazima tufanye tathmini ya wapi tumefikia na wapi tumekwama katika kupambana na tatizo la utapiamlo hapa nchini,” alisema.

Pia amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya wahakikishe wanaisimamia mikoa na halmashauri zao kutekeleza afua zilizoainishwa katika Mpango Mkakati Jumuishi wa Kitaifa wa Lishe kwa kuzijumuisha katika mipango yao na kuzitengea fedha kwenye bajeti zao za kila mwaka.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu alisema amefurahishwa sana na kaulimbiu ya mkutano huo isemayo Lishe Bora: Msingi wa Maendeleo ya Viwanda Tanzania” ambayo kimsingi inaendana na dhamira yetu ya kujenga uchumi wa viwanda kama kichocheo cha mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu.

Pia alitumia fursa hiyo kuwahamasisha wadau wawekeze kwenye viwanda vya usindikaji wa vyakula vilivyoongezwa virutubishi ili kuongeza wingi wa vitamini na madini katika vyakula na hatimaye kuboresha lishe na afya ya jamii. “Napenda kusisitiza kuwa Serikali imeandaa mazingira mazuri ya uwekezaji hivyo tutumie fursa hii kikamilifu,” aliongeza.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kufungua mkutano huo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Bibi Ummy Mwalimu alisema kuna baadhi ya Halmashauri na mikoa hazijaunda Kamati za Afua za Lishe.

“Ninaomba Halmashauri na mikoa ikamilishe kuunda kamati za mikoa na pia watendaji wahakikishe fedha zimetengwa na zinatolewa. Lakini cha msingi ni kwamba fedha hizi zitumike kwa matibabu ya utapiamlo na masuala ya lishe na si vinginevyo,” alisisitiza.

-ends-

 

 
Our website is...
 
mod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_counter
mod_vvisit_counterToday38
mod_vvisit_counterYesterday124
mod_vvisit_counterThis week460
mod_vvisit_counterLast week825
mod_vvisit_counterThis month2345
mod_vvisit_counterLast month3455
mod_vvisit_counterAll days513980
Copyrights ©2013, The United Republic of Tanzania, Prime Minister's office All Rights Reserved