Logo
Sunday, 03 September 2017 00:00    PDF 

Fuatilieni maendeleo ya viwanda katika maeneo yenu - Majaliwa

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watendaji katika mikoa yote nchini wahakikishe wanafuatilia maendeleo ya viwanda mbalimbali katika maeneo yao.

Amesema mpango wa Serikali wa kujenga uchumi wa viwanda unalenga kuinua uchumi wa Taifa kutoka wa chini kwenda wa kati, hivyo ni muhimu kuvifuatilia.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana (Jumamosi, Septemba 2, 2017) alipozungumza na watendaji na wananchi wa mkoa wa Morogoro alipofanya ziara katika kiwanda cha MOPROCO.

Alisema licha ya kukuza uchumi wa Taifa, viwanda vitasaidia katika kutatua tatizo la ukosefu wa ajira hususani kwa vijana kwani vina uwezo wa kuajiri watu wengi.

“Viwanda hivi vinatupa uhakika wa ajira nchini kwa sababu vina uwezo wa kuajiri watu wengi na wa kada mbalimbali, hivyo ni muhimu tukafuatilia utendaji wake.”

Waziri Mkuu aliongeza kuwa mbali na kutoa ajira nyingi, pia viwanda vitawezesha wakulima kupata soko la uhakika la mazao yao na kukifanya kilimo kuwa na tija.

Alisema kwa muda mrefu sekta ya viwanda nchini ilikuwa haifanyi vizuri jambo ambalo lilisababisha kuongezeka kwa tatizo la ajira na mazao yalikosa soko.

Hata hivyo, Waziri Mkuu alitoa wito kwa wafanyakazi walioajiriwa katika viwanda mbalimbali kuwa waaminifu ili kuviwezesha viwanda hivyo kuendelea na uzalishaji.

Pia aliwataka wakulima waongeze uzalishaji wa mazao mbalimbali ili kuviwezesha viwanda viwe na uhakika wa upatikanaji wa malighafi ndani ya chini.

Awali, Meneja Mkuu wa kiwanda cha MOPROCO, Bw. Arif Abood aliiomba Serikali iongeze kodi kwenye mafuta yanayotoka nje ya nchi ili kulinda viwanda vya ndani.

Alisema uingizwaji wa mafuta kutoka nje ya nchi kwa kiasi kikubwa ulichangia kufungwa kwa viwanda vya ndani vya mafuta kwa sababu ya kukosa soko.

Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu aliambatana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Walemavu, Bibi Jenista Mhagama na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Bw. Charles Mwijage pamoja na maofisa wengine wa Serikali.

-ends-

 

 
Our website is...
 
mod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_counter
mod_vvisit_counterToday38
mod_vvisit_counterYesterday124
mod_vvisit_counterThis week460
mod_vvisit_counterLast week825
mod_vvisit_counterThis month2345
mod_vvisit_counterLast month3455
mod_vvisit_counterAll days513980
Copyrights ©2013, The United Republic of Tanzania, Prime Minister's office All Rights Reserved