Logo
Saturday, 14 October 2017 00:00    PDF 

‘Tumuenzi Baba wa Taifa kwa kuiga maisha yake’

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaomba Watanzania waendelee kumuenzi Hayati Baba wa Taifa, Mwl. Julius Nyerere kwa kuiga maisha yake na utendaji wake.

Ameyasema hayo leo (Jumamosi, Oktoba 14, 2017) aliposhiriki ibada maalumu ya kumuombea Mwl. Nyerere iliyofanyika katika Kanisa Katoliki la Minara Miwili, Zanzibar.

Ibada hiyo ya kumbukumbu ya miaka 18 ya kifo cha Mwl. Nyerere ni sehemu ya maadhimisho ya kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru uliozimwa leo katika mkoa wa Mjini Magharibi visiwani Zanzibar.

Katika ibada hiyo, Waziri Mkuu amewasisitiza wananchi wahakikishe wanamuenzi Mwl. Nyerere kwa kuendeleza mambo mema yote aliyoyafanya enzi za uhai wake.

Awali, Katibu wa Jimbo Katoliki Zanzibar, Padri Cosmas Shayo ambaye aliongoza ibada hiyo aliwaomba waamini wamuenzi Mwl. Nyerere kwa kudumisha umoja na mshikamano wa Taifa. “Hayati Baba wa Taifa Mwl. Nyerere aliwapenda watu wote bila kujali Imani zao wala itikadi zao. Alikuwa mzalendo na alitaka Watanzania waishi maisha bora.”

Padri Shayo aliongeza kuwa tunu za amani na umoja zilikuwa miongoni mwa falsafa kuu ya Mwl. Nyerere, ambapo matokeo yake ni umoja na mshikamano wa Taifa uliopo.

Ibada hiyo ilihudhuriwa na Makamu wa Pili wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Ally Idd, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Bi. Jenista Mhagama, Mke wa Waziri Mkuu Mama Mary Majaliwa.

Wengine ni Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto, Bi. Mauldine Castico, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, Naibu Waziri –OWM (Kazi, Ajira na Vijana), Bw. Anthony Mavunde, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Walemavu, Bi. Stella Alex Ikupa na mwakilishi wa familia ya Mwalimu Nyerere, Bw. Makongoro Nyerere.

 

-ends-

 
Our website is...
 
mod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_counter
mod_vvisit_counterToday39
mod_vvisit_counterYesterday124
mod_vvisit_counterThis week461
mod_vvisit_counterLast week825
mod_vvisit_counterThis month2346
mod_vvisit_counterLast month3455
mod_vvisit_counterAll days513981
Copyrights ©2013, The United Republic of Tanzania, Prime Minister's office All Rights Reserved