Logo
Monday, 16 October 2017 00:00    PDF 

Mawaziri tumieni madaraka yenu kwa manufaa ya Taifa - Waziri Mkuu

*Asisitiza Uwaziri si fursa ya kujitajirisha

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Mawaziri watumie madaraka yao kwa manufaa ya Taifa na kamwe wasiyatumie kama fursa ya kujitajirisha wao binafsi.

Ameyasema hayo leo (Jumatatu, Oktoba 16, 2017) alipozungumza na baadhi ya Mawaziri, Manaibu na Makatibu Wakuu katika kikao kilichofanyika jijini Dar es Salaam.

Amesema Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli amesisitiza kwamba amewateua ili wafanye kazi na kamwe wasitumie madaraka waliyopewa kwa maslahi yao binafsi.

“Madaraka haya ya Uwaziri si fursa ya kujipatia utajiri, tunatakiwa tufanye kazi kwa weledi, uadilifu, bidii na uaminifu mkubwa ili kuondoa kero za wananchi kwa wakati.”

Amewataka Mawaziri na Manaibu Waziri wazingatie Katiba ya nchi, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali ya Serikali katika utekelezaji wa majikumu yao ya kila siku.

Waziri Mkuu amesema Mawaziri hao wanatakiwa wasimamie utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka kuanzia mwaka 2016/2017 hadi 2020/2021. Pia wasimamie utekelezaji wa ahadi zote zilizopo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 pamoja na ahadi alizozitoa Rais Dkt. Magufuli wakati wa kampeni za uchaguzi.

Waziri Mkuu amewaagiza mawaziri wahakikishe wanakwenda kufanya ufuatiliaji wa tathmini ya utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo inayohusu sekta zao na akawataka wakahimize ukusanyaji wa mapato.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amewataka Mawaziri hao wakapunguze urasimu katika utekelezaji wa malengo ya Serikali kwa sababu wananchi wanahitaji kuhudumiwa kwa wakati.

Mawaziri waliohudhuria kikao hicho ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais –TAMISEMI, Bw. Suleiman Jaffo pamoja na Manaibu wake, Bw. Joseph Kandege na Bw. George Kakunda, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Bi Ummy Mwalimu na Naibu wake Dkt. Faustine Ndungulile.

Wengine ni Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe na Naibu wake Bw. Jumaa Aweso, Waziri wa Viwanda na Biashara, Bw. Charles Mwijage na Naibu wake, Mhandisi Stella Manyanya.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla na Naibu wake, Bw. Josephat Hasunga, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako na Naibu wake, Bw. William Ole Nasha, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Bw. Abdallah Ulega pamoja na Makatibu Wakuu wa Wizara hizo.

-ends-

 

 
Our website is...
 
mod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_counter
mod_vvisit_counterToday39
mod_vvisit_counterYesterday124
mod_vvisit_counterThis week461
mod_vvisit_counterLast week825
mod_vvisit_counterThis month2346
mod_vvisit_counterLast month3455
mod_vvisit_counterAll days513981
Copyrights ©2013, The United Republic of Tanzania, Prime Minister's office All Rights Reserved