Logo
Friday, 15 September 2017 00:00    PDF 

HOTUBA YA MHESHIMIWA KASSIM M. MAJALIWA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WAKATI WA KUAHIRISHA MKUTANO WA NANE WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,

TAREHE 15 SEPTEMBA, 2017 - DODOMA

UTANGULIZI

1. Mheshimiwa Spika, tarehe 5 Septemba, 2017 tulianza kikao cha kwanza cha mkutano wa nane wa Bunge lako tukufu na leo tunafikia tamati. Ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kuhitimisha shughuli zote zilizopangwa kwa amani, salama, tukiwa na afya na uzima.

2. Mheshimiwa Spika, Napenda kutumia nafasi hii ya awali kukupongeza Mheshimiwa Spika, kwa hekima, busara na uwezo mkubwa wa kuliongoza Bunge hili ukisaidiwa na Mheshimiwa Naibu Spika na Wenyeviti wa Bunge. Waheshimiwa Wabunge watakubaliana nami kwamba kwa mara nyingine ushuhuda huu ni dhahiri na umejidhihirisha wazi katika kikao hiki ambapo mmeongoza Bunge hili kwa umahiri mkubwa na kuendelea kuonesha ukomavu wa kisiasa kwa kuwa wavumilivu sana. Vilevile, ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa kazi nzuri pamoja na michango yenu mizuri ya maoni na ushauri tulioupokea wakati wa mijadala ya hoja mbalimbali zilizowasilishwa na Serikali katika mkutano huu.

3. Mheshimiwa Spika, wakati tukiendelea na kikao hiki cha Bunge, wapo baadhi ya waheshimiwa wabunge na wananchi tunaowawakilisha katika majimbo yetu walipata misiba ya ndugu, jamaa na marafiki. Nitumie nafasi hii kuwapa pole wote waliofikwa na misiba hiyo. Aidha, kama ambavyo wote tunakumbuka mnamo tarehe 7 Septemba, 2017 tulipata taarifa ya tukio la kusikitisha lililotokea hapa Dodoma la mashambulizi na kupigwa risasi kwa Mbunge mwenzetu, Mheshimiwa Tundu Antipas Lissu (Mbunge wa Singida Mashariki). Naungana na Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Mawaziri na Wabunge pamoja na wananchi mbalimbali kwa kumpa pole kwa majeraha na maumivu makubwa aliyoyapata, tunamwombea apone haraka na kurejea kuungana na familia yake, pia nasi kwa shughuli za hapa bungeni.

4. Mheshimiwa Spika, Nitumie nafasi hii kuungana na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoa pole nyingi kwa Meja Jenerali Mstaafu Vicent Mritaba kutokana na tukio la kushambuliwa kwa risasi Jumatatu ya tarehe 11 Septemba, 2017 nyumbani kwake ambaye bado anaendelea na matibabu kwenye hospitiali ya Lugalo.

Serikali inalaani vitendo hivyo na matukio hayo ya kinyama. Ni mwezi na nusu sasa tumeanza kuanza utulivu kufuatia vifo vya raia na askari wetu wa Jeshi la Polisi waliouawa kikatili huko maeneo ya Mbagala - Dar es Salaam, Mkuranga, Rufiji na Kibiti, mkoa wa Pwani. Nitumie fursa hii kusisitiza kwamba kwa matukio haya Serikali haitafumbia macho na tayari Vyombo vya Dola vimeagizwa kuhakikisha kwamba vinawatafuta kwa mbinu zote wale wote waliohusika katika vitendo hivyo. Nirejee kuwasihi Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote wavute subira wakati Serikali na vyombo vya dola vinashughulikia matukio haya kwa umakini mkubwa. Jambo la msingi ni kwamba kila mmoja wetu adumishe hali ya ulinzi na usalama nchini.

PONGEZI KWA WABUNGE WAPYA

5. Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu, Bunge lako Tukufu liliwaapisha Waheshimiwa Wabunge Wapya Nane wa Viti Maalum walioteuliwa hivi karibuni. Napenda kutumia nafasi hii kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote hao, ambao ni Mhe. Alfredina Apolinary Kahigi (Mb.); Mhe. Kiza Hussein Mayeye (Mb.); Mhe. Nuru Awadh Bafadhili (Mb.); Mhe. Rukia Ahmed Awadh (Mb.); Mhe. Shamsia Aziz Mtamba (Mb.); Mhe. Sonia Jumaa Magogo (Mb.); Mhe. Zainab Mndolwa Amir (Mb.); na Mhe. Rehema Juma Migila (Mb.).

PONGEZI KWA JAJI MKUU WA TANZANIA

6. Mheshimiwa Spika, tarehe 10 Septemba, 2017 Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alimteua Mheshimiwa Jaji Profesa Ibrahim Hamis Juma kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania. Napenda kupitia Bunge lako tukufu nimpongeze Mheshimiwa Profesa Ibrahim Hamis Juma kwa kuteuliwa kuwa Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania. Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kutoa ushirikiano mkubwa kwake katika kuongoza Muhimili wa Mahakama. Aidha, nampongeza Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman kwa kazi kubwa na nzuri aliyofanya katika kipindi chake cha Uongozi wa Muhimili huo, hususan kuweka misingi imara ya Muhimili wa Mahakama.

MASWALI, MISWADA NA MAAZIMIO

7. Mheshimiwa Spika, Katika Mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge wamepata fursa ya kuuliza maswali ya kawaida ya msingi yapatayo 119 na maswali 295 ya nyongeza na kujibiwa na Serikali. Vilevile, Waheshimiwa Wabunge walipata fursa ya kujadili miswada mitatu na maazimio manne. Vilevile, Bunge lako Tukufu lilipokea na kupitisha taarifa ya Kamati ya Sheria ndogo kuhusu uchambuzi wa Sheria ndogo zilizowasilishwa katika Mkutano wa Sita na Mkutano wa Saba wa Bunge.

8. Mheshimiwa Spika, Miswada ya Sheria iliyojadiliwa na kupitishwa na Bunge lako tukufu ni:

(i) Muswada wa Sheria ya Reli wa Mwaka 2017 (The Railways Bill, 2017);

(ii) Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali Na. 3 wa Mwaka 2017 [The Written Laws (Miscellaneous Amendments - No.3), Bill, 2017];

(iii) Muswada wa Sheria ya Madaktari, Madaktari wa Meno na Wataalam wa Afya Shirikishi wa Mwaka 2016. (The Medical, Dental and Allied Health Professions Bill, 2016).

9. Mheshimiwa Spika, Maazimio yaliyowasilishwa na kuridhiwa na Bunge lako Tukufu ni yafuatayo:

(i) Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Amani na Usalama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki; (East African Community Protocol on Peace and Security);

(ii) Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Kuanzisha Kamisheni ya pamoja ya Bonde la Mto Songwe kati ya Tanzania na Malawi (Convention on the Establishment of a Joint Songwe River Basin Commission Between Tanzania and Malawi);

(iii) Azimio la Bunge la Bunge la Kuridhia Itifaki Nyongeza ya Tano ya Mwaka 1994; Itifaki Nyongeza ya Sita ya Mwaka 1999; Itifaki Nyongeza ya Saba ya Mwaka 2004; Itifaki Nyongeza ya Nane ya Mwaka 2008; na Itifaki Nyongeza ya Tisa ya Mwaka 2016 ya Katiba ya Umoja wa Posta Duniani;

(iv) Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba (Intergovernmental Agreement – IGA) baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Uganda kuhusu Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (East Africa Crude Oil Pipeline – EACOP) kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga (Tanzania);

10. Mheshimiwa Spika, napenda kurejea tena kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao mizuri iliyotolewa wakati wa kujadili miswada na maazimio hayo muhimu ambayo yana manufaa mengi kwa nchi yetu. Serikali itafanyia kazi maoni na ushauri uliotolewa.

11. Mheshimiwa Spika. Napenda kuwapongeza na kuwashukuru Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri kwa kazi nzuri na umahiri mkubwa waliouonesha wakati wa kuwasilisha Miswada na Maazimio yaliyojadiliwa katika mkutano huu pamoja na kutoa ufafanuzi mbalimbali katika kujibu hoja za Waheshimiwa Wabunge. Aidha, nimpongeze Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na wataalam wake kwa kazi kubwa na nzuri ya kuandaa kwa wakati maazimio na miswada iliyowasilishwa hapa bungeni.

MWENENDO WA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA SERIKALI 2017/2018

12. Mheshimiwa Spika, katika mkutano wa saba wa Bunge lako tukufu, mwezi Juni, 2017 tulipitisha Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2017/2018 ya jumla ya shilingi trilioni 31.7. Utekelezaji wa Bajeti hiyo ulianza Mwezi Julai, 2017. Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba Serikali inaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa bajeti hiyo na kwa ujumla mwenendo wa utekelezaji unaridhisha.

13. Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka jitihada kubwa za kuimarisha ukusanyaji mapato ya ndani kwa kutumia mifumo ya kielektroniki. Katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Agosti, 2017, Serikali imefanikiwa kukusanya jumla ya shilingi trilioni 2.448. Kati ya mapato hayo, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekusanya kiasi cha shilingi trilioni 2.305, sawa na asilimia 92 ya lengo la kukusanya jumla ya shilingi trilioni 2.492. Serikali inaendelea kuwahamasisha wafanyabiashara watumie mashine za kielektroniki za EFD kulipa kodi stahili na kutoa ushirikiano kwa TRA kwa kulipa kodi kwa hiari bila shuruti.

14. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa matumizi ya Serikali, katika kipindi cha Julai hadi Agosti, 2017, Serikali imetoa jumla ya shilingi trilioni 3.944 zinazotokana na mapato ya ndani na fedha za nje. Kati ya fedha hizo, shilingi trilioni 3.107 ni fedha za matumizi ya kawaida ikijumuisha malipo ya mishahara ya watumishi wa umma na deni la taifa na shilingi bilioni 836.8 zilitolewa na HAZINA kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Katika kipindi hicho cha miezi miwili, Mamlaka za Serikali za Mitaa (Halmashauri zote nchini) zimepelekewa kiasi cha shilingi bilioni 117.558.

15. Mheshimiwa Spika, sehemu ya fedha za matumizi ya maendeleo zilizotolewa na Serikali kwa kipindi cha Julai hadi Agosti, 2017 zinajumuisha kiasi cha shilingi bilioni 351.1 ambazo zimeelekezwa kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya kipaumbele na maeneo muhimu ya huduma za jamii. Baadhi ya miradi ya kipaumbele iliyopewa fedha ni pamoja na miradi ya ujenzi na ukarabati wa barabara kupitia Mfuko wa Barabara (TANROADS na TARURA) - shilingi bilioni 94.439; Mradi wa Nishati ya Umeme Vijijini (REA) - shilingi bilioni 38.411; Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu - shilingi bilioni 30.614, Miradi ya Maji kupitia Mfuko wa Maji - shilingi bilioni 20.740 na Mfuko wa Reli - shilingi bilioni 14.5. Maeneo mengine ni Mradi wa Ufuaji Umeme – Kinyerezi I – Extension - shilingi bilioni 14.702; ununuzi wa chakula cha Taifa kupitia NFRA - shilingi bilioni 5; mradi wa kujenga na kufufua maeneo ya viwanda kupitia SIDO - Shilingi Bilioni 5, Mradi wa ununuzi na ukarabati wa meli za abiria na mizigo, Shilingi Bilioni 24.496; na Shilingi Bilioni 25 kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vitendanishi. Tunaendelea na mradi wa kuimarisha Vituo vya Afya.

16. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutoa fedha zaidi za bajeti kwa miradi ya maendeleo ikiwemo miradi ya kipaumbele kwa kadri tunavyoendelea kuimarisha ukusanyaji wa mapato. Ninawaomba Waheshimiwa Wabunge na Madiwani muendelee kushirikiana na Serikali katika jitihada hizi, hasa kuhamasisha wananchi walipe kodi kwa hiari na mhimize Halmashauri zitumie zaidi mifumo ya kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato.

MABORESHO YA MFUMO WA PLANREP NA FFARS

17. Mheshimiwa Spika, napenda kuwafahamisha Waheshimiwa Wabunge kwamba tarehe 5 Septemba, 2017 nikiwa hapa Dodoma nilipata fursa ya kuzindua mifumo miwili ya kielektroniki inayohusu kuboresha Upangaji Mipango na Bajeti katika Mamlaka za Serikali za Mitaa; na kuimarisha usimamizi wa fedha za Umma katika ngazi za msingi zinazotoa huduma za Elimu na Afya. Mfumo wa Kwanza unahusu kuboresha taratibu za kupanga Mipango, kuandaa Bajeti na kutoa Taarifa kwa upande wa Mamlaka za Serikali za Mitaa unaojulikana kwa lugha ya Kiingereza kama “Planning, Budgeting and Reporting System - PlanRep”; na Mfumo wa Pili unahusu kuboresha taratibu za ukusanyaji mapato, malipo na kutoa taarifa za fedha za Vituo vya Umma vya kutolea huduma za Jamii katika Mamlaka za Serikali za Mitaa; unaojulikana kwa lugha ya Kiingereza kama “Facility for Financial Accounting and Reporting System - FFARS”.

18. Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli - Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania muda wote amekuwa akisisitiza kubana matumizi katika utekelezaji wa shughuli za Serikali; na Waheshimiwa Wabunge watakubaliana nami kwamba kwa muda mrefu huko nyuma, tumekuwa tukitumia muda mrefu na gharama kubwa katika mchakato wa kuandaa na kuwasilisha Mipango na Bajeti za Mamlaka za Serikali za Mitaa; na za mamlaka mbalimbali za Serikali. Vilevile, gharama kubwa zilitumika katika ufungaji wa Hesabu za Mwaka za Halmashauri na Mikoa. Uzinduzi wa mifumo hiyo miwili ya TEHAMA, unaenda sambamba na azma ya Mheshimiwa Rais ya kuhimiza kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na kutumia vizuri rasilimali za umma. Napenda kueleza kwa kifupi manufaa na faida za Mifumo hiyo ya “PLANREP” na Mfumo wa malipo na kutoa taarifa za fedha za vituo vya kutoa huduma, kuwa ni pamoja na:-

Moja: Kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utendaji kazi wa watumishi wa umma hasa katika eneo la mapokezi ya fedha, utunzaji na matumizi ya fedha za umma. Hii ni kuanzia katika vituo vya kutolea huduma za elimu na afya vilivyopo vijijini (hususan vituo vya afya, zahanati na shule za msingi na sekondari) hadi katika ngazi ya Halmashauri;

Mbili: Kuimarisha usimamizi wa mapato na matumizi sahihi ya fedha za umma katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, kwa kuzingatia Mkakati wa Serikali ya Awamu ya Tano wa Serikali Kuu kupeleka fedha za matumizi ya kawaida na shughuli za maendeleo moja kwa moja katika vituo vya kutolea huduma za jamii ikiwemo elimu na afya;

Tatu: Kupunguza na kuokoa wastani wa takriban shilingi bilioni 4 kila mwaka zilizokuwa zinatumika kwa ajili ya zoezi zima la kufanya maandalizi na mchakato wa kuandaa mipango na bajeti kuanzia ngazi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa hadi Taifa. Gharama hizo zilijumuisha kuandaa machapisho mbalimbali, nauli, mafuta pamoja na posho za kujikimu kwa watumishi wanaoshiriki kuandaa mipango na bajeti za Halmashauri.

19. Mheshimiwa Spika, kufuatia kukamilika kwa mifumo hii miwili, sasa ni wajibu wa kila mkoa, kila halmashauri na vituo vya kutolea huduma za elimu na afya katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kutoa taarifa ya mapato na matumizi kwa wadau husika na mamlaka zinazohusika. Vilevile, ngazi zote za Mamlaka za Serikali za Mitaa lazima zitoe taarifa za mapato na matumizi kwa wananchi wanaowahudumia kupitia mikutano, mbao za matangazo, tovuti zao, vyombo vya habari na njia nyinginezo;

20. Mheshimiwa Spika, lengo la Serikali la kutumia mifumo ya TEHAMA ni kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utendaji kazi wa shughuli za Serikali. Hivyo, ni muhimu mifumo iliyozinduliwa itumike kwa ufasaha ili kuleta tija inayotarajiwa na isitumike kukwamisha shughuli za Serikali au mipango ya utoaji huduma kwa wananchi.

21. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuwaomba Waheshimiwa Wabunge na Madiwani washirikiane na Serikali kufuatilia utekelezaji wa mifumo hii miwili ili ilete tija na ufanisi, hasa katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri; na kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili fedha zilizotengwa zitumike ipasavyo; na ubora na thamani ya miradi inayotekelezwa katika Halmashauri iwiane na thamani ya fedha (yaani value for money); zilizotolewa na Serikali.

22. Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa hii kuishukuru Serikali ya Marekani ambayo imetoa mchango mkubwa wa fedha katika kusaidia kuboresha mifumo hiyo miwili kupitia Mradi wa Kuimarisha Mifumo ya Sekta ya Umma (Public Sector System Strengthening – PS3). Aidha, kipekee niwashukuru wataalam wetu wa ndani kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI na wataalam kutoka Wakala wa Serikali Mtandao pamoja na watendaji wa ndani wa mradi wa kuimarisha Mifumo ya Sekta ya Umma (PS3); kwa kufanikiwa kutengeneza mifumo hii maalum ya kuandaa Mipango na Bajeti kwa ajili ya Mamlaka za Serikali za Mitaa; na ule wa usimamizi wa fedha za Serikali katika ngazi za msingi zinazotoa huduma za elimu na afya. Mifumo hii imebuniwa na Watanzania. Tunawashukuru na kuwapongeza sana wataalam wetu Watanzania wazalendo kwa ubunifu wao na umahiri waliouonesha katika kuboresha mifumo hii miwili.

USIMAMIZI WA SEKTA YA MADINI

23. Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kwamba yamekuwepo malalamiko kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge, Wananchi na Asasi mbalimbali wakionesha kutoridhishwa kwao na mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa na usimamizi wa Serikali katika Sekta hiyo. Aidha, yapo malalamiko kuwa Taifa letu limekuwa halinufaiki ipasavyo na Sekta hii kwa sababu mikataba iliyopo haitoi fursa kwa Serikali kupata gawio la kutosha, kupata kodi na mapato mengine mbalimbali yanayotokana na shughuli za uchimbaji wa madini zinazofanywa na makampuni yaliyopo nchini.

24. Mheshimiwa Spika, Kupitia Ilani ya Uchaguzi wa CCM ya Mwaka 2015 ilitamka wazi kuwa itashughulikia kelo ya umiliki wa rasilimali za Nchi na Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amesimamia vilivyo. Katika kuyapatia ufumbuzi matatizo hayo, Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walijadili na kupitisha Miswada miwili ambayo ni Mswada wa Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu masharti hasi katika Mikataba ya Maliasili za Nchi, na pili ni Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Nchi kuhusiana na Umiliki wa Maliasili ya Mwaka 2017.

25. Mheshimiwa Spika, miongoni mwa mambo yaliyomo katika miswada hiyo ni pamoja na ushirikishwaji wa wananchi katika umiliki wa rasilimali za nchi, uzuiaji wa usafirishaji wa rasilimali nje ya nchi kabla ya kuongezwa thamani, mashauri kati ya mwekezaji na Serikali kutopelekwa Mahakama za Nje na badala yake kutafutiwa ufumbuzi katika Mahakama za Ndani pamoja na wawekezaji kuhifadhi fedha zao katika Benki za hapa nchini.

Jambo jingine ni pamoja na kadri inavyofaa kwa kulihusisha Bunge juu ya maslahi ya Wananchi katika Mikataba hii.

26. Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa hii kuwapongeza Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uamuzi wao thabiti na wa kizalendo kwa kuzipitisha sheria hizi kwa manufaa ya Taifa na Wananchi kwa ujumla. Serikali kwa upande wake imeanza utekelezaji wa usimamizi wa rasilimali hizi kwa kuzingatia maslahi ya Taifa.

Aidha, naomba nitumie fursa hii kuwaomba Watanzania waunge mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano katika kuhakikisha kuwa Watanzania na Taifa kwa ujumla wananufaika ipasavyo na rasilimali za nchi yao.

SEKTA YA KILIMO

JITIHADA ZINAZOCHUKULIWA NA SERIKALI KUIMARISHA UZALISHAJI WA MAZAO MAKUU MATANO YA BIASHARA NCHINI

27. Mheshimiwa Spika, naomba uniruhusu nitumie nafasi hii kueleza kwa kifupi jitihada za Serikali ya awamu ya Tano na maelekezo mahsusi ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuimarisha usimamizi katika uzalishaji na uuzaji wa mazao makuu matano ya awali ya biashara hapa nchini. Maelekezo na jitihada hizi zina lengo la kuwawezesha wakulima wetu wengi wa vijijini ambao ni takriban asilimia 75 ya Watanzania wote, kulima kilimo cha kisasa, chenye tija na cha kibiashara ili kuwawezesha kuondokana na umaskini. Vilevile, kuwawezesha wakulima kupata mbinu za kisasa za kuyafikia masoko ya uhakika ya mazao yao ili kupata bei nzuri na itakayowaongezea kipato.

28. Mheshimiwa Spika, ili kutekeleza azma hiyo, Serikali imeamua kuanza kwa kuweka mkazo wa kuyaendeleza kwa kasi mazao makuu matano ya biashara yakiwemo pamba, tumbaku, korosho, chai na kahawa. Mazao haya ni muhimu sana katika kuwezesha mkakati wa Serikali ya Awamu ya Tano wa kufikia uchumi wa viwanda. Mazao haya ndiyo mhimili wa kutoa malighafi za kuendesha viwanda husika na yana mnyororo mpana wa uzalishaji ambao una fursa ya kutoa ajira nyingi. Mazao mengine ya kibiashara ambayo yatawekewa mkazo ni katani, ufuta, alizeti, mbaazi, ngano n.k.

29. Mheshimiwa Spika, pamoja na fursa kubwa tuliyo nayo ya kuendeleza mazao hayo, kwa kipindi kirefu uzalishaji wa mazao hayo makuu ya biashara ulishuka. Kushuka huko kulitokana na changamoto kadhaa zikiwemo kupungua tija katika uzalishaji, baadhi ya wakulima kuacha kulima mazao hayo kutokana na wakulima kukatishwa tamaa na viongozi wa vyama vyao vya ushirika kutotekeleza vyema wajibu wake wizi, dhuluma kwa wakulima na pia ushiriki mdogo wa maafisa kilimo katika kusimamia kilimo cha kitaalam.

30. Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na changamoto hizo, Serikali ya Awamu ya Tano imeweka kipaumbele cha kuzipatia ufumbuzi ili kuongeza uzalishaji na kukuza kipato cha mkulima. Moja ya hatua zinazochukuliwa na Serikali ni kuyasimamia mazao hayo moja kwa moja kupitia maafisa kilimo na Bodi za Mazao hayo. Serikali itahakikisha kuwa kila taasisi iliyopewa dhamana ya kusimamia mazao hayo, inatekeleza majukumu yake ipasavyo sambamba na kuhakikisha kwamba watendaji wake wanatekeleza majukumu yao kwa uadilifu na ufanisi mkubwa.

VYAMA VIKUU NA VYAMA VYA MSINGI VYA MAZAO

31. Mheshimiwa Spika, hivi karibuni Serikali imefanya uchunguzi ili kubaini changamoto zinazosababisha kupungua kwa uzalishaji wa mazao haya matano ya biashara. Matokeo ya uchunguzi huo yanaonesha kwamba, huduma zisizoridhisha za ugani na utafiti, ukosefu wa pembejeo bora, uwingi wa vyama vya msingi na vyama vikuu vinachangia kuzorota kwa kilimo cha mazao hayo. Kwa muda mrefu vyama vingi vya ushirika wa mazao viligubikwa na (i) ubadhirifu unaofanywa na baadhi ya viongozi wa vyama hivyo; (ii) Kuyumba kwa bei kwenye soko la dunia; na (iii) Bodi za Mazao kushindwa kusimamia kikamilifu uendelezaji wa mazao husika na badala yake wamewaachia wenye makampuni binafsi waendeleze mazao hayo.

32. Mheshimiwa Spika, pamoja na kusimamia mazao hayo, ziko jitihada zinaendelea za kuboresha mazao mengine ya kibiashara na chakula. Moja ya jitihada inayoendelea sasa ni kutafuta masoko ya mazao ambayo hayajanunuliwa kama vile tumbaku ipatayo tani zaidi ya 22,441; mbaazi ambazo hazijanunuliwa na zimeshuka bei; chai ambayo ina migogoro katika Wilaya za Rungwe na Lushoto. Mazao haya yameshuka bei kutokana na kushuka kwa bei kwenye soko la dunia. Hata hivyo, Serikali inafanya jitihada za kutafuta masoko kwenye nchi hitaji. Hivyo wakulima wavute subira.

MFUMO WA UNUNUZI WA MBOLEA KWA PAMOJA

33. Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza kutekeleza mfumo wa kuwawezesha wakulima kupata mbolea kwa gharama nafuu kwa kuagiza kwa pamoja kwa njia ya zabuni. Njia hii itashusha bei kutoka ya awali ya mfuko uliokuwa unauzwa kati ya sh. 70,000 - 100,000 na sasa utapatikana kwa kati ya sh. 53,000 - 60,000/.

34. Mheshimiwa Spika, ni matumaini yetu kuwa kila mmoja atamudu kupata mbolea. Mbolea hizo zimeanza kuingia nchini tayari kwa kusambazwa na Serikali imeendelea kusimamia kuhakikisha mkulima ananufaika na mazao yake. Hata hivyo, Serikali imeweka mkazo ufuatao ili kukuza sekta ya kilimo:-

(i) Maafisa Kilimo (W), Maafisa Ugani Kata na Vijiji wasimamie mazao katika maandalizi ya mashamba na masoko.

(ii) Kumfikishia mkulima pembejeo ikiwemo mbolea na mbegu kwa wakati.

(iii) Kusimamia ushirika wa wakulima.

(iv) Masoko ya mazao kwa kuondoa tozo zisizo na tija, mazao yote kununuliwa kwa fedha za Kitanzania, kwa mfano: zao la tumbaku kuanzia msimu ujao litanunuliwa kwa fedha za Kitanzania badala ya Dola za Marekani.

(v) Kupunguza vyombo/taasisi zinazosimamia mazao ili kuondoa mkanganyiko wa utoaji huduma.

(vi) Kusimamia mifumo ya masoko yake na kupambana na wanunuzi nje ya mifumo iliyokusudiwa. Kwa mfano, zao la korosho (kangomba) na zao la tumbaku (vishada). Mifumo hiyo kwa sasa haina nafasi.

SEKTA YA ELIMU

35. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2017/2018 Serikali imeendelea na mpango wa kutoa elimu bila malipo kwa kupeleka fedha moja kwa moja katika shule za umma za msingi na sekondari. Kiasi cha fedha kinachopelekwa shuleni kwa ajili ya kugharamia elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari ni jumla ya shilingi bilioni 23.868 kwa mwezi. Kiwango hicho kimeongezeka kutokana na mafanikio yaliyopatikana katika mwaka wa kwanza wa sera ya elimu bila malipo ambapo kulikuwa na ongezeko kubwa la udahili wa wanafunzi wa darasa la kwanza, kidato cha kwanza na cha tano pamoja na ongezeko la wanafunzi wa shule za umma za bweni.

36. Mheshimiwa Spika, natoa wito kwa viongozi wa mikoa, wilaya na halmashauri kuhakikisha kuwa fedha za kugharamia elimu bila malipo zinatumika vizuri na kwa madhumuni yaliyokusudiwa. Waheshimiwa Wabunge mkiwa Viongozi na Madiwani kwenye Halmashauri zenu mnaombwa kuiunga mkono Serikali kwa kufuatilia utekelezaji wa sera hii hususan ufuatiliaji wa matumizi ya fedha hizo kwenye Halmashauri zenu na kote nchini. Nawasihi wazazi waendelee kuandikisha shule kila mtoto anayestahili kujiunga na elimu ya awali na darasa la kwanza.

UCHAGUZI WA WANAFUNZI WA KIDATO CHA TANO MWAKA 2017/2018

37. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2017/2018, jumla ya wanafunzi 93,019 walikuwa na sifa za kujiunga na kidato cha tano. Kati ya wanafunzi hao, wanafunzi 71,987 sawa na asilimia 77.4 walichaguliwa katika awamu ya kwanza na ya pili ili kujiunga na kidato cha tano mwaka huu. Majina ya wanafunzi waliobaki yamewasilishwa Baraza la Ufundi la Taifa (National Council for Technical Education - NACTE) ili wapangiwe katika vyuo vya ufundi.

38. Mheshimiwa Spika, napenda kuwahamasisha wananchi waendelee kujitolea kwa hali na mali kujenga shule za kidato cha tano na sita ili kuongeza idadi ya wanafunzi wanaojiunga na vidato hivyo. Aidha, ni vema kipaumbele kiwekwe kwenye shule za bweni ili kuwawezesha wanafunzi kujifunza kwa usalama na kupata malezi bora. Serikali inaendelea kuzifanyia kazi changamoto zilizojitokeza katika upangaji wa wanafunzi kwenye shule za bweni. Kama ilivyodokezwa na Waheshimiwa Wabunge katika michango mbalimbali hapa Bungeni. Lengo ni kuhakikisha nafasi zilizopo katika shule zote za bweni zinatumika ipasavyo.

SEKTA YA AFYA

UPATIKANAJI WA DAWA, VIFAA, VIFAA TIBA NA VITENDANISHI

39. Mheshimiwa Spika, hali ya upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini imeendelea kuimarika, ambapo, kati ya Julai na Agosti 2017, kiwango cha upatikanaji wa dawa katika Bohari ya Dawa kimeongezeka hadi kufikia asilimia 82 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 50 kwa kipindi cha mwaka 2016/17. Aidha, kiwango cha upatikanaji wa dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya kimeongezeka hadi kufikia asilimia 90 kutoka asilimia 60 katika mwaka wa fedha 2016/2017.

40. Mheshimiwa Spika, mafanikio haya yanatokana na Serikali kuongeza mgao wa fedha katika sekta ya afya nchini kutoka shilingi trilioni 1.988 mwaka 2016/2017 hadi kufika shilingi trilioni 2.222 mwaka 2017/2018. Ongezeko hili ni sawa na asilimia 11.77. Aidha, bajeti ya dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi imeongezeka kutoka shilingi bilioni 31 mwaka 2015/16 hadi kufikia shilingi bilioni 269 mwaka 2017/18. Aidha, mafanikio haya pia yametokana na Bohari ya Dawa kuanza kununua dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji badala ya washitiri wa kati waliokuwa wanauza bidhaa hizo kwa gharama kubwa.

Vituo vya kutolea huduma za afya kuwa na vifaa vya kutosha.

41. Mheshimiwa Spika, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliahidi kuwa, Serikali itahakikisha kila kituo cha kutolea huduma za afya nchini kinakuwa na vifaa vya kutosha ili kuweza kutoa huduma bora kwa wananchi.

42. Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa ahadi hii ulianza mwezi Aprili 2017, ambapo Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ilianza kusambaza vitanda ishirini (20) vya kawaida, vitanda vitano (5) vya kujifungulia, magodoro ishirini na tano (25) na mashuka hamsini (50) katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

43. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Agosti 2017, Serikali imekamilisha usambazaji wa vifaa vifuatavyo: jumla ya vitanda 3,208 katika Halmashauri 162, magodoro 3,189 katika Halmashauri 160, mashuka 7,570 katika Halmashauri 159 na jumla ya vitanda 322 vya kujifungulia katika Halmashauri 69 nchini.

44. Mheshimiwa Spika, usambazaji wa vifaa hivyo umekamilika kwa asilimia 85. Serikali inaendelea na zoezi la usambazaji wa vifaa hivyo na kukamilisha kazi hii katika kipindi kifupi iwezekanavyo ili kuwawezesha wananchi kupata huduma bora za afya pindi wanapozihitaji. Jambo la msingi kwa watendaji katika ngazi mbalimbali ni kuhakikisha katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya vinavyomilikiwa na Serikali na akinamama wajawazito wanapata matibabu bure.

UWEZESHAJI VIJANA

45. Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012, asilimia zaidi ya 35 ya Watanzania ni vijana na hivyo Serikali imeamua kuandaa mpango wa kuwekeza kwao ili nguvu kazi hii iweze kuchangia kikamilifu katika kujenga uchumi wa Taifa kupitia Mpango wa Kutathmini na Kurasimisha Ujuzi uliopatikana nje ya Mfumo Rasmi wa Mafunzo. Jumla ya vijana 1,000,000 wamelengwa kupata urasimishaji ujuzi kati ya mwaka 2017 na 2021. Hadi sasa vijana kadhaa wanaendelea kunufaika na mpango huu kutoka mikoa mbalimbali.

Miongoni mwa faida za programu hii ni pamoja na kuwasaidia mafundi waliojifunza kupitia sehemu za kazi kupata kazi zenye staha na kuwajengea uwezo wa kushiriki na kushindana kikamilifu katika soko la ajira, lakini pia kuinua tija mahali pa kazi na kusaidia waajiri/wenye makampuni kukidhi viwango katika eneo la rasilimali watu.

Mpango huu unafadhiliwa kwa asilimia 100 na Serikali na unatekelezwa kwa pamoja na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi – VETA.

SEKTA YA BARABARA

KUANZISHWA KWA WAKALA WA BARABARA ZA VIJIJINI NA MIJINI

(Tanzania Rural and Urban Roads Agency-TARURA)

46. Mheshimiwa Spika, Sote tunatambua kilio kikubwa na cha muda mrefu kilichotolewa na wadau mbalimbali wa Mamlaka za Serikali za Mitaa wakiwemo Waheshimiwa Madiwani, Waheshimiwa Wabunge, Wakuu wa Mikoa na wananchi na wadau wa sekta ya barabara kuhusu umuhimu wa kuwa na Wakala wa Barabara Vijijini. Aidha, Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015 katika Ibara ya 39 (a) (iii) (Ukurasa wa 54) inaielekeza Serikali kuanzisha Wakala/Taasisi itakayosimamia kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara za Halmashauri, Miji na Majiji ambazo ziko chini ya TAMISEMI ifikapo mwaka 2020;

47. Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Bunge lako tukufu kuwa tayari Serikali imeunda Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini unaojulikana kwa lugha ya Kiingereza kama Tanzania Rural and Urban Roads Agency- TARURA. Tarehe 2 Julai, 2017 nilipata fursa ya kuuzindua rasmi Wakala huo hapa mjini Dodoma. Wakala huu umeanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Wakala za Serikali (Sura 245) na ulitangazwa rasmi katika Gazeti la Serikali Na.211 la tarehe 12 Mei, 2017.

48. Mheshimiwa Spika, TARURA imeanzishwa rasmi ikiwa ni jitihada za Serikali za kuimarisha Sekta ya Barabara za Miji na Vijijini. Aidha, Uzinduzi wa Wakala huu ni kielelezo cha dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kuboresha maisha ya wananchi hususan waishio vijijini. Majukumu ya Wakala ni ujenzi, ukarabati na matengenezo ya madaraja na barabara za Vijijini na Mijini zilizokuwa zikitengenezwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuimarisha usafiri na usafirishaji katika maeneo hayo;

49. Mheshimiwa Spika, kuanzishwa kwa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini kunatarajiwa kuondoa kero zifuatazo:

· Barabara za Halmashauri kujengwa chini ya kiwango tena kwa kutumia muda mrefu kuliko makubaliano ya kimkataba;

· Tabia ya baadhi ya viongozi na watendaji wasio waadilifu wanaoziibia Halmashauri kupitia kandarasi za ujenzi wa barabara; na

· Migongano ya kimaslahi miongoni mwa baadhi ya Madiwani na watumishi wa Halmashauri katika kusimamia ujenzi wa barabara za Halmashauri kupitia zabuni zinazosimamiwa na Halmashauri.

50. Mheshimiwa Spika, ni matumaini yangu kuwa TARURA itasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha mtandao wa barabara za vijijini na hivyo kuwawezesha wananchi wengi zaidi kusafiri na kusafirisha bidhaa za mashambani kwa urahisi ndio kichocheo cha ukuaji wa uchumi vijijini. Naomba kutoa rai kwa wadau wote wa barabara nchini wakiwemo viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa wakiwemo Waheshimiwa Wabunge na Madiwani kuusoma Mpango Kazi wa Wakala huo, ili kutoa msukumo katika kuboresha barabara za vijijini na mijini zilizoko kwenye maeneo yao.

51. Mheshimiwa Spika, napenda kulieleza Bunge lako tukufu kuwa, Serikali imepokea hoja ya Waheshimiwa Wabunge ya kupewa ufafanuzi wa kutosha kuhusu majukumu ya TARURA. Hoja hiyo itafanyiwa kazi mapema iwezekanavyo ili kuwawezesha Waheshimiwa Wabunge kuisimamia Serikali vizuri kwenye eneo hili la barabara za Halmashauri nchini.

HITIMISHO

52. Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kuwashukuru tena wote waliosaidia kufanikisha mkutano huu. Shukrani za pekee ni kwako wewe Mheshimiwa Spika pamoja na Naibu Spika kwa kutuongoza vizuri. Aidha, nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yao pamoja na watumishi wote wa Serikali walioisaidia Serikali kujibu maswali na kuwasilisha hoja za Serikali hapa Bungeni.

53. Mheshimiwa Spika, kipekee namshukuru Katibu wa Bunge, Dkt. Thomas Kashilillah pamoja na watumishi wote wa Ofisi ya Bunge kwa kufanikisha mkutano huu. Nawashukuru wale wote waliokuwa na jukumu la ulinzi na usalama ili kuhakikisha mkutano huu unafanyika na kumalizika salama. Napenda pia niwashukuru madereva wote kwa kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi mkubwa.

Nawashukuru pia waandishi wa habari kwa kuhakikisha kuwa habari za hapa bungeni zinawafikia wananchi kwa namna mbalimbali. Mwisho, niwashukuru wananchi wa Dodoma kwa ukarimu wao wa kutupatia huduma zote muhimu na hivyo kukamilisha mkutano huu kwa mafanikio makubwa.

54. Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kutoa hoja kuwa Bunge lako tukufu sasa liahirishwe hadi siku ya Jumanne, tarehe 7 Novemba, 2017 litakapokutana saa 3.00 asubuhi hapa mjini Dodoma.

55. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

 

 
Our website is...
 
mod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_counter
mod_vvisit_counterToday82
mod_vvisit_counterYesterday106
mod_vvisit_counterThis week291
mod_vvisit_counterLast week798
mod_vvisit_counterThis month2448
mod_vvisit_counterLast month3555
mod_vvisit_counterAll days524633
Copyrights ©2013, The United Republic of Tanzania, Prime Minister's office All Rights Reserved