Logo
Friday, 09 February 2018 00:00    PDF 

Akiba ya fedha za kigeni yaongezeka - Majaliwa

*Asema rekodi hiyo haijawahi kufikiwa kwa miaka minne

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema akiba ya fedha za kigeni imeongezeka na kufikia dola za Marekani bilioni 5.91 kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa kwa takriban miaka minne kuanzia mwaka 2013.

Ameyasema hayo leo (Ijumaa, Februari 9, 2018) bungeni mjini Dodoma wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa 10 wa Bunge la 11. Bunge limeahirishwa hadi Aprili 3, mwaka huu.

Waziri Mkuu amesema mbali na kuongezeka kwa akiba ya fedha za kigeni, pia thamani ya mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi ilikuwa takriban dola za Marekani bilioni 8.695 ikilinganishwa na wastani wa dola bilioni 8.828 kwa miaka mitatu iliyopita.

Akielezea mafanikio mengine, Waziri Mkuu amesema kuwa utekelezaji wa bajeti kwa kipindi cha nusu mwaka ni wa kuridhisha ambapo ukusanyaji wa mapato ulifikia sh. trilioni 12.95 sawa na asilimia 82.8 ya lengo lililopangwa katika kipindi hicho.

“Matumizi ya fedha hizo yameelekezwa katika kugharamia shughuli mbalimbali za Serikali za kuhudumia wananchi na miradi ya kipaumbele kama ilivyopangwa na Bunge lako tukufu... na baadhi ya miradi hiyo ni kuanza kwa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha Standard Gauge,” amesema.

Ameitaja miradi mingine kuwa ni kugharamia Mpango wa Elimumsingi Bila Malipo, kugharamia Mpango wa Ununuzi wa Dawa, Vifaa Tiba na Vitendanishi na utekelezaji wa miradi ya usambazaji maji vijijini na mijini na usambazaji wa umeme vijijini kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA).

Miradi mingine ni ununuzi wa meli za abiria na mizigo, ukarabati na ujenzi wa baadhi ya viwanja vya ndege na kuendeleza maeneo ya uwekezaji wa viwanda katika mikoa mbalimbali nchini.

Hakika kwa mafanikio haya, tuna kila sababu ya kumpongeza Rais Dkt. John Magufuli kwa uongozi wake mahiri na juhudi anazofanya za kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma muhimu na maendeleo ya haraka.”

Waziri Mkuu amesema Serikali ya Awamu ya Tano itasimamia utekelezaji wa ahadi zake ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba malengo yaliyowekwa kwa mwaka 2017/2018 yanafikiwa kwa kiwango kikubwa.

Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali itaendelea kuimarisha na kujenga misingi na mifumo imara ya ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kuwe na mapato endelevu kwa ajili ya kugharamia matumizi yake.

“Vilevile, tutahakikisha kuwa tuna usimamizi madhubuti wa ukusanyaji wa mapato ambao utasaidia kupanua wigo na kudhibiti ukwepaji wa kodi kupitia urasimishaji wa shughuli za uchumi kwa kuwezesha ukuaji wa biashara katika sekta ndogo na za kati ambazo ndiyo mihimili wa kuzalisha ajira na kukuza uchumi,” ameongeza.

Akizungumzia kuhusu viashiria mbalimbali vya kiuchumi, Waziri Mkuu amesema vinaonesha kwamba hali ya uchumi ni nzuri na pato la Taifa katika kipindi cha Julai hadi Desemba, 2017 lilikua kwa wastani wa asilimia 6.8.

“Hali hii inaashiria kwamba tuna matarajio makubwa ya kufikia lengo la mwaka la ukuaji wa asilimia 7.0. Sekta zilizochangia kwa kiwango kikubwa katika ukuaji huo ni habari na mawasiliano, uchimbaji madini, biashara, ujenzi na uzalishaji viwandani,” amesema.

-ends-

 

 
Our website is...
 
mod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_counter
mod_vvisit_counterToday82
mod_vvisit_counterYesterday106
mod_vvisit_counterThis week291
mod_vvisit_counterLast week798
mod_vvisit_counterThis month2448
mod_vvisit_counterLast month3555
mod_vvisit_counterAll days524633
Copyrights ©2013, The United Republic of Tanzania, Prime Minister's office All Rights Reserved