Logo
WATOTO WA WAFUGAJI WAGUSWA NA SOKO LA MIFUGO LA KIMKAKATI LONGIDO
Thursday, 22 March 2018 00:00    PDF 

Katika kijiji cha EWORENDEKE, kata ya KIMOKOUWA, Wilayani LONGIDO mkoani ARUSHA, kijiji hicho kipo takriban kilomita 4 kutoka Namanga, mpaka wa Tanzania na Kenya.

Hapo kuna Soko la Kimkakati la mifugo Longido, linalohusika na uuzaji wa  mifugo kutoka mikoa takribani 7 ya hapa nchini Tanzania. Wafugaji huuza mifugo hiyo hapa nchini na nchi za jirani, soko hilo ambalo limejengwa na  Programu ya Miundo mbinu ya Masoko, Uongezaji wa Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini (MIVARF), limekuwa ni neema kwa watoto wa kaya zinazozunguka soko hilo.

Watoto wa wafugaji wa  jamii ya kimaasai ambao ndiyo wanufaika wa soko hilo wameguswa na uwepo wa soko hilo kwa kupata maziwa ya mbuzi bure. Watoto hao hukamua maziwa hayo kutoka kwa mbuzi ambao hufikishwa sokoni hapo muda wa jioni na kusubiri kuuzwa usiku ambapo mnada wa mifugo kwa wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi hufanyika sokoni hapo.

Mratibu wa Kitaifa wa Program ya MIVARF,Walter Swai, amebainisha kuwa tangu Program hiyo ianzishwe kutekelezwa  rasmi mwaka 2011, katika mikoa yote ya Tanzania bara na Zanzibar imekuwa ikichochea faida nyingi, zaidi ya malengo mahususi yaliyokusudiwa na Program ambayo, ni kufanikisha azma ya Serikali ya Tanzania ya kuongeza kipato  kwa wananchi  pamoja na uhakika wa chakula kwa kaya zenye kipato cha chini hususan maeneo ya vijijini.

“’Kuna maeneo tumejenga barabara za vijijini hasa kutoka maeneo ya uzalishaji, lakini tumekuta katika maeneo hayo ardhi imepanda thamani, hivyo hivyo katika soko la Kimkakati Longido  tayari  tunaona hata akina mama  wameanza biashara ya mama lishe lakini na watoto wao wanapata maziwa ya mbuzi bure kwaaajili ya lishe yao” alisema Swai.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa Mifugo wilayani Longido, Saruni Laizer amesema kuwa hayo ni mojawapo ya  manufaa ya soko hilo lililojengwa na Program ya MIVARF, kwani watoto wao wanakuwa na afya bora  kwa  kunywa maziwa ya mbuzi ambayo huyapata bure na kisha huyachemsha na kuyatumia kwa matumizi ya nyumbani.

Soko hilo litawanufaisha wananchi wapatao 14,2000  wa wilayani Longido ambapo asilimia 95 ni wafugaji na wanaojishughulisha na biashara za mifugo, pamoja na kuwa wafugaji ni walengwa wa Program hiyo , walengwa wengine ni wakulima wadogo,  wavuvi na wafanyakazi wa kazi za mikono (artisans), Wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo walioko vijijini.

MIVARF;  ni Programu ya Miundo Mbinu ya Masoko na Huduma za Kifedha Vijijini  iliyobuniwa  na serikali ya Tanzania  kwa  kushirikiana na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo yaani (IFAD) na Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB). Dhumuni la kuanzishwa kwa Programu ya MIVARF ni; Kuboresha miundo mbinu ya masoko, barabara za vijijini, maghala na masoko, Kuwawezesha wananchi waishio vijijini na  kuongeza thamani mazao ya kilimo.

Mwisho.

 
Our website is...
 
mod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_counter
mod_vvisit_counterToday16
mod_vvisit_counterYesterday120
mod_vvisit_counterThis week496
mod_vvisit_counterLast week810
mod_vvisit_counterThis month2993
mod_vvisit_counterLast month3838
mod_vvisit_counterAll days521623
Copyrights ©2013, The United Republic of Tanzania, Prime Minister's office All Rights Reserved