Logo
Tuesday, 20 March 2018 00:00    PDF 

Waziri Mkuu ataka suluhisho la magonjwa yasiyoambukiza barani Afrika

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Mawaziri wa Afya kutoka nchi tisa za Afrika watoe mapendekezo ya namna ya kutokomeza magonjwa yasiyoambukiza kwa Wakuu wa Nchi hizo ili yafanyiwe kazi.

Aliyasema hayo jana jioni (Jumatatu, Machi 19, 2018) wakati akifungua Mkutano wa 65 wa Mawaziri wa Afya kutoka nchi tisa wanachama wa Jumuiya ya Afya kwa nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini (ECSA-HC).

Alisema magonjwa yasiyoambukiza ni miongoni mwa magonjwa ambayo yameendelea kuwatesa wananchi kwa kiasi kikubwa katika nchi nyingi za Bara la Afrika, hivyo ni vema mawaziri hao wakatoa mapendekezo ya namna ya kuyatokomeza.

Waziri Mkuu alisema magonjwa hayo yanaweza kudhibitiwa kwa kuhamasisha wananchi kuboresha lishe na kusisitiza ulaji wa vyakula bora, kufanya mazoezi na kubadili mitindo ya maisha.

“Magonjwa yasiyoambukiza yanaongoza kwa kusababisha vifo katika baadhi ya nchi wanachama wa ECSA. Magonjwa haya yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya mfumo wetu wa lishe na maisha, hivyo ni muhimu suala hili likatafutiwa ufumbuzi.”

Waziri Mkuu alisema magonjwa yasiyoambukiza pamoja na magonjwa mengine ya milipuko kama ebola, homa ya bonde la ufa, dengue, homa ya manjano yamekuwa kikwazo cha maendeleo kwa katika baadhi ya nchi.

Pia, Waziri Mkuu aliongeza kuwa sekta ya afya ni muhimu katika kuboresha maendeleo ya nchi zote iwe ni zilizoendelea au zinazoendelea, hivyo changamoto zote zinazoikabili sekta hazina budi kupewa kipaumbele na kutafutiwa ufumbuzi.

Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Jinsia, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto, Bibi Ummy Mwalimu alisema malengo ya mkutano huo ni kuzungumzia changamoto mbalimbali zinazohusu sekta ya afya na kuyapatia ufumbuzi.

Mkutano huo ulihudhuriwa na Mawaziri wa Afya kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afya kwa nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini ambazo ni Tanzania, Malawi, Lesotho, Uganda, Kenya, Rwanda, Zambia, Zimbabwe na mwakilishi kutoka nchini Mauritius.

Pia ulihudhuriwa na Katibu wa Jumuiya hiyo, Profesa Yoswa Dambisya, mwakilishi wa Benki ya Dunia, Dk. Paolo Belli pamoja na wadau wa sekta ya afya kutoka nchi hizo.

-ends-

 

 
Our website is...
 
mod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_counter
mod_vvisit_counterToday16
mod_vvisit_counterYesterday120
mod_vvisit_counterThis week496
mod_vvisit_counterLast week810
mod_vvisit_counterThis month2993
mod_vvisit_counterLast month3838
mod_vvisit_counterAll days521623
Copyrights ©2013, The United Republic of Tanzania, Prime Minister's office All Rights Reserved