Logo
Sunday, 08 April 2018 00:00    PDF 

Waziri Mkuu awataka Mabalozi watangaze vivutio vya uwekezaji

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nchi za Urusi na Rwanda watumie fursa hiyo kutangaza vivutio vilivyopo nchini ili kuvutia wawekezaji kwenye sekta mbalimbali ikiwemo ya utalii.

Pia amewataka mabalozi hao kila mwisho wa mwaka, wajifanyie tathmini ya mafanikio waliyoyapata kutokana na uwakilishi wao katika mataifa ya nje na wajihoji ni kwa kiasi gani wamechangia kwenye uboreshaji wa maendeleo ya Taifa.

Ametoa maagizo hayo leo (Jumapili, Aprili 8, 2018) wakati akizungumza na Balozi Ernest Mangu anayeiwakilisha Tanzania nchini Rwanda na Balozi Simon Mumwi anayeiwakilisha Tazania nchini Urusi, ofisini kwake mjini Dodoma.

Waziri Mkuu amesema Tanzania ina vivutio vingi vya utalii ikiwa ni pamoja na uwepo wa mbunga za wanyama, hivyo ni vyema wanapoondoka wachukue nyaraka zote zitakazowasaidia kutangaza vivutio vya utalii ili kuongeza idadi ya watalii wanaokuja nchini.

Amesema mbali na kutangaza sekta ya utalii, pia watafute wawekezaji kwenye sekta nyingine kama vile madini, viwanda na kutafuta masoko ili wafanyabiashara na wakulima wa Tanzania waweze kuuza bidhaa zao nje ya nchi.

“Pia mkajifunze mbinu ambazo wenzetu wanazitumia kuboresha sekta mbalimbali ambazo na sisi tunazo hapa nchini kama za viwanda na kisha mje mtueleze namna ya kuziboresha. Kujifunza ni jambo zuri, hivyo msisite kufanya hivyo huko mwendako.”

Pia Waziri Mkuu amewataka mabalozi hao wakawatambue na kuwaunganisha Watanzania waishio kwenye nchi wanakoiwakilisha Tanzania ili nao washiriki kwenye ujenzi wa uchumi wa viwanda na wawasisitize wafuate sheria za nchi wanazoishi lakini wasisahau nyumbani.

Waziri Mkuu amewasisitiza mabalozi hao waende kupunguza gharama za uendeshaji wa Balozi zao kwa kuzuia matumizi katika mambo yasiyo ya lazima. “Pia maslahi ya nchi lazima mkayasimamie huko mwendako hasa katika masuala ya kiuchumi.”

Kwa upande wao, mabalozi hao wamesema watahakikisha wanayafanyia kazi maelekezo yote waliyopewa na Waziri Mkuu ikiwa ni pamoja na kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na nchi wanazoziwakilisha.

-ends-

 

 
Our website is...
 
mod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_counter
mod_vvisit_counterToday16
mod_vvisit_counterYesterday120
mod_vvisit_counterThis week496
mod_vvisit_counterLast week810
mod_vvisit_counterThis month2993
mod_vvisit_counterLast month3838
mod_vvisit_counterAll days521623
Copyrights ©2013, The United Republic of Tanzania, Prime Minister's office All Rights Reserved