Logo

 

Tarehe Mosi Desemba kila mwaka huadhimishwa Siku ya UKIMWI Duniani. Katika ngazi ya kitaifa mwaka huu maadhimisho haya yatafanyika jijini Dar es Salaam Kuanzia tarehe 25 Novemba 2013 na kufikia kilele chake tarehe 1 Desemba 2013.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi kwenye kilele cha maadhimisho haya yatakayotanguliwa na matukio mbalimbali ikiwemo Maonyesho ya Shughuli za wadau wa udhibiti UKIMWI Nchini yatakayofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja Mkoani Dar es Salaam kuanzia tarehe 25 Novemba 2013.

Vilevile kutakuwa na kongamano la kitaifa la kutathmini hali na mwelekeo wa udhibiti UKIMWI nchini litakalofanyika tarehe 27 na 28 Novemba 2013 kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam na Uzinduzi wa Mkakati wa Tatu (3) Taifa wa Kudhibiti UKIMWI.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inaendelea kuwa “TANZANIA BILA MAAMBUKIZI MAPYA YA VVU; VIFO VITOKANAVYO NA UKIMWI NA UNYANYAPAA INAWEZEKANA”. Kauli mbiu hii inalenga kutoa msukumo wa utekelezaji wa mikakati ya kudhibiti UKIMWI kitaifa na kimataifa ili kufikia azma ya sifuri tatu (3) yaani maambukizi mapya sifuri, vifo sifuri na unyanyapaa sifuri ifikapo mwaka 2015. Kauli mbiu hii inahimiza utekelezaji wa dhati wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia (Millennium Development Goals-MDGs) na maazimio yaliyowekwa kwenye Mkutano Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu UKIMWI uliofanyika mwaka 2001 Jijini New York, Marekani.

Wageni mbalimbali watashiriki katika maadhimisho haya ya kitaifa ikiwa ni pamoja na Mawaziri, Mabalozi wa nchi mbalimbali hapa nchini, Wawakilishi wa Mashirika ya Umoja wa Kimataifa, Wadau wa maendeleo na Viongozi mbalimbali wa Kitaifa na wa Mikoa ya jirani, Viongozi wa Dini n.k.

Tunapenda kutoa wito kwa wananchi katika ngazi mbalimbali ikiwa ni pamoja na sehemu za kazi, makanisani, misikitini, mashuleni, na katika jumuia zetu mbalimbali kuadhimisha siku hii kwa njia mbalimbali kama vile Makongamano, Kumbukumbu za Wapendwa wetu waliofariki kwa UKIMWI, Midahalo, Mikutano ya wazi, Vipindi kupitia vyombo vya habari, Kutembelea na kutoa misaada kwa yatima na wagonjwa wa UKIMWI, Kuzima mishumaa nk.

Siku ya UKIMWI Duniani iliasisiwa  rasmi na Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) mwaka 1998 na imeendelea kuadhimishwa kila mwaka ifikapo Desemba mosi kwa uratibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na UKIMWI (UNAIDS).

Maadhimisho haya hutoa fursa ya kutathmini hali halisi na mwelekeo wa udhibiti wa UKIMWI na vilevile kubaini changamoto, mafanikio na mikakati mbalimbali katika kupambana na janga hili. Siku hii pia hutoa nafasi ya kuwakumbuka wale wote waliopoteza maisha yao kutokana na janga la UKIMWI na kuwajali yatima waliotokana na janga hili. Katika ngazi ya kitaifa siku hii huadhimishwa kwa mzunguko katika mikoa yote ya Tanzania Bara na mwaka jana iliadhimishwa kitaifa mkoani Lindi.

Mwaka huu Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) na Uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam wameratibu maadhimisho haya kitaifa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.

 

WOTE MNAHIMIZWA KUADHIMISHA MAONYESHO HAYA KATIKA MAENEO YENU

 

“TANZANIA BILA MAAMBUKIZI MAPYA YA VVU, VIFO VITOKANAVYO NA UKIMWI NA UBAGUZI NA UNYANYAPAA INAWEZEKANA”

 

TUNAWATAKIA MAADHIMISHO MEMA YA SIKU YA UKIMWI DUNIANI MWAKA 2013

 
Our website is...
 
mod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_counter
mod_vvisit_counterToday81
mod_vvisit_counterYesterday106
mod_vvisit_counterThis week290
mod_vvisit_counterLast week798
mod_vvisit_counterThis month2447
mod_vvisit_counterLast month3555
mod_vvisit_counterAll days524632
Copyrights ©2013, The United Republic of Tanzania, Prime Minister's office All Rights Reserved